Kuna mashabiki wa Yanga wanaamini Kisinda akiondolewa kikosini ghafla tu watapata bonge la winga linaloishi vichwani mwao. Mpira una njia zake, wanapaswa kumuheshimu Kisinda na makocha wanaompa nafasi ili aweze kuendana na mfumo wa timu.
Wanayanga wanapaswa kufanya tathmini ya mechi toka mechi moja kwenda mechi nyingine ili kuepuka kukariri kwamba uchezaji wa Kisinda upo vile vile toka mechi ya kwanza mpaka leo.
Makocha hawaangalii kwa jicho la kishabiki bali wanaangalia uwezo wa asili wa mchezaji kisha wanaanza kumjenga katika yale wanayoyataka wao kwenye mfumo wa timu ndio maana utaona mchezaji hachezi wanavyotaka mashabiki lakini kocha anaendelea kumpa nafasi.
Kuna wakati Yanga waliwahi kutamani Farid Musa atemwe lakini baada ya muda wakampigia makofi Nabi kwa kuboresha kiwango cha Farid ambaye kwa sasa kocha Nabi anamtumia mpaka kwenye nafasi ya beki wa kushoto.
Makocha wanaangalia uwezo asilia wa mchezaji kisha wanaangalia uwezo wa mchezaji kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi na ukiona mchezaji anaendelea kupewa nafasi basi huyo anayafanyia kazi maelekezo ya kocha.
Mashabiki wanahitaji kujikumbusha kuhusu Jesus Moloko wakati anatua Yanga na alivyo sasa. Uongozi pia huwa unaangalia mchezaji ambaye anadhibitika ambaye akikaa sawa timu inaweza kumtegemea. Sio kila mchezaji mzuri anadhibitika.
Tuisila akikaa sawa ataisaidia timu kwa sababu akitolewa uwanjani hatalumbana na kocha, hautamsikia Tuisila ana utovu wa nidhamu wa aina yeyote. Wanayanga wanapaswa kuwaheshimu viongozi wao wanaokaa na hao wachezaji na kujua tabia zao.
Tuisila Kisinda mpaka sasa yupo kwenye njia sahihi na anafanya vizuri sana na timu. Saizi anakaa na mpira, analifuata boksi sio kibendera tena, na inapobidi anatoa pasi na sio kukimbia tu na mpira bila kuangalia mazingira. Kisinda mwenye ubora anakuja upesi.
Kitu muhimu watu wa mpira wanatakiwa kujua ni gharama kubwa kumpata winga mwingine na kumjenga mpaka kufikia uwezo wanoutarajia mashabiki wengi Lakini kwa Kisinda bado hatua chache sana ashangiliwe uwanja mzima.