Kinachokosekana kwenye yai kitafute kwenye kuku. Panga kuwa na kuku. Hatupangi kushindwa, tunashindwa kupanga. Kinachokosekana kwenye mto kitafute kwenye ziwa. Ukitamani kwenda mbali liache yai, tafuta kuku. Wacha kitanda ili kutanda. (Methali ya Kiswahili). Kutanda ni kuenea au kutandaa.

Ukitamani kwenda mbali kiache kitanda. Kutafuta ni kuthubutu. Ili kupanga lazima ujue ulichonacho. Ulichonacho ni yai. Jogoo wanaowika yalikuwa mayai (methali ya Tanzania). Lakini huenda hujaridhika na yai.

“Kutoridhika ni hatua ya kwanza katika maendeleo ya mtu,” alisema Oscar Wilde. Usiridhike na hali uliyomo. Usiridhike na yai. Nuia kuwa na kuku. “Kutoridhika ni takwa la kujitegemea,” alisema Waldo Emerson. Unapotaka kupanga usiridhike na yai.

Kuna hadithi juu ya kifaranga cha mwewe. Kifaranga cha mwewe kilikaa na vifaranga vya kuku na kujifunza kuchakura kama vifaranga vya kuku. Kila mara kifaranga cha mwewe kilitamani kuruka na kupaa juu kama mwewe, lakini vifaranga vya kuku vilikizomea kifaranga cha mwewe na kukikatisha tamaa.

Siku moja kifaranga cha mwewe kilijaribu kupaa na kilifanikiwa kupaa. Watu wengi tunaishi kama vifaranga vya kuku, kumbe ni mwewe. Acha kitanda ili kutanda. Huenda wewe ni mwewe, kuwa na ndoto kubwa.

Ndoto yako ni ipi? Ndoto yako ni kuwa na kuku badala ya yai?  “Iandike ndoto ukaifanye iwe wazi sana katika vibao.” (Habakuki 2:2). Kwanza, ndoto yako iandike. Pili, ifanye iwe wazi. Dk. Myles Munroe alisema: “Andika chini mawazo yako, shauku na vipawa na uyasome kila siku jioni kwa wiki nzima. Kisha jiulize: “Je, mawazo haya yanashikilia ukweli? Je, ni kile ninachotaka kufanya?” Kama jibu ni ndiyo, yahifadhi mahala ambapo unaweza kuyarejea tena. Yafanyie kazi. Si kwa kusema: “Asali, asali,” utamu utaingia mdomoni.

Ili kuwa na kuku utahitaji kubadilika au kubadili mazingira. Kadiri ya John Maxwell katika kitabu chake ‘How Successful People Grow’ anasema hivi: “Badilika na mazingira yasibadilike – kukua ni polepole na kugumu. Badili mazingira na usibadilike – kukua ni polepole na ni kugumu kidogo. Badili mazingira na badilika – kukua ni kwa kasi na kuna mafanikio zaidi.”

Kuwa na yai kunaweza kumaanisha kuwa mtu wa wastani. “Kataa kuwa mtu wa wastani. Acha moyo wako upae kwa juu kadiri uwezavyo,” alisema Aiden Wilson Tozer. Ota ndoto kubwa na zifanyie kazi. Jenga ghorofa ya kufikirika angani, lakini iwekee msingi ardhini.

“Lisha akili yako na mawazo makubwa, huwezi kwenda juu zaidi ya unavyofikiri,” alisema mwanasiasa wa Uingereza, Benjamin Disraeli. Usijiwekee mipaka ya kufikiria makubwa.

Unakosa nini? Ni mambo gani unayoyakosa mahali ulipo katika shughuli zako, katika familia yako? Kama unakosa wateja katika biashara yako, huenda mahali ulipo ni kama upande wa mlima usiopata mvua. Hapo kuna kitu unakikosa kwenye yai.

Ukihamia mahali pengine unapata kuku. Lakini hata saa ya kufungua biashara na kufunga zinasema kitu. Ukichelewa kufungua biashara yako asubuhi na kufunga mapema jioni, unaambulia yai. Huenda wafanyakazi wako hawamjali mteja, unaambulia yai.

Unataka nini? Kuna mambo unayoyataka na mambo unayohitaji. Kuhusu mahitaji, kuna mahitaji ya kimwili na mahitaji ya kisaikolojia. Wanasaikolojia wanasema watu wana mahitaji saba ya kisaikolojia: kuwa mtu muhimu, usalama, kukubalika, kupendwa, sifa, nidhamu na Mungu. “Kila kitu Mungu anachokutumia kinahitajika. Asichokupa hakihitajiki kwako,” alisema John Newton.

Tafuta. “Hakuna kitu kitakujia kwa kukaa na kukisubiri,” alisema Zoe Kazan. Kutafuta kunahitaji kubanduka. Awashwaye ndiye ajikunaye. Aliyefikwa na shida ndiye anayejisaidia wala hawangojei wengine waje kumsaidia.

Thubutu. “Hatuthubutu kwa sababu mambo ni magumu; ni kwa sababu hatuthubutu mambo ni magumu,” alisema mwanafalsa wa Ugiriki.