Kutokana na uchumi wa viwanda unaoendelea kukua nchini, idadi ya wafanyabiashara wanaoagiza malighafi na mizigo kutoka nje kuja Tanzania inazidi kuongezeka.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeliona hili na inaendelea kuboresha huduma zake kuhakikisha wafanyabiashara wanaagiza malighafi na kuuza bidhaa wanazozalisha nje ya nchi bila bughudha.
Kuwarahisishia wateja wetu, TPA imeona ni vema iwajulishe tena wafanyabiashara wanaopitisha mizigo katika bandari za Tanzania utaratibu ulio bora wa kuagiza mzigo kutoka nje ya nchi. Hii inaondoa uwezekano wa mfanyabiashara kubabaishwa na ‘vishoka’, akazunguzwa na watu wasiofuata taratibu zilizowekwa na Bandari.
Tumeona ni vema tueleze njia ambazo mfanyabiashara anapaswa kuzifuata ili aweze kuagiza na kuupata mzigo wake kwa njia rahisi. Hatua hizo ni kuanzia kabla mzigo haujafika bandarini, kuwasili kwa mzigo mpaka kutoka kwa mzigo bandarini.
Wakala wa meli kutangaza kuhusu kuwasili kwa meli bandarini
Hatua ya kwanza inayofanyika katika mchakato wa usafirishaji wa mizigo majini ni Wakala wa Meli (Shipping Agent) kutangaza au kutoa taarifa katika mfumo wa bandari (Harbour View System) kuhusu matarajio ya kuwasili kwa meli bandarini.
Hatua hii ni muhimu kwani inaiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuanza kufanya mchakato wa kuipokea meli husika ili iweze kupata huduma zinazohitajika bandarini.
Taarifa za awali za kuwasili kwa meli bandarini ambazo hutolewa kupitia mfumo wa TPA hufuatiwa na vikao vya mipango vya wadau wa bandari ambavyo hufanyika kila siku mchana. Vikao hivyo hupanga jinsi ya kuzihudumia meli baada ya kuwasili bandarini.
Wakala wa meli anatakiwa saa 48 kabla meli haijawasili bandarini awasilishe taarifa za mzigo (cargo manifest) kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uitwao TANCIS. Taarifa hizo zikishapokelewa, TRA huzihakiki na kuzithibitisha juu ya usahihi wake.
Taarifa hizo za mzigo baada ya kuhakikiwa na kuthibitishwa katika mfumo wa TRA wa TANCIS ndipo TPA huzipakua (download) taarifa hizo ili kuziingiza katika mfumo wa bandari (cargo system) kwa ajili ya kuzichambua huku bandari ikisubiri kuwasili kwa meli kuleta mzigo husika bandarini.
Kuwasili kwa meli bandarini
Baada ya TPA kuziweka taarifa za mzigo kwenye mfumo wake wa kuhudumia mizigo na wakala wa meli kukamilisha malipo ya meli katika mamlaka husika zikiwemo TRA na TPA, kinachofuata ni kuwasili kwa meli bandarini.
Hatua inayofuata baada ya meli kuwasili bandarini ni TPA kushusha mzigo kutoka melini kulingana na taarifa za mzigo (cargo manifest) kama zilivyowasilishwa kutoka TRA kwa kupitia mfumo wa TANCIS na taarifa hizo kuchambuliwa na TPA kwa kutumia mfumo wa bandari (cargo system).
Bill of Lading
Ni vema ikafahamika kwa mwagizaji mzigo mtarajiwa na yule aliyeagiza mzigo tayari anasubiri kuutoa bandarini kwamba, kabla mzigo haujawasili mteja anatakiwa awe ameshaletewa nyaraka halisi (original bill of lading) kutoka kwa aliyeuza mzigo (shipper au consignor au exporter).
Bill of lading ni nyaraka muhimu sana ambayo inaonyesha anuani ya muuzaji mzigo, jina la nchi ulikonunuliwa mzigo, jina la meli, jina la mwenye mzigo na anuani yake, kama mzigo huo ni gari, nyaraka hiyo pamoja na taarifa hizo hapo juu ni lazima ionyeshe namba ya chassis ya gari, uzito wake, gari jipya au lililotumika na kama ni kontena nyaraka hizo zitaonyesha anuani ya mtumaji, jina la bandari kontena lilikopakiwa, jina la meli itakayochukua, aina ya mzigo, anwani ya mwenye kontena, namba za kontena na jina la bandari ambako kontena litateremshwa.
Mteja kutafuta Wakala wa Forodha
Mara tu mwagizaji anapopokea bill of lading ya mzigo wakeatatakiwa amtafute wakala wa forodha ampatie nyaraka hizo kwa lengo la kumsaidia mwagizaji kutoa mzigo bandarini. Wakala wa forodha kisheria ndiye aliyeidhinishwa na TRA kutoa mizigo ya wateja bandarini.
Wakala wa forodha baada ya kukabidhiwa nyaraka halisi ya mzigo wake, atatakiwa awasilishe nyaraka hizo kwa mamlaka husika kulingana na aina ya mzigo. Mamlaka husika itapokea nyaraka kwa ajili ya uhakiki na itachukua sampuli ya mzigo kwa ajili ya uhakiki. Mamlaka hizo ni kama vile Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Wizara ya Kilimo, Mkemia Mkuu wa Serikali, n.k.
Baada ya hatua ya uhakiki kukamilika, mamlaka husika itatoa cheti cha ubora na uhalali wa mzigo. Cheti hicho pamoja na nyaraka za mzigo husika zitatakiwa kuwasilishwa TRA kwa ajili ya mchakato wa kulipia ushuru. Kabla mchakato wa kulipa ushuru haujafanyika, TRA watafanya ukaguzi wa mzigo kwa macho au mubashara.
Release Order na Delivery Order
Taratibu za ukaguzi zikishakamilika wakala wa forodha atatakiwa kulipa ushuru wa mzigo wa mteja wake. Ushuru ukishalipwa, TRA watampatia wakala wa forodha nyaraka ya kutolea au kuondoshea mzigo bandarini (release order).
Aidha, wakala wa forodha atatakiwa kwenda kwa wakala wa meli (shipping agent) ambaye kampuni yake ya meli ndiyo iliyoleta mzigo bandarini kwa ajili ya kulipia nyaraka ya kupata mzigo (delivery order). Malipo hayo baada ya kukamilika wakala wa forodha atakabidhiwa nyaraka au kibali cha kupata mzigo wa mteja wake.
Mpaka kufikia hapo, wakala wa forodha atakuwa ameshapata nyaraka za kupata na kutolea mzigo. Wakala wa forodha atatakiwa aziwasilishe nyaraka hizo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa njia ya mfumo wa bandari wa kielektroniki ili kupata tozo za bandari.
Wakati wakala wa forodha atakapokuwa anafanya hivyo, wakala wa meli atakuwa tayari ameshatuma nyaraka au kibali cha kutolea mzigo (delivery order) kwenye mtandao wa TPA kwa lengo la kumtambulisha na kumthibitisha wakala wa forodha kwamba ndiye atakayehusika kutoa mzigo wa mteja ulioletwa na meli ya kampuni yake.
Kulipa tozo za bandari
Baada ya nyaraka hizo kuwasilishwa kwa njia ya kielektroniki, TPA itazifanyia tathmini ya gharama za huduma ambazo imezitoa kwa mzigo kupata tozo za bandari kwa mzigo wa mteja, na ikishakamilisha itampelekea wakala wa forodha kwa njia ya kielektroniki kwa kumpatia namba ya kumbukumbu kwa ajili ya kulipia (payment reference number).
Akishapata namba ya kumbukumbu ya kulipia, wakala wa forodha atatakiwa kulipia tozo za bandari kupitia benki mojawapo kati ya TIB, NMB, CRDB na Standard Chartered au kwa njia ya simu.
Wakala wa forodha baada ya kulipia tozo za bandari malipo hayo yatakuwa yameonekana moja kwa moja kwenye mtandao wa TPA.
Wakala wa Forodha kuchukua mzigo wa mteja wake bandarini
Baada ya kukamilisha malipo ya tozo za bandari, hatua inayofuata sasa ni wakala kuchukua mzigo wa mteja wake. Hatua ya kuchukua mzigo ni muhimu kuielewa sana. Endapo mzigo unaotakiwa kutolewa bandarini ni wa kuchukuliwa na lori, wakala wa forodha atatakiwa kuingia kwenye mfumo wa TPA ili kujaza taarifa za namba ya lori litakalochukua mzigo, jina la dereva na namba ya leseni ya dereva. Iwapo mzigo unaochukuliwa ni gari linalotembea lenyewe, wakala wa forodha atatakiwa kuingiza kwenye mfumo wa TPA jina la dereva na namba ya leseni ya dereva.
Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hizo kwenye mfumo wa TPA, wakala wa forodha atapata kibali kwa ajili ya lori husika au dereva husika ili kuingia bandarini kuchukua mzigo. Lori likishapakiwa na taratibu za ukaguzi wa mwisho kufanyika, lori likiwa na mzigo wa mteja litaruhusiwa kutoka bandarini, au dereva akiwa na gari jipya ataruhusiwa kutoka bandarini na gari la mteja.
Iwapo una tatizo au swali kuhusiana na huduma za bandari usisite kuwasiliana nasi kwa kupiga simu au kutuma meseji za bure kupitia namba 0800110032 au 0800110047.