Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukichapisha habari zinazoruhusu Taifa letu. Hii ndiyo imekuwa kazi yetu kubwa kwa mwaka huu wa tano wa uhai wa Gazeti la JAMHURI.
Wasomaji wetu wanatambua namna tulivyoandika habari ‘nzito’, zikiwamo za wale ‘wasioandikika’ kuanzia kwenye biashara ya dawa za kulevya, ufisadi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), utapeli katika biashara ya madini, ufisadi katika Wizara ya Maliasili na Utalii na maeneo mengine mengi mno.
Tumeifanya kazi hiyo wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, na tumeendelea nayo wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Tofauti ya awamu hizi mbili ni moja; nayo ni kwamba Awamu ya Nne ilitia pamba masikioni, lakini Awamu ya Tano walau imeonyesha nia ya kweli ya kusoma, kufuatilia na kutoa majawabu kwa baadhi ya mambo.
Katika mpango huu mahsusi wa kuiunga mkono Serikali kwenye harakati zake za kurejesha maadili na uadilifu katika Taifa letu, isingewezekana kwa namna yoyote kuandika baadhi ya habari bila kuigusa Awamu ya Nne, na hasa kiongozi wake, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete.
Ni kwa sababu hiyo, kila tulipojaribu kuibua ufisadi au mambo yasiyofaa, tumejikuta jina la Kikwete likiwa mbele.
Kwa mfano, isingewezekana aslani, kuandika habari za wizi, ufisadi na uhujumu uchumi katika Bandari na TRA bila kumgusa Kikwete. Upo ushahidi wa kimaandishi na wa kimazingira kuwa kama si Kikwete aliyehusika moja kwa moja kwenye kashfa nyingi zinazomwandama, basi familia yake au kundi lililojipenyeza hata kuwa karibu naye, lilihusika.
Wizi na ufisadi katika TPA tumeuandika Kikwete akiwa madarakani. Ufisadi katika Wizara kama ya Maliasili na Mazingira tumeuandika sana, lakini kwa namna ambayo hadi leo si rahisi kuijua, kiongozi huyo alikaa kimya.
Tulishauri na kuhadharisha juu ya mambo mengi mno, lakini hatukusikilizwa. Leo Rais John Magufuli, anapoamua kuyashughulikia haya pamoja na wizi mkubwa ulivyofanywa na watawala waliopita, tunakuwa hatuna jingine, isipokuwa kumsaidia kuyajua mengi. Bado tuna kazi kubwa.
Wizi kama ule uliofanyika wakati wa Mkutano wa Smart Partnership, ulikuwa wa wazi kabisa. Tuliuandika, lakini Kikwete hakujisumbua kuwawajibisha wezi. Wizi wa mafuta, tumeuandika sana, lakini hakuna hatua.
Kwa ufupi ni kwamba hakuna linalofanywa sasa na Awamu ya Tano ambalo vyombo vya habari havikupata kuliandika au kulitangaza! Safari za nje za viongozi, matibabu nje ya nchi, rushwa na mambo mengine mengi yaliandikwa.
Hatuna ugomvi binafsi na Rais (mstaafu) Kikwete, lakini tutakuwa wanafiki kuamua kukaa kimya bila kuyataja mazuri na mabaya yake. Tunayaandika ili hawa walio madarakani sasa wajue wasipowajibika vilivyo kwa wananchi, nao watasemwa.
Alimradi tunayosema ni ya kweli na yasiyo na chembe ya husda, hatuoni sababu ya kusita kwa sababu ni haki ya Watanzania kujua nini kilichowakwaza na nani aliyebariki mkwazo huo.
Ili tuendelee tunapaswa kujua tulikotoka, tulipo na tuendako. Hicho ndicho tunachokifanya. Kizazi za cha sasa na kijacho kina haki ya kuyajua haya ambayo kundi fulani, kwa maslahi binafsi linajitahidi kuona hayasemwi wala kuandikwa.