tulia acksonSiku kama ya jana, Novemba 23, miaka 39 iliyopita katika Kijiji cha Bulyaga, Kata ya Tukuyu, wilayani Rungwe mkoani Mbeya kwenye familia ya Akson Mwansasu, alizaliwa binti kitinda mimba.

Ilikuwa ni kiu ya mama ambaye licha ya kuwa na watoto wengine 10, alitaka kutulia kwa kupata mtoto wa kike na ndipo alipozaliwa binti huyo katika uzazi wa 11 na kupewa jina la Tulia.

Mama akatulia baada ya Mungu kumtuliza kwa binti Tulia ambaye pia alitulia tangu alipoanza kuisaka elimu na kuonesha mwanamke anaweza, akianza safari yake katika Shule ya Msingi Mabonde, Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya.

Matoke0 ya darasani yalifanya Wizara ya Elimu impangie kuendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Loleza iliyoko jijini Mbeya, barabara ya kwenda Mtaa wa Ghana alikohitimu kidato cha nne.

Akapasua tena na kujiunga na Shule ya Wasichana ya Zanaki ambako alimalizia masomo yake ya kidato cha sita mwaka 1997. Kwa hiyo, utaona kwamba elimu yake ya sekondari alisoma katika shule za Serikali za wasichana na kufanya vema.

Mwaka 1998 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitivo cha sheria na kufanikiwa kuhitimu chuoni hapo. Alitunukiwa shahada ya sheria mwaka 2001.

Mwaka huohuo wa 2001, Chuo hicho Kikuu cha Dar es Salaam kilimtaka kubaki chuoni hapo kwa ajili ya kufundisha sheria, hivyo alifundisha huku akiendelea kusaka shahada ya uzamili.

Akiwa bado anafundisha chuoni hapo, mwaka 2003 alimaliza masomo kabla ya kufanya mtihani wa uwakili wa kujitegemea mwaka 2004. Mwaka 2005 alijiunga na Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini kufanya shahada ya uzamivu na kufanikiwa baada ya miaka miwili. Tulia alitulia na kwa sasa ni dakta wa sheria.

Mwaka 2008 alikwenda chuo cha Max Planck Institute for International and Social Law cha  Munich, nchini Ujerumani alikokuwa akifanya ‘post doctoral research’.

Mwaka 2009 alirudi nchini katika ajira yake ya awali ya ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na aliteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria, nafasi ambayo alikuwa nayo mpaka mwaka 2014.

Akiwa Makamu Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria alifanikiwa kushika nafasi hiyo kwa vipindi viwili tofauti, hii yote ni kutokana na taratibu zake kuwa ni mkataba wa miaka mitatu ingawa unaweza kuteuliwa tena baada ya kumalizika kwa mkataba wa awali.

Kutoka wajumbe wa elimu ya juu, Dk. Tulia alikuwa miongoni mwa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne katika Bunge la Katiba lililofanyika kwa awamu mbili.

Awamu ya kwanza lilifanyika kuanzia Februari 18, 2014 hadi Aprili 25, 2014. Kwa siku 21 za kwanza alikuwa miongoni mwa wajumbe waliotunga kanuni za Bunge hilo lililoongozwa na Mwenyekiti Samwel Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan.

Utungaji wa kanuni hizo ulikuwa ni wa ‘vuta nikuvute’ hasa kwa wanasheria waliokuwa wakioneshana umahiri wa kuchambua sheria mbalimbali hadi kufikia kupata kanuni ambazo upinzani hawakuzifurahia sana ingawa mambo yalisonga.

Mwaka huohuo wa 2014 aliteuliwa na Chuo Kikuu cha Bayreuth cha nchini Ujerumani ili kufanya utafiti kuhusu hifadhi za jamii, utafiti uliojulikana kama Awarded the Alexander Von Humboldt Research Fellowship.

Alipaswa kufanya utafiti huu kwa kipindi cha miaka mitatu tu, ambapo alianza Machi mwaka huu na kuwapo nchini Ujerumani hadi Agosti aliporudi kwa ajili ya likizo fupi.

Hata hivyo, utafiti huo aliufanya kwa kipindi cha miezi sita tu, kwani akiwa katika mapumziko, ndipo alipoteuliwa tena na Kikwete kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Septemba 9, mwaka huu.

Amekuwa naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miezi miwili tu kutokana na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, kutengua uteuzi huo na kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, akiwa ni mbunge wa kwanza kati ya nafasi 10 za wabunge aliopewa Rais kwa mujibu wa sheria.

Kati ya kazi nzito alizofanya akiwa Mwanasheria Mkuu ni kuongoza jopo la mawakili wa Serikali katika kesi maarufu kwa jina la mita 200, kwani kulitokea mvutano baina ya vyama vya upinzani na Serikali katika kutafsiri sheria ya umbali wa wananchi kukaa mara baada ya kupiga kura.

Mahakama Kuu ilitafsiri sheria hiyo kwa kuagiza wapigakura kukaa mbali kwa zaidi ya mita hizo baada ya kuridhishwa na hoja za upande wa Serikali ambako Dk. Tulia alikuwa kinara kwa kutaka korti iamue hivyo.

Alhamisi Novemba 19, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipiga kura ya kumchagua Tulia kuwa Naibu Spika wa Bunge hilo. Uchaguzi huo ulifanyika mapema asubuhi ndani ya Ukumbi wa Bunge. Katika uchaguzi huo, Dk. Tulia (CCM) alipata kura 250 kati ya 351 za wabunge wote, huku mpinzani wake, Magdalena Sakaya (CUF) akipata kura 101.

Sasa amekuwa mbunge pia tena Naibu Spika, vipi kuhusu utafiti wake huko Ujerumani? Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii yaliyofanyika mara baada ya kushinda, Dk. Tulia anasema: “Nimesitisha.”

Akizungumzia kuhusiana na kusitisha utafiti wake aliokuwa ameuanza nchini Ujerumani, anaeleza kuwa kwa sasa anatafakari njia mbadala ya kumuwezesha kuendelea na utafiti huo bila kuathiri majukumu yake aliyonayo kwa sasa.

“Najaribu kuendelea na kuwasiliana na Bayreuth Unirvesity kuona jinsi ya kumaliza utafiti huo, hata kama ni kwa vipindi tofauti tofauti badala ya muda wote kuwa nje ya nchi kwa ajili hiyo,” anasema.

Wakati Dk. Tulia akisema hayo, hafichi hisia zake kuhusu shukrani zake kwa Rais Dk. Magufuli kwa kumuona anafaa kuwa mbunge, hivyo kumteua katika nafasi hiyo kubwa iliyozaa kubwa zaidi ya unaibu spika.

“Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli ameonesha imani kwangu, nami sitamwangusha. Pia nawashukuru wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunipigia kura na kunipitisha kuwa Naibu Spika,” anasema Dk. Tulia.

“Nilikubali uteuzi na hasa kuwa mbunge kwa sababu siku zote nimekuwa nikipenda kufanya kazi za kijaamii, lakini pia nimekuwa na lengo la kuwa profesa hivyo nahitaji kutimiza hilo,” anasema.

Dk. Tulia anasema anatarajia kuliona Bunge la 11 kuwa na changamoto nyingi kuliko mabunge mengine yaliyotangulia kwa kuwa wabunge wengi ni vijana tofauti na hapo awali.

“Watanzania wana matarajio makubwa sana na Bunge hili, wanatarajia kuweza kuwabadilishia maisha, hivyo mimi binafsi natarajia kuwa Bunge litakalokuwa na miswada mingi kutokana na mabadiliko,” anasema.

Anaamini kuwa hoja za wabunge zitaongezeka kutokana na mambo yanayowakabili wapiga kura na Taifa kwa ujumla, huku wakitaka kutolewa ufumbuzi wa kudumu na Serikali.

Kwake anasema kwamba amejipanga kukabiliana vurugu za aina yoyote kwa kufuata kanuni na taratibu na miongozo ya kibunge, “lakini ikumbukwe kuwa sababu za fujo au vurugu zipo nyingi ikiwamo hulka ya mtu binafsi.”

Anaongeza: “Lakini zipo hoja za msingi ambazo zinaweza kufafanuliwa na kusaidia kuongeza uelewa unaoweza kuepusha vurugu au kutoelewana.

“Katika Bunge la 10 mambo mengi yametokea, na tayari yameweza kufuatiliwa kwa karibu huku mengine yakitafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuchukua hatua stahiki. Sitaraji kuliona Bunge hili likishindwa kufanya kazi kwa ushirikiano na maelewano.

“Kama Naibu Spika, nitafanya kazi kwa ukaribu na Spika, tutasimamia sheria na kanuni za Bunge na kufuatilia hoja zote zitakazoibuliwa na wabunge maana kazi ya Bunge ni kusimamia Serikali.

“Binafsi sitapuuza jambo lolote ikiwa ni pamoja na kusimamia hoja zote za wabunge na kuzifanyia kazi. Mimi ni mwanasheria siyo mwanasiasa, hivyo nitafanya kazi zangu kutokana na kanuni na sheria za Bunge na si vinginevyo. Ila naahidi kuwa nitafanya kazi kwa unyenyekevu mkubwa,” anasema.

Dk. Tulia ambaye ameolewa na James Andilile na wamebahatika kupata mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minne, anasema siri ya mafanikio hayo kuwa “ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

“Ni Mungu yeye amepanga niwe hivi nilivyo, nifike hapa nilipofika maana yeye ndiye anayejua na anayepanga maisha yetu. Naamini lengo lake kwangu linatimia atakavyo yeye. Pia juhudi binafsi ni muhimu ili kufikia malengo husika.

“Kila mwanadamu anapaswa kufanya bidii na kutokata tamaa, mimi kwetu ni mtoto wa 11 kati ya watoto 11 wa Akson Mwansasu. Sikujisikia mnyonge kwa sababu ya mwanamke au mtoto wa mwisho.”