Bajeti inakusaidia usijiibie

“Ukinunua usilolihitaji, unajiibia,” ni methali ya Sweden. Bajeti inakusaidia kuandika mahitaji ya kweli chini baada ya tafakuri ya kina. Ukinunua kitu kwa vile jirani yako amekinunua unajiibia. Ukinunua kitu ili kumwonyesha mwenzi aliyekuacha kuwa maisha yamekunyokea na si kwa vile unakihitaji, unajiibia. 

Usipojilipa, unajiibia. Mtu anaweza kuwa na biashara kubwa, akawalipa wafanyakazi wake wakaweza kuwa na siku ya kutoka kwenda kuogelea na kujiburudisha kidogo lakini yeye kamwe hana muda na namna ya kujilipa. Ukinunua vitu kwa vile pesa ipo mfukoni unajiibia. 

Bajeti ina sura nyingi. Kadiri ya Dave Ramsey: “Bajeti ni kuiambia pesa yako mahali pa kwenda badala ya kushangaa imekwenda wapi.” Bajeti ni kidhibiti cha matumizi ya ovyoovyo. Kuwa na bajeti ni hatua ya kutafsiri mpango katika matendo. Bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi.

Kuwa na bajeti ni hatua ya kutafsiri ahadi katika matendo. Ni ramani inayochukuliwa katika safari ya kiuchumi. Hakuna jambo baya kama kusafiri bila kujua kikomo cha safari au namna ya kufika mwisho wa safari, yaani bila kuwa na ramani. Ikumbukwe mwisho wa mwezi baadhi ya watu huishiwa pesa. Mwezi Januari huwa ni mwezi mbaya. Kuna sababu ya kuwa na bajeti na kuiheshimu. Kauli ya Biblia ya “Toa hesabu ya mapato na matumizi.” (Luka 16: 2) ni msingi wa kidini wa bajeti na mipango.

Kwanza, bajeti inakupa picha ya pesa unayoingiza kwa upande wa mapato. Hivyo kama unaingiza kidogo unaweza kupanga namna ya kuongeza kipato: kuongeza vyanzo vya mapato, kutafuta kazi nzuri zaidi, kuongeza ujuzi ili kuongeza kipato au kuanzisha biashara ndogo na kubwa.

Pili, bajeti inakushtua kama alama nyekundu imeanza kujitokeza katika mapato na matumizi yako. Inakufanya ukae mkao wa kujiandaa kwa lolote lile. Kutumia ni haraka, kupata ni polepole (Methali ya Urusi).

Tatu, bajeti inakupa picha ya matumizi yako, hivyo kukusaidia kujua wapi pa kubana na wapi pa kupanua wigo wa matumizi, ikiwa matumizi hayo ni mkakati wa kuongeza mapato. Bajeti inakufungua macho kujua pesa yako inakwenda wapi.

Nne, bajeti inakusaidia usiingie shamba la madeni bila kujua. Na kama umeingia tayari bajeti inakusaidia kuwa na mpango wa kutoka. “Tatizo la deni  kwenye kitovu chake ni tatizo la bajeti.”

Tano, kuwa na bajeti kunakuwezesha kuidhibiti pesa badala ya pesa kukudhibiti. Unakuwa na udhibiti wa asilimia 100 ya pesa yako. “Afadhali kulala kitandani bila kula chakula cha usiku kuliko kuamkia kwenye madeni.”

Sita, bajeti inakusaidia kuwa na vipaumbele vya malengo.

Saba, bajeti inakusaidia kuwekeza.

Nane, bajeti inakusaidia kupanga namna ya kujilipa. Kuna baadhi ya watu wana biashara na kampuni kubwa lakini hawajilipi. Tisa, bajeti inakusaidia kuongelea pesa kwa urahisi na wanafamilia.

Kumi, bajeti inakusaidia “siku ya mvua” ambapo hainyeshi bali mbingu zinamwaga maji. “Siku ya mvua” ni siku ya mambo yanayotokea ghafla bila kupanga. “Siku ya mvua” inadokeza dharura. “Siku ya mvua” inadokeza yasiyotarajiwa.

Kumi na moja, bajeti inabainisha mambo unayoyathamini.  “Usiniambie unachokithamini, nionyeshe bajeti yako, nitakwambia unachokithamini,” alisema Joe Biden.

Kumi na mbili, bajeti inakusaidia kuhakikisha pesa yako inatosha. Bajeti si kwa ajili ya taasisi tu, bajeti si kwa ajili ya tajiri tu, bajeti ni kwa ajili ya mtu yeyote.