Mkurugenzi Mkuu wa CZ Information & Media Consultant LTD, Cyprian Majura Nyamagambile amsemema kwamba anatarajia kumfikisha mahakamani Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kufuatia kauli zake za uongo alizozitoa na kuchafua taswira ya Tanzania.
Cyprian ameyasema hayo leo Januari 15 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba, yeye na wanasheria watamfungulia mashtaka mbunge huyo.
Amesema kuwa, wamefikia uamuzi huo kutokana na maneno aliyoyatoa Lissu kabla ya kwenda nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu, kwamba Tanzania kwa sasa sio mahali salama pa kuishi na eneo hatarishi kwa maisha ya binadamu.
“Tundu Lissu aliutangazia Umma na dunia nzima kwamba Tanzania sasa si salama tena, nchi hii watu wanakufa hovyo hovyo kitu ambacho si cha kweli anapotosha. Tanzania ni salama watu wanaabudu vizuri, wanajieleza vizuri ndiyo maana mimi nipo hapa najieleza kama kusingekuwa na uhuru wa kujieleza mimi nisingekuwa hapa.”
Cyprian amesema wanampeleka mahakamani kwa sababu ameidhalilisha nchi kitaifa na kimataifa wanampa siku mbili tu atoe ushahidi wake na uthibitisho kwamba Tanzania siyo salama.
“Tunampa siku mbili atoe uthibitisho wa kauli zake vinginevyo tutampeleka mahakamani, na japokuwa tutampeleka katika mahakama za ndani, nakala yake itapelekwa The Hague Uholanzi kwenye Mahakama ya Kimataifa,” amesema Cyprian Musiba.