Makala iliyopita nilijadili namna uvivu, udokozi, na udhuru vinavyotukwamisha Watanzania wengi.

Nikasema hizo ni miongoni mwa sababu chache, kati ya nyingi zinazowafanya baadhi ya waajiri nchini mwetu waamue kuajiri wageni bila kujali maumivu ya kiwango cha mishahara na malipo mengine wanayotumia kwa wageni hao.

Nimepata simu nyingi na ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wasomaji wengi. Wengi waliniunga mkono, na wachache walitofautiana nami. Hilo la kutofautiana ni jema.

Msomaji mmoja amesema haya: “Nimekusoma vizuri sana kwenye Jamhuri leo (Machi 8). Mchana huu nilienda sehemu kupata chakula, wahudumu walikuwapo wamekaa, lakini iliwachukua dakika 10 kuja kutusikiliza. Uliyoyaandika ni kweli tupu. Hongera kwa kuliona hilo. Huo ndio ukweli mchungu.”

Mwingine akaandika hivi: “Kakangu, umesahau lingine…kum-supervise Mtanzania bora kusukuma majabali mlimani. Mfanyakazi Mtanzania anataka afanye anavyotaka.”

Kuna msomaji alikuwa na haya: “Mkuu miaka7 nimefanya kazi na Wachina as a marketing officer, mshahara wangu haukuzidi laki 7, meneja wangu Mchina alikuwa analipwa dola 2,500; ana certificate ya social science kazi zote nilikuwa nafanya mimi, napingana na dhana yako kuhusu Watanzania.

Kwa dhana hizo ambazo mmewajengea Watanzania ndio mna wa in-courage wawekezaji feki kutunyonya, hebu mpe Mtanzania package nzuri toka siku ya kwanza uone. Nilikuwa nawaamini lakini kwa makala yako hii sikuamini tena. Hukufanya research ya kutosha.”

Kama nilivyoasema, hii ni sehemu ndogo, kati ya simu na ujumbe mfupi wa maandishi nilivyopokea kutoka kwa wasomaji wetu wengi sana. Awali ya yote niwashukuru mno Watanzania kwa kuendelea kutuunga mkono JAMHURI. Pale inapotokea mitazamo yetu ikatofautiana, tujue tofauti hizo ni njema. Katika somo la fizikia kunafundishwa “msuguano”. Bila msuguano, hakuna mwendo! Ili chombo cha usafiri, au chombo kingine kiweze kutoka sehemu moja hadi nyingine, msuguano ni muhimu. Lakini tofauti na misuguano ya ugomvi, misuguano ya kimaendeleo ni kama ile ya matairi ya magari. Kama ni mbele-yote yaende. Kama ni nyuma-yote yaende nyuma. Ikitokea haya yanataka kwenda mbele, mengine yanataka kurudi nyuma, hapo hakuna mwendo! Tusiwe kama matairi yanayokinzana. Tutofautiane mitazamo kwa nia njema ya kwenda bega kwa bega mbele.

Bado naamini katika maneno ya Baba wa Taifa ya kwamba: “Kosa moja kubwa sana ambalo linatokana na unafsi ni kutaja makosa ambayo sisi wenyewe hatunayo, na kuficha makosa ambayo sisi wenyewe tunayo. Hii ni kosa lile lile linalotufanya tulaumu tusiowapenda, na kutolaumu tunaowapenda, bila kujali ukweli. Nimetaja makosa haya ili yatusaidie, siyo katika kuwahukumu wenzetu tu ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe, ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi.”

Watanzania walio wengi tumekuwa watu wa kupenda kulaumu tu, na si kutafuta chanzo au sababu za mkwamo wetu. Haishangazi kuona hadi leo bado tupo tunaowashutumu wakoloni kwa kutukwamisha kimaendeleo! Lakini tumekuwa wavivu kujiuliza sababu zinazotufanya tuwe wachovu kimaendeleo, ilhali waliokuwa wachovu wenzetu wa miaka hiyo, leo wako mbali mno. Juzi, tulipokea ugeni wa Rais kutoka Vietnam. Sina sababu ya kueleza hapa, lakini kwa anayetaka kujua nani katuroga Watanzania, anaweza kupitia historia ya kimaendeleo ya Vietnam; akaongeza na ya mataifa mengine ya Korea Kusini, Indonesia, Malaysia na kadhalika. Hapo atajua hawa wenzetu walikuwa wapi, wako wapi na wanakwenda wapi. Kisha ajiulize sisi tuna dira au mwelekeo upi. Tofauti ya hao na sisi ni kuwa wao tangu mapema walijua wanakokwenda kwa hiyo hawajapotea! Kwa kawaida usipojua unakoenda, huwezi kupotea! Watanzania wengi hatujui hii safari yetu tunataka hitimisho lake liwe wapi, kwa hiyo tunapuyanga tu. Hatujui tuendako kwa hiyo hatuoni kama tumepotea!

Kwenye kupuyanga huku, ndimo tunamoshuhudia viji-sababu vingi vinavyotumiwa kuhalalisha uvivu, wizi, udokozi, na udumavu wa kimaendeleo. Ndiyo maana utawasikia wengine wakisema Rais Magufuli apunguze kasi! Watanzania huwezi kujua wanahitaji jua au mvua! Kwao kila jambo halifai. Tuwe na rais mtembezi kama aliyepita, kosa. Tumempata rais aliyeamua kuketi nyumbani ashughulikie kero za wananchi, nongwa!

Maudhui yangu bado ni yale yale, ya kwamba endapo Watanzania hatutabadilika na kuweza kwenda na kasi ya mabadiliko ya kimaendeleo ya dunia ya leo, kamwe malalamiko yetu hayatakoma.

Msomaji mmoja amejaribu kuonesha ni kwa namna gani alifika hotelini, lakini akaketi kwa dakika 10 bila kuhudumiwa! Hili kwa Tanzania hii si jambo la ajabu hata kidogo! Kwa wanahabari, wanasema hiyo si habari. Habari ni pale Mtanzania anapochangamka kumpokea mgeni na kumhudumia kwa kasi na kwa viwango.

Msomaji anayesema kwamba ana elimu kubwa, lakini analipwa kidogo kuliko Mchina mwenye elimu ndogo, lazima ajiulize maswali kadhaa ili apate jawabu.

Miongoni mwa matatizo makubwa kabisa miongoni mwetu, ni kuendekeza malalamiko kana kwamba kulalama pekee ndiyo suluhu ya matatizo yetu. Tunakosea.

Mwalimu Nyerere, katika kijitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962, anasema haya:

“Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo.

“Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu.

“Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, na kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo.

“Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalamu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n. k.-lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchaguzi wa kweli, siyo sababu ya uvivu wa kutumia akili!

“Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si ya dawa hata kidogo. Nikienda kwa mganga anitibu maradhi yangu, namtazamia kuwa kazi yake ya kwanza ni kujua hasa, siyo kwa kubahatisha, naumwa nini; kazi yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu; kazi yake ya tatu ni kujua dawa ya ugonjwa wangu. Daktari asipojua ugonjwa wangu na sababu zake hawezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona, atakuwa kaniponya kwa bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo hawezi kumponya mgonjwa, na ni daktari wa hatari sana.”

Maneno haya ya Mwalimu yanatuasa tutumie akili kutatua matatizo yetu badala ya kulaumu tu au kumsukumia Mungu kila tunapokwama. Ajira zinapochukuliwa na wageni, hatuna budi kujiuliza ni kwanini zinachukuliwa na tufanye nini ili zisichukuliwe.

Katika ulimwengu wa leo ambako ubepari umetamalaki, hakuna mwajiri anayeweza kumvumilia mtumishi mwizi, mdokozi, mvivu, asiyekoma kuwa na udhuru, anayelalama tu, au asiye mbunifu. Wenye viwanda, mashamba au kampuni za uzalishaji wanachoangalia ni faida na uendelevu wa shughuli zao. Hawako tayari kuajiri watu wezi au wavivu kwa sababu tu ni Watanzania wenzao! Hakuna kitu cha aina hiyo.

Uvivu wa kutumia akili unaweza kutufanya tuwachukie wageni ilhali sisi wenyewe ndiyo chanzo cha yote haya. Kuna wakati fulani Watanzania wenzetu waliibuka na kujaribu kuonesha namna Watanzania na wasio Watanzania- wenye rangi nyeupe- wanavyolihujumu Taifa. Mimi sikuona sababu ya kuwaandama ndugu zetu hao kwa sababu kwenye orodha ya viongozi wa Serikali yetu kwa wakati huo, na hata sasa sioni mwenye ngozi nyeupe wa kusema yupo pale TIC, Hazina, Wizara ya Madini, au kwingineko, anayewapendelea ‘weupe’ wenzake!

Tubadilike. Tuache udokozi. Tuache wizi. Tuache kutumia vibaya muda wetu wa kazi. Tujitume, tuwe na nidhamu kwenye kazi na tuache kulalama tu kana kwamba yupo wa kutuondolea adha zinazotukabili.

Tufike mahali kila Mtanzania ajione ana wajibu halali na fursa ya kutumika yeye kama chachu katika maendeleo yake binafsi, ya jamii yake, na Taifa kwa jumla.

Sasa wengi wetu tunatega masikio kusikia nani kateuliwa kuwa nani katika Serikali hii kana kwamba wateuliwa hao ndiyo wenye mwarobaini wa kumaliza matatizo yetu. Bila kubadili tabia katika utendaji kazi wetu, hata waletwe mawaziri na wakuu wa mikoa malaika, bado Tanzania itabaki ile ile. Tupambane kubadili mfumo wa uongozi unaowafanya viongozi wawe wasindikizaji tu badala ya chachu na dira ya maendeleo.

Ndiyo maana tunasema mapambano haya ya kuwa na Tanzania mpya yanayoongozwa na Rais John Magufuli, yatafanikiwa tu endapo kila mmoja wetu na kwa nafasi yake atatekeleza wajibu wake. Bado nasisitiza kuwa kwa mwenendo wa sasa, bila kubadilika, ajira zitaendelea kushikwa na wageni. Dawa pekee ya kukomesha hilo ni kwa sisi Watanzania kubadilika. Tuache kulalama.