Kila mara Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetamba kwamba ndicho baba wa mageuzi nchini Tanzania.
Kinasema kuwa mwaka 1992, licha ya asilimia 80 ya Watanzania kutaka Taifa letu liendelee kuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa, ndicho kilichopindua maoni hayo na kukubali yale ya asilimia 20 ya Watanzania na hatimaye kukarejeshwa mfumo wa siasa ya vyama vingi.
Tulidhani kwa tambo hizo, CCM ingekuwa ya kwanza kuonyesha dhamira ya kweli ya kukubaliana na matokeo ya siasa za ushindani. Kinyume chake, chama hicho kikongwe barani Afrika sasa kinatia aibu. Kinalazimisha mambo ambayo ni aibu.
Haya mambo yaliyoanzia kwenye umeya wa manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni, na hatimaye kwenye uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam, si tu kwamba kinaashiria uhuni wa kisiasa, bali pia ni dalili ya uvunjifu wa amani katika nchi yetu.
CCM walipoingia kwenye ushindani wa vyama vingi walipaswa waheshimu uamuzi wa wapigakura. Mara zote CCM imekuwa ikiongoza manispaa na majiji kwa sababu wapigakura ndivyo walivyoamua na vyama vya upinzani havikufanya mizengwe kukwamisha au kuharibu uchaguzi wa mameya.
Iweje sasa baada ya wapigakura kuamua kuwachagua wagombea wa vyama vya upinzani CCM ione nongwa? Kwanini CCM wanataka wao ndiyo wapate kila kitu kwa asilimia 100? Kama ni chanzo cha matatizo, kwanini wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM wasianze kutimuana kuanzia kata hadi mkoa kwa kushindwa kukipa ushindi chama chao?
Haya mambo yanayofanywa sasa na CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam juu ya uchaguzi wa mameya tunakosa maneno sahihi ya kuyatumia, isipokuwa ni kusema huu ni uhuni wa kisiasa ambao watu wastarabu lazima waupinge.
Ni uhuni kwa sababu haiwezekani CCM wautafute ushindi kwa nguvu kwa kuwapeleka madiwani na wabunge ambao inajulikana dhahri kuwa si wakazi wa maeneo husika? Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene, alishalitolea maelezo jambo hili kisheria. Tulidhani CCM wangekuwa wasikivu na kukubali yaishe.
Badala yake kauli ya Waziri ambayo kimsingi ni kauli ya Rais, imeendelea kupuuzwa kwa namna inayotia shaka.
Tanzania sharti ijitofautishe na mataifa mengine ya Afrika. Kulazimisha au kung’ang’ania kutawala si hulka nzuri kwa mustakabali wa Taifa letu. Haya yanayofanywa na CCM sasa ni mwanzo wa chuki na hatima yake ni uvunjifu wa amani.
Wahenga walisema asiyekubali kushindwa si msindani. CCM wakubali kuwa wameshindwa na kwa sababu hiyo watumie busara kukubali kuachia umeya ili wajipange kwa ajili ya mwaka 2020. Alimradi sote tunaijenga Tanzania, tunawaasa CCM wawaachie wapinzani umeya huu maana wapigakura ndiyo walioamua iwe hivyo.