Kama si sasa ni lini?
Kuna methali ya Kiyahudi isemayo: “Kama si sasa ni lini? Kama si sisi ni nani?” Katika makala hii tutazungumzia sehemu ya kwanza ya methali. Kama si sasa ni lini? Liwezekanalo sasa lisingoje saa ijayo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.
“Sasa ndio wakati wa neema.”(2 Wakorintho 6:2). Sasa ni baraka. Sasa ni neema. Sasa ni fanaka. Sasa ni bahati. Sasa ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Nafasi ya kujaribu tena inaitwa sasa. Sasa iwe ndefu au fupi, ni muda. Sasa ni fursa.
Ni kama fimbo, iwe ndefu au fupi ni fimbo. Mtu awe mrefu au mfupi, ni mtu. Sasa ni wakati uliopo, muda huu, kinyume cha baadaye. Sasa ni wakati wa kuanza uliloliamua kulifanya. Sasa ni wakati wa kuwa na nidhamu ya kumalizia ulilolianza. Unataka kuwa na elimu ya juu, kama si sasa ni lini? Unataka kufungua biashara, kama si sasa ni lini? Unataka kuvunja rekodi yako ya mwaka jana, kama si sasa ni lini?
Unataka kupima afya yako, kama si sasa ni lini? Unataka kuwa na vyanzo vingi vya pesa, kama si sasa ni lini? Unataka kuwa mcha Mungu, kama si sasa ni lini? Unataka kuwa na pasipoti, kama si sasa ni lini? Unataka kuweka akiba ya pesa kwa ajili ya kesho isiyojulikana, kama si sasa ni lini?
Methali ya China inatuasa: “Usiogope kutembea polepole, uogope kusimama tu.” Ni kama methali nyingine isemayo maji yanayotiririka hayachafuki. Maji yakituama kwenye dimbwi baadaye yananuka. Unapopiga hatua ni bora kuliko kuwa na kigugumizi cha uamuzi au maendeleo. Huwezi kununua inchi ya muda kwa inchi ya dhahabu. Muda ukipita, umepita. Kuwa na mti wa kijani moyoni labda ndege anayeimba atakuja. Kwa ufupi jiandae. “Fursa inapokuja, unakuwa umechelewa sana kujiandaa,” alisema John Wooden, mchezaji wa mpira wa kikapu. Jiandalie fursa kabla ya fursa kugonga hodi.
Fursa ipo mikononi mwako ichangamkie sasa. Sasa ni mwanzo. “Chochote unachokipenda kifanye sasa, muda hauko upande wako,” alisema Marty Rubin. Wakati wa kuamka kutoka usingizi wa nitafanya kesho ni sasa. Muda wa kutumia teknolojia ni sasa. Katika sasa kuna uwezekano usio na kikomo. Ukiishi katika sasa mambo mengine yatajipanga. Jana huwezi kuibadilisha, kesho bado ni ndoto.
Kuna hadithi juu ya mtu ambaye aliandika wosia kumrithisha shetani nyumba yake, shamba lake na kibanda chake. Hakimu alitoa hukumu hii: “Liache shamba liote magugu. Udongo umomonyoke. Acha nyumba iharibike na miti ya kibanda ioze.” Kutofanya lolote ni kumrithisha shetani. Fanya kitu sasa. Panga na tekeleza mpango. “Kupanga ni kuleta wakati ujao katika wakati uliopo ili kufanya kitu juu yake,” alisema Alan Lakein.
Kusitasita ni adui wa kufanya mambo sasa. Kuna methali ya Wahaya isemayo: “Wamekupa habari za msiba wakati wa kiangazi, umekwenda msibani wakati wa masika.” Wenye kusitasita hupigiwa methali hii. Jambo linalostahili kutendwa papo hapo lisipotendwa kwa wakati ufaao hutia hasara.
“Maadui wetu wa kweli wa maisha yetu ni ‘ingekuwa’ na ‘kama.’ Wanatuvuta nyuma kuingia wakati uliopita, usiobadilishwa na mbele, wakati ujao usiotabirika. Lakini maisha halisi yanachukua nafasi hapa na kwa sasa,” alisema Padri Henri Nouwen. Majuto ni mjukuu, mwishowe huja kinyume.
Kujipanga ni sasa. Ukarimu ni sasa. Kuwekeza ni sasa. Kujitathmini ni sasa. Kujiendeleza ni sasa. Kuwa mtu wa watu ni sasa. Kuwa na vipaumbele ni sasa. Kuacha jina zuri ni sasa. Ukianza jambo zuri usiliache bila kulikamilisha.