Anzia wengine wanapoishia

Mwisho unaweza kuwa mwanzo wa kitu kipya. “Kila mwanzo mpya unatoka kwenye mwisho wa mwanzo mwingine,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki, Seneca. 

Mababu zetu na nyanya zetu walitunza hadithi na methali kwenye vichwa vyao, sisi tumeanzia walipoishia, tunatunza kwenye vitabu, mitandaoni na vichwani pia.

Michael Jackson alikutana na watoto wa mitaani wakicheza dansi inayojulikana kama ‘backslide’, yaani dansi ya kucheza kwa kurudi nyuma. Aliomba kufundishwa aina hiyo ya dansi. Baadaye aliipa jina ‘The Moonwalk’ – mwendo wa mwezi. Aliipeleka dansi hiyo jukwaani ikatoka kama kitu kipya. Alianzia watoto wa mitaani walipoishia.

Baadhi ya Wayahudi wamekuwa na utamaduni wa kuacha sehemu ndogo katika nyumba bila ya kuimalizia. Jambo hili linaonyesha maisha ya mtu hapa dunia ni shughuli ambayo ina kipengele ambacho hakikumalizika au hakikukamilika. Ni fahari kubwa kukamilisha kile ambacho binadamu mwenzetu amekiacha bila kukikamilisha. Anzia mwingine alipoishia. Mtazamo tuupatao kutoka kaulimbiu ya Gazeti la JAMHURI, ‘Tunaanzia Wengine Wanapoishia.’ Uvuke mipaka ya tasnia ya uandishi wa habari. Mtazamo huu unaweza kuingia katika familia, ofisini, kiwandani, kwenye kampuni na kwenye taasisi mbalimbali.

Kama baba yako alikuwa fundi seremala na aliishia kuranda ubao kwa kutumia randa ya mbao, anzia hapo tumia mashini za umeme. Kama mzazi wako alikuwa na dawa ya kienyeji ya kushusha sukari inayopanda kuzidi kawaida, ipeleke Taasisi ya Taifa ya Utafiti inayoitwa NIMR ifanyiwe kazi. Anzia mzazi wako alipoishia. Kama wazazi wako walitumia jembe la mkono kulima, anzia walipoishia, tumia trekta.

Charles Babbage anasemwa kuwa ni Baba wa Kompyuta. Ni Mwingereza, mwanamahesabu, injinia na mwanafalsafa. Aligundua injini ya uchambuzi mwaka 1837. Injini hii ilikuwa na kitengo cha kujumlisha, udhibiti wa mtiririko msingi na kumbukumbu iliyounganishwa. 

Steve Paul Jobs alileta mapinduzi ya kompyuta ndogo pamoja na uhuishaji wa picha na muziki katika kompyuta. Alianzia wengine kama Charles Babbage walipoishia. Suala ni kuanza wengine wanapoishia. “Si lazima uwe mkubwa ili kuanza, lakini lazima uanze ili kuwa mkubwa,” alisema Joe Sabah.

James Finley (1756-1828) anajulikana kama mjenzi, msanii, mchoraji wa daraja angiko. Ingawa hakuna daraja lake angiko ambalo limedumu hata leo, Thomas Telford alianzia alipoishia James Finley. Daraja kubwa angiko lilijengwa na Thomas Telford na kukamilika mwaka 1826 huko Wales.

Daraja la Kigamboni ni la aina yake kwa uzuri Afrika Mashariki lenye urefu wa meta 680. Ni daraja angiko refu Afrika Mashariki. James Finley angekuwa anafufuka angeshangaa uzuri wa daraja na maendeleo makubwa katika wazo alilokuwa nalo la daraja angiko. Anzia wengine wanapoishia.

Tukitupia jicho maisha ya kijijini, watoto hawana budi kuanzia wazazi walipoishia. Rafiki yangu Patrick Mwai wa Kenya akiwa mdogo alimsaidia baba yake ambaye alikuwa fundi seremala. Baadaye Patrick Mwai alikwenda chuo cha ufundi na kujifunza useremala. Leo hii ana kiwanda kikubwa sana kinachoajili watu wengi cha kutengeneza vifaa vya mbao vya kubebea maua. Kiwanda kinachotumia umeme. Alianzia baba yake alipoishia.

Kama mzazi wako ameishia kwenye kioski, anzia alipoishia uwe na duka. Kama mzazi wako ameishia kuwa na gazeti, anzisha jarida na kiwanda cha kuchapisha vitabu. Kama mzazi wako amekuwa akilima kahawa kwenye shamba dogo, anzia hapo kuwa na mashamba makubwa ya kahawa. Kwa maneno mafupi na matamu, anzia pale wengine wanapoishia.