Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Nambatatu), ameomba na kupewa uraia, JAMHURI linathibitisha.
Kiboye ambaye anajulikana pia kwa jina la Jared Samweli Kiboye, amepewa uraia wa Tanzania mwaka jana baada ya kubainika kuwa alikuwa Mkenya.
Hayo yalibainika wakati alipopeleka maombi ya kupatiwa Kitambulisho cha Taifa. Wananchi kadhaa wa Rorya na Tarime walimwekea pingamizi.
Kutokana na pingamizi hilo, Idara ya Uhamiaji ilimtaka athibitishe uraia wake.
“Hakutaka malumbano makali, akakiri kuwa kweli hakuzaliwa Tanzania. Akaanza taratibu za kuomba uraia na kufanikiwa mwaka jana,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:
“Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa Kiboye ni raia wa Kenya na si raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura 357, Rejeo la 2002.”
Taarifa hiyo imesema mwanasiasa huyo machachari jukwaani amefuata taratibu zinazotakiwa kisheria za kuomba na hatimaye kupewa uraia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.
Amepewa uraia wa Tanzania wa tajnis (naturalization) kwa cheti Na. 0004230 cha Mei, mwaka jana.
Kwa kufanikiwa kupata uraia, sasa Kiboye anaruhusiwa kuomba na kupewa kitambulisho cha uraia cha Tanzania; pamoja na haki nyingine, lakini si kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa za Idara ya Uhamiaji zinaonyesha kuwa Kiboye ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Msati Highway, Kata ya Nyamisangura, anatoka ukoo wa Kijaluo unaoitwa Kakienja ulioko Homabay nchini Kenya.
Mwanzoni, aliyekuja ni baba yake na watoto akiwamo [Kiboye]. Baba yake alitambuliwa na kuorodheshwa kwenye daftari maalumu la wahamiaji haramu mwaka 2004 wilayani Tarime.
Mwaka jana, katika toleo Na. 345, JAMHURI liliandika juu ya utata wa uraia wa mwenyekiti huyo, sababu iliyomfanya anyimwe hati ya kusafiria kwenda nchini China kwenye ziara ya mafunzo akiwa na wenzake kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Alizungumza na JAMHURI na kurusha lawama kwa wapinzani wake wa kisiasa, akisema wameshupalia suala hilo huku wakitambua kuwa yeye amezaliwa, amesoma na kufanya shughuli zote nchini Tanzania.
“Sitaki nilisemee jambo hilo sana kwa sababu liko kwenye mikono ya wakubwa huko. Naomba uwaulize hao wakubwa wao wataongea,” amesema.
Akitaja majina ya hao anaosema ni wakubwa (JAMHURI linahifadhi majina yao), alisema: “Sasa wewe ukiongea na wakubwa hao watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukuambia kinachoendelea. Mimi sijawahi kuwa raia wa Kenya bwana, ndiyo maana nimekwambia waulize hao wakubwa watakwambia.
“Vita niliyonayo si ya kawaida, mimi sijawahi kuwa Mkenya hata siku moja, hayo ni maneno tu watu wanasema. Ndiyo maana nimekwambia ongea na hao wakubwa watasema. Mimi ni Mtanzania, nimezaliwa Tanzania. Bibi yangu mzaa baba yangu ni Mtanzania, sheria inasema mmoja wa wazazi akiwa ni Mtanzania hata mtoto ni Mtanzania.
“Mimi nimezaliwa Tanzania, nimekulia Tanzania na nimesoma hapa hapa. Baba yangu nilimuuliza, maana sikuwa nayajua hayo, mimi nimesoma Shule ya Msingi Ryagati, lakini sasa kilichotokea ni kwamba nilimuuliza baba yangu, maana yeye anasema ni Mtanzania.
“Lakini jambo la uraia wangu lilianza wakati wa kampeni za urais, nikiwa Katibu Mwenezi wa Wilaya [Rorya], sasa wale wakawa wanalazimisha niunge mkono upinzani.
“Mimi sikumuunga mkono, jitihada za waliokuwa viongozi wangu wa mkoa na wilaya, maana wao walitaka nimpigie debe Edward Lowassa, walikuwa wameteka kila mtu huku Mara. Baada ya kuwakatalia mpango wao ndipo wakaanza kunitengenezea zengwe la uraia.”
Hata hivyo, Kiboye anakiri kuwa baba yake aliingia Tanzania akiwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu.
“Mimi baba yangu amekuja Tanzania akiwa na umri wa miaka mitatu, baada ya bibi yangu kuachana na babu, bibi huyo alikuwa Mtanzania na baada ya kurudi Tanzania, bibi akafa. Baba yangu amekuja hapa kabla ya Uhuru, na hata serikali ilisema watu wote waliokutwa wakati wa Uhuru wote ni raia, sasa nashangaa mambo haya yametoka wapi tena!
“Sasa baada ya kuniambia bibi alikuja hapa Tanzania akiwa amembeba baba yangu mgongoni, mpaka alishiriki kumwondoa mkoloni hapa… anasema walitangaziwa na Rais Julius Nyerere kwamba watu wote waliokutwa hapa na Uhuru, wote ni raia.
“Hii juzi tena imeibuka, na mpaka imeniacha hoi na sasa nimechoka. Nilikwenda kuongea na baba yangu ambaye sasa ana umri wa miaka 85 na mama yangu ana umri wa miaka 82. Hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi [wa wakati huo], Dk. Mwigulu Nchemba, nilimwambia haya ninayokuambia,” alisema Kiboye.
Kuhusu majina mawili – Jared Samweli Kiboye na Samwel Kiboye Nambatatu, anasema: “Hilo la Jared ndilo nimesomea. Sasa mimi niliamua kwenda mahakamani nikaomba nitumie majina yote mawili, nikasema naomba majina yote yawe yangu, hasa baada ya kuona jina la Samwel Kiboye Nambatatu limekuwa maarufu sana, mimi ni mwanasiasa, jina ambalo linaeleweka sana ni mtaji kwenye siasa.
“Hapo sasa ndiyo nikaamua kuachana na jina la Jared, lakini hilo ni jina ambalo nimesomea shule ya msingi, lakini likaja kumezwa na Samwel Kiboye, watu wamekuwa wakiniita Samwel…Samwel…Samwel… Ikabidi niombe kubadili jina, sasa jina la ‘Nambatatu’ ndilo limenipa ujiko, sasa kama nisingeomba kibali cha mahakama kubadili jina mimi ningeanguka maana hilo linafahamika sana.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alipoulizwa mwaka jana kuhusu uraia wa Kiboye, alijibu: “Huyu ni kiongozi wa CCM wa miaka mingi, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Wilaya, Mwenezi wa Mkoa, alikuwa Umoja wa Vijana… mimi namfahamu Nambatatu, muda mrefu, nimekataa kulishabikia suala la uraia wake maana ni majungu tu. JAMHURI ni ka-gazeti kadogo ambako kanaibua mambo mazito mazito, ni ka-gazeti ambako watu serious [makini] kama mimi tunakosoma. Sitarajii na ninyi mtakuwa kwenye mwendelezo wa majungu, ninakuhakikishia kwamba sina taarifa hiyo, na huwezi kuwa mwenyekiti wa CCM kama si raia. Kuna watu aligombea nao akawachapa, nadhani ndio wanaleta jambo hili na ninaamini ni majungu tu.”