Yapo mengi ambayo ningependa niwashirikishe wasomaji wa Safu hii. Wiki kadhaa zilizopita, makala yangu moja iliibua mjadala. Ilihusu Katiba mpya.
Msimamo wangu si kupinga Katiba mpya, lakini bado naamini Katiba mpya pekee si suluhisho la matatizo yote yanayoikabili nchi yetu.
Nitaendelea kuamini kuwa matatizo mengi ya Tanzania ni zaidi ya Katiba mpya! Hatuna viongozi wawajibikaji, na kwa sababu hiyo wananchi nasi tumebaki tukifanya mambo mengi ya hovyo hovyo, huku tukisingizia ukosefu wa Katiba mpya!
Juzi, nimekutana na mwalimu wangu wa kitaaluma, Jenerali Ulimwengu. Hakuwa mbali na ukweli wa yale niliyoyasema. Aliniambia: “Huhitaji Katiba mpya kuwakamata wezi”.
Hapa ndipo unapoona kuwa kumbe kuwakamata wezi wa makontena na wakwepa kodi si lazima tusubiri Katiba mpya. Yapo mengi tunayoweza kuyafanya wakati tukisubiri hiyo Katiba mpya.
Pili, ningependa nirejee pongezi zangu za dhati kwa Rais John Magufuli, kwa kuisuka Wizara ya Maliasili na Utalii. Ameliokoa Taifa kwa kuwaondoa manabii wa wizi na hujuma za rasilimali za nchi yetu. Kuna makala nyingi na ndefu nitakazoandika kama ushauri wangu kwa viongozi wapya – Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Kwa sasa itoshe kusema, asante sana Ndugu Rais.
Tumeufunga mwaka 2015 na kuuanza Mwaka Mpya kukiwa na mjadala mwingine nchini. Unahusu ubomoaji majengo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria. Miji kadhaa, ikiwamo Dar es Salaam na Mwanza, imeshaonja shubiri hiyo.
Mtu aliyepata jeraha kubwa linalostahili kushonwa, huhitaji sindano yenye dawa ya ganzi. Ganzi, kwa kadri tulivyozoea kwa teknolojia ya miaka mingi, humwingia mtu kwa kudungwa sindano. Sindano iliyojazwa ganzi hudungwa mwilini na kusababisha maumivu ya muda mfupi tu kabla haijaanza kufanya kazi yake.
Sindano moja anayochomwa mgonjwa anayehitaji huduma ya kushonwa majeraha ni ya maana na muhimu sana kwa sababu inamwezesha kuepuka maumivu mengi ambayo angeyapata endapo angeshonwa bila kutiwa ganzi. Kwa maneno mengine, mgonjwa hawezi kuyakubali maumivu makali na marefu eti kwa kukataa kudungwa sindano moja ya ganzi!
Sishangilii adha wanazopata wananchi wanaohamishwa kutoka maeneo waliyojenga kinyume cha sheria. Hata hivyo, naunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuipanga miji yetu. Kama ilivyo sindano ya ganzi, faida za kuondolewa kwa watu walio maeneo hayo kwa baadaye ni kubwa kuliko malalamiko yao na ya ‘wanaojiita watetezi wa haki za binadamu’.
Wakati wa ujenzi wa Barabara ya Ubungo-Mlandizi, yalikuwapo malalamiko kama haya ya sasa ya wanaoishi mabondeni. Serikali ilichukua uamuzi mgumu kwa kuwahamisha wananchi walioishi ndani ya hifadhi ya barabara kinyume cha sheria. Ulikuwa uamuzi mchungu, lakini faida zake zimegusa wengi zaidi.
Kama nchi, hatuna budi kuwa na Serikali yenye nia ya dhati katika kuleta mabadiliko yenye tija kwa watu wengi zaidi.
Natambua wapo wanaohoji: “Kwanini wa mabondeni waondolewe? Kama ni mafuriko, si watakufa wao?” Hizi ni fikra dhaifu. Kwanza, hatuna hakika endapo wote watakaokumbwa na mafuriko watafariki dunia! Wapo watakaojeruhiwa. Kuwatibu majeruhi ni gharama kwa ndugu na kwa Taifa. Tunapowaona polisi wakisisitiza matumizi ya kufunga mikanda katika magari au kuvaa kofia ngumu kwenye bodaboda, wanafanya hivyo kwa sababu kuu ya kulinda uhai wa wananchi. Lakini kuna sababu nyingine zaidi ya hiyo.
Nayo ni kwamba gharama ya kumtibu abiria aliyekaidi kufunga mkanda au kuvaa kofia ngumu, ni kubwa kuliko gharama ya kuwatumia polisi kusimamia nidhamu hiyo katika vyombo vya usafiri. Watu wanapoumia kwa uzembe, wanaobeba gharama ni walipa kodi hata kama watatibiwa na ndugu. Dawa zinaagizwa kwa fedha za kigeni. Tukipunguza ajali zinazosababishwa na uzembe, maana yake tunapunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuokoa nguvu kazi.
Hivyo hivyo, kuwahamisha watu wanaoishi mabondeni ni kuliepushia Taifa hasara kubwa. Vifo, maradhi na madhara mengine wanayopata watu wanaoishi sehemu zisizostahili athari zake zinavuka hadi kwa wale wasioishi maeneo hayo.
Kama nchi, tunapaswa tuwe na mahali pa kuanzia. Kabla ya kuzuru mataifa yaliyoendelea, nilidhani sifa ya mataifa hayo ni wingi wa viwanda, magari, majengo marefu na mazuri, ukwasi wa wananchi katika mataifa hayo, na kadhalika. Lakini nilipofika huko nikabaini kuwa nchi kuendelea ni zaidi ya hayo. Mpangilio mzuri wa miji ni sehemu ya vigezo vya taifa lililoendelea. Kwa ufupi, kigezo kimojawapo cha kuwaweka watu wa taifa fulani kwenye kundi la walioendelea au ambao hawajaendelea ni aina ya mpangilio wao wa mambo mbalimbali, yakiwamo makazi.
Mji wa Kigali nchini Rwanda sasa unatajwa kama mji msafi na uliopangiliwa vizuri katika Afrika. Ni mji unaomfanya mgeni anayetoka Ulaya au Asia, akastaajabu na kuondokana na ile dhana ya kwamba hakuna lililo zuri au jema katika Afrika. Hapa kwetu ukisifu maendeleo ya Rwanda, utaambiwa kwa sababu Rwanda ni nchi ndogo! Kama udogo ni hoja, basi Tanzania ingekuwa mbele kuliko Marekani yenye watu zaidi ya milioni 360. Tanzania yenye watu milioni 45 ingekuwa mbele kabisa kimaendeleo kuliko China yenye watu bilioni 1.4. Uchache si hoja, bali muhimu ni mipangilio ya maendeleo.
Mipangilio ya miji ni mipangilio ya maisha. Mpangilio wa mji unatosha kabisa kumwezesha mgeni kuzijua akili za wenyeji wake. Mazingira ya nyumbani kwangu yanatosha kabisa kumfanya mgeni, bila kupewa mhadhara, atambue mimi ni mtu wa aina gani.
Unapoingia nyumbani kwa mtu ukakuta sebuleni kumetundikwa sidiria na nguo za ndani, utakuwa umeshajua aina ya akili za watu wanaoishi katika nyumba hiyo.
Unapoingia katika nyumba ukakuta watu wazima wameweka viatu kwenye jokofu, hutahitaji jirani wa kukueleza mtindio wa akili walionao wenye nyumba hiyo.
Lakini hata mama mwenye nyumba anapoajiri mfanyakazi wa ndani, anajua wajibu wa mfanyakazi huyo ni kufanya usafi maliwatoni ambako ndiko kunakostahili kimpangilio kutumiwa kwa haja. Lakini ukikuta mama mwenye nyumba anajisaidia sebuleni au barazani kwa sababu tu anajua yupo mwajiriwa wa kuondoa uchafu huo, utashangaa kwa nini hajahamishiwa Mirembe!
Tena si kawaida kwa kijana mwenye mzuzu kutaka kuwa na ubia wa matumizi ya chumba cha wazazi wake. Mzazi atoke matembezi, amkute kijana ‘kawahi’ chumbani kwa wazazi wake, amejipumzisha bila wasi wasi wowote, mzazi mwenye weledi atajua mwanae ana kasoro.
Hivyo hivyo, wageni wanaozuru nchini mwetu wanapokutana na ujenzi huu au mipango miji yetu, si tu wanatushangaa, lakini pia wana haki ya kushauri tupimwe akili maana binadamu mwenye utashi hawezi kuishi hovyo kuliko mnyama asiye na utashi.
Lakini wageni hao watatushangaa zaidi pale wanapobaini kuwa kuna wananchi wanaofanya juhudi za kuwakwamisha wale wanaothubutu kuiweka miji yetu katika mpangilio wa kibinadamu.
Watu waungwana wangeungana na Serikali katika kuhakikisha kuwa miji yetu inafumuliwa na kupangiliwa upya ili si tu ivutie machoni pa wageni na wenyeji, lakini hatua hiyo isaidie wakati wa ukoaji au upelekaji huduma muhimu kama za maji na kadhalika kwa wananchi.
Hali ilivyo leo kwenye miji yetu ni ya kushangaza na kutia hasira. Nyumba ikiwaka moto hakuna namna gari la zimamoto litakavyoweza kuifikia. Hakuna mgeni anayezuru kwa jamaa yake bila kupokewa na mwenyeji maana hakuna mitaa wala barabara za kumwezesha kufika mwenyewe. Hii ni aibu katika dunia ya watu waliostaarabika.
Ipo hoja dhaifu ya kwamba Serikali ilikuwa wapi hadi watu wakajenga mabondeni au katika maeneo mengine yasiyoruhusiwa. Tena basi, wengine wanakwenda mbali zaidi na kuhoji kwamba kama walijenga sehemu zisizostahili, kwanini walipelekewa huduma kama maji na umeme?
Hizi ni hoja dhaifu. Ni dhaifu kwa sababu tulipoamua kuwa na utaratibu wa Serikali mpya kila baada ya miaka mitano, tulifanya hivyo kwa lengo la kupata mabadiliko chanya.
Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa na udhaifu wake ambao Serikali ya Awamu ya Tano ina wajibu halali wa kuurekebisha. Haiwezekani makosa yaliyofanywa na awamu zilizopita yakabarikiwa kwa sababu yalitendwa na Serikali. Kwanini swali hili liulizwe tu kwenye ubomoaji majengo yaliyojengwa sehemu zisizostahili?
Kwanini hatuhoji kwenye makontena ambako mabilioni ya shilingi sasa yanakusanywa? Nani anaweza kusimama na kuhoji uhalali wa Serikali ya sasa kubana wafanyabiashara hao wa makontena kulipa kodi waliyokwepa wakati wa Awamu ya Nne? Je, waachwe kwa sababu makosa yaliyofanywa na Serikali iliyopita yanastahili kuhalalishwa?
Kwa miaka 10 tulikuwa na Serikali iliyolegea. Watu walijitwalia maeneo ya wazi. Wakajenga bila hofu yoyote. Waliojenga sehemu zisizostahili walipelekewa umeme na huduma nyingine kwa rushwa.
Maeneo ya wazi yamevamiwa. Viwanja vya michezo vimeporwa na kujengwa nyumba za kuishi, kumbi za starehe na hata makanisa ya kibiashara. Barabara za mitaa zimefungwa kwa sababu matajiri fulani hawataki watu wapite jirani na nyumba zao. Maeneo ya makaburi yamevamiwa. Sehemu za kuzikia zimepungua.
Mafuriko katika maeneo kama Msasani ni mambo yaliyohalalishwa na wanasiasa na watendaji wala rushwa. Njia za maji zimefungwa. Mvua zikinyesha nusu saa jiji linamezwa! Shule na huduma nyingine za kijamii zinafungwa. Je, Rais Magufuli na wasaidizi wake wawe wazembe hata waruhusu adha hizi ziendelee kuwasumbua Watanzania wengi? Tunatoa wapi uhalali wa kupinga jambo hili?
Watendaji wa mipango miji wamepuuzwa. Wanasiasa, hasa madiwani ndiyo chanzo kikuu cha upuuzi huu. Watendaji wanapotaka kuwaondoa wavamizi, wanasiasa wamejitokeza kusema “waacheni, hawa ni wapiga kura wetu”. Kwao, kupata kura ni kwa maana zaidi kuliko uhai na ustaarabu katika jamii.
Wapo wanaohoji kwamba wa mabondeni wanaoondolewa wataenda kuishi wapi? Nami nawauliza, kabla ya kuvamia maeneo hayo walikuwa wakiishi wapi? Je, tukubali sasa wamachinga watundike mitumba kwenye ukuta wa Ikulu na wakiondolewa wahoji wataenda wapi? Nani kasema Tanzania imejaa hadi pomoni kiasi cha watu kukosa sehemu za kuishi?
Mwisho, nasema uamuzi wa kuipanga miji na hata vijiji vyetu ni uamuzi sahihi. Yeyote anayependa ustaarabu ataunga mkono uamuzi huu wa Serikali. Lakini ili uamuzi huu uwe na tija, yale mahekalu ya wakubwa yakishushwa, hawa wa Jangwani wataondoka wenyewe maana watajua Serikali imedhamiria. Kama nyegere wanaishi kwa mpangilio, seuze binadamu?
Kuijenga nchi kuna gharama zake. Moja ya gharama hizo ni kuwapanga walioamua kuishi nje ya mpangilio.