Na Dk. Reubeni Lumbagala, JamhuriMedia, Dodoma

Ukosefu wa ajira ni moja ya tatizo linaloikabili nchi yetu na kimsingi si Tanzania pekee bali na nchi nyingi duniani. Kutokana na tatizo hili, hatua madhubuti na stahiki zimekuwa zikichukuliwa na wadau wote muhimu yaani serikali, sekta binafsi, jamii na vijana wenyewe ili kuhakikisha kuwa fursa za kazi na ajira zinaongezeka ili kupunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa.

Uwepo wa idadi kubwa ya vijana mtaani huku kukiwa na fursa chache za ajira si jambo lenye afya. Ninajua serikali haijalala, inaendelea kuumiza kichwa katika kutatua tatizo hili na hata ule mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ni sehemu ya kupambana na changamoto ya ajira nchini. Na wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete kuhakikisha vijana wanapata kazi.

Rais alisema: “Kazi yako kubwa kwenye ile wizara ni uratibu wa kuhakikisha vijana wanapata ajira zao. Kunakuwa na uzalishaji wa kazi katika sekta nyingine, kilimo, madini, uvuvi kote kuna ajira kwa vijana. Nataka ukawe mratibu na ukahakikishe kila sekta inatoa ajira kwa Vijana na tukikuuliza Ridhiwani mpaka kufikia Desemba mwaka huu kama tupo Januari mwakani, tumetengeneza ajira ngapi uniambie kwenye finger tips kisekta, kilimo wapo hivi, ndio kazi yako. Kazi yako sio wewe kutengeneza ajira kwa vijana, kazi yako ni kuhakikisha sekta zinatengeneza ajira kwa vijana nawe unaratibu kazi lakini na haki zao.”

Kimsingi, mafanikio katika sekta ya elimu nchini kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo na vyuon vikuu yamechangia ongezeko kubwa la wahitimu.

Kumekuwa na uboreshaji mkubwa wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku serikali ikibeba mzingo wa kutoa ruzuku ya elimumsingi bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ili kutoa fursa sawa kwa watoto na vijana wa Kitanzania kupata elimu bila vikwazo.

Na pale wanafunzi hao wanapofanya vyema katika mithani ya kidato cha sita na hatimaye kuendelea na masomo ya shahada katika vyuo vikuu, serikali imekuwa ikitoa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Haya yote yanafanyika kwa nia njema kabisa kuhakikisha vijana wa Tanzania wanakuwa na maarifa, ujuzi na stadi stahiki za kuwawezesha kujitegemea.

Moja ya changamoto katika mfumo wetu wa elimu kabla ya maboresho ya mitaala yaliyofanyika ilikuwa ni ukosefu wa ujuzi wa kuwezesha vijana kuajiriwa au kujiajiri wenyewe baada ya elimu zao na wengine hata baada ya kozi.

Ni wazi wahitimu wa hatua mbalimbali wamekuwa wakiandaliwa kuajiriwa bila kuwa na stadi na ujuzi wa kujiajiri, hali hii ikapelekea Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za kuziba udhaifu huu kwa kufanya maboresho ya mitaala ambapo sasa mafunzo ya amali yanapewa msukumo mkubwa ili kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na ujuzi wa kuwasaidia kujitegemea bila kutegemea ajira rasmi.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni taasisi yenye dhamana ya kuchochea maendeleo ya elimu nchini kwa kutoa mikopo lakini pia kuwasaidia wanufaika wake wa mikopo kuwa na ujuzi stahiki ambao utakuwa nyenzo muhimu ya kuajiriwa na kujiajiri na hatimaye kuwa na uwezo wa kurejesha mikopo waliyokopeshwa.

Ni katika muktadha wa kuwajengea uwezo wahitimu ili kuajiriwa kirahisi au kujiajiri, Bodi imeandaa mafunzo rasmi ya kuwasaidia wahitimu ili wawe na ujuzi ambao ni mtaji muhimu katika maisha yao, hasa baada ya kuhitimu masomo yao.

Bodi kwa kushirikiana na taasisi ya Adanian Labs wameandaa mafunzo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho na wahitimu katika michepuo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) na sayansi ya kompyuta ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa na hivyo kuwa na vipato ambavyo pamoja na kuendesha maisha yao, watachangia maendeleo ya uchumi wa nchi lakini pia watakuwa na uwezo wa kurejesha fedha walizokopeshwa vyuoni.

Hivyo basi, Bodi, mbali ya kutoa mikopo na kuwadai wanufaika wake, sasa imeamua kujiongeza na kufanya jitihada za kuwatafutia fursa wanufaika wake ili wawe na uwezo wa kurejesha fedha na hatimaye wengine waweze kusoma kupitia marejesho ya fedha zao. Hii ni hatua murua na ya kupongeza sana.

Mafunzo haya muhimu yenye lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa mwaka wa mwisho na wahitimu wa fani za Tehama na kompyuta ambao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu yatasaidia sana kuwaongezea umahiri, stadi na ujuzi ambao ni muhimu sana katika kujitegemea kiuchumi badala ya kubaki nyumbani wakisubiri ajira rasmi serikalini au katika sekta binafsi.

Mafunzo haya yatatolewa bure kwa njia ya mtandao kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Agosti 5, 2024. Kwa kuwa mafunzo haya yataendeshwa kwa njia ya mtandao, kila mwombaji anapaswa kuwa na kompyuta na intaneti ili kuweza kujifunza kikamilifu na kupata ujuzi na stadi muhimu.

Kwa ushindani uliopo sasa katika soko la ajira, mhitimu mwenye ujuzi wa kutosha anajiweka katika nafasi nzuri ya kuajiriwa na kujiajiri na ndiyo maana taasisi mbalimbali zinashauriwa kutoa fursa kwa wahitimu kujitolea katika taasisi zao ili kuwaongezea ujuzi wanafunzi na wahitimu kwani ujuzi huo ni muhimu katika kujitegemea kiuchumi.

Sanjari na hilo, uamuzi wa Bodi ya Mikopo kushirikisha wadau wengine kuwajengea uwezo wanafunzi na wahitimu ni wa kupongezwa kwani unasaidia moja kwa moja kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wa Tanzania kwa kuhakikisha wanapata ujuzi na stadi kuendana na mazingira, ushindani na soko la ajira.

Kwa wataalamu wa Tehama na kompyuta jitokezeni kwani fursa hii si ya kuichezea, ombeni kujiunga na mafunzo haya ili mjiongezee uwezo na ujuzi na hatimaye muwe na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kulipa fedha mlizosomeshwa kwa maendeleo ya nchi yetu.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.

Please follow and like us:
Pin Share