HAYA HAPA MATOKEO KIDATO CHA NNE 2024 GUSA CHINI

https://matokeo.necta.go.tz/results/2024/csee/CSEE2024/CSEE2024.ht

Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya watahiniwa 557,796 ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwezi Novemba mwaka 2024, ambapo wasichana ni 296,051 na wavulana ni 261,745.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dkt Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa wa shule 477,262 kati ya 516,695 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 92.37 wamefaulu kwa kupata madaraja I, II, III na IV, ukilinganisha na mwaka 2023 ambapo watahiniwa waliofaulu walikuwa 471,427 sawa na asilimia 89.36, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.01.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea ufaulu wao pia umepanda kwa asilimia 10.07, ambapo kwa mwaka 2024 waliofaulu ni 15,703 sawa na asilimia 62.51, tofauti na mwaka 2023 ambapo waliofaulu walikuwa 13,396 sawa na asilimia 52.44.

Baraza la mitihani limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 459 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo, ambapo watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha kanuni za mtihani.

Aidha limefuta matokeo yote ya watahiniwa 67 waliobainika kufanya udanganyifu na watahiniwa 05 walioandika lugha ya matusi katika skripiti zao katika mtihani wa kidato cha nne.

Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30 (2) (b) cha kanuni za mitihani mwaka 2016.

Katika hatua nyingine baraza limefungia kituo cha P6384 BSL Open School kilichopo mkoani Shinyanga kuwa kituo cha mitihani ya taifa kutokana na kuratibu mipango ya udanganyifu.