Kuna taarifa kwamba kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, inakusudia kumleta raia wa Kenya kuwa Mkurugenzi Mkuu!
Sijadili kwa sababu anayekusudiwa kuletwa ni Mkenya, la hasha! Najadili hoja hii kwa sababu siamini kama Watanzania, kwa mamilioni tumemkosa mmoja wa kuiongoza kampuni hii. Na hapa tukumbuke tunaletewa mgeni kuongoza kampuni licha ya kwamba tuna miaka takribani 57 ya kuwa taifa huru lenye wasomi wa kila kada.
Kampuni ya Vodacom, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mwaka jana ilikuwa na wateja milioni 12.4. Hii imeiwezesha kuwa na asilimia 31 ya ‘market share’. Ina wanahisa zaidi ya 40,000. Inafanya miamala ya M-Pesa ya wastani wa Sh trilioni 2.6 kwa mwezi.
Ndugu zangu, kwa takwimu hizi tutakubaliana kuwa hii si kampuni ndogo au ya kuachwa iingie mikononi mwa watu tunaotambua kuwa ni washindani wetu wakubwa.
Kila mara sikosi mada yenye maudhui ya kuwahadharisha Watanzania kwa ujanja-ujanja unaofanywa na Wakenya. Tunazungumza ushirikiano, sawa hili ni jambo jema sana. Sisi tunaounga mkono Umajui wa Afrika tungependa kuiona Afrika inatimiza ndoto ya waasisi ya kuwafanya Waafrika kuwa kitu kimoja. Tungependa kuona tunaondosha vikwazo vya wananchi kusafiri, kufanya biashara na shughuli nyingine kwa uhuru ndani ya Afrika, lakini siyo kwamba kuifanya Tanzania kuwa uwanja wa kuongozwa hata kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu. Ushirikiano una mipaka yake. Hata mgeni anapoingia nyumbani kuna sehemu haruhusiwi kuingia, na hiyo si kwa sababu ya roho mbaya ya mwenyeji wake, bali ni kutokana na misingi ya kimaadili tu.
Afrika tunataka iwe moja. Huko ndiko tunakokusidia kwenda, lakini kabla ya kuingia kichwa kichwa, hatuna budi kujiandaa kwa kuhakikisha tunajijengea uwezo- na kubwa zaidi kwenye hoja hii ni kwa Watanzania wenyewe kujiamini na kujiona kuwa tunaweza kufanya yale tunayoweza kuyafanya. Tusipoweza, tuombe msaada wa wageni.
Historia ya Wakenya dhidi ya Watanzania ina mtanziko usiohitaji shahada kuutambua. Wametuulia vitu vingi chini ya uongozi wao hapa nchini. Wapo wanaokumbuka namna aliyekuwa kiongozi wa Precision Air alivyoitendea kampuni hiyo. Precision Air ilichungulia kaburi kabla ya kurejeshwa kwa Watanzania.
Nimesoma andiko linalowahadharisha Watanzania dhidi ya mbinu za Kenya. Kiwanda pekee cha kutengeneza transforma cha TANELEC kilikabidhiwa uongozi wa Wakenya kikiwa kinawika kwa kutengeneza transfoma nzuri mno ndani na nje ya Afrika. Wakenya wamekiua.
Kiwanda cha Bia cha Kibo (Kibo Breweries) kilichukuliwa na African Breweries chini ya Mkurugenzi Mkuu kutoka Kenya, mwisho wake kilifungwa. Kiwanda cha Bia cha Serengeti kilichochukuliwa na East African Breweries kimeonja machungu ya Wakenya. Zitto Kabwe naye anasema baada ya kuchukua kiwanda hicho, Wakenya wakahaha kuhakikisha kinayumba ili bia yao aina ya Tusker ipate soko nchini Tanzania. Bia za Serengeti hazina umaarufu ule tulioujua. Soko lake la hisa la asilimia 15 limepotea. Hisa za Serengeti zimepungua na kufikia asilimia 7 kwa sasa.
Ukiyatazama yote haya unaona kuwa huwa hayatokei kwa bahati mbaya, bali ni mkakati wa Wakenya kuiumiza Tanzania na wakati huo huo kutufanya sisi kuwa soko lao.
Mwaka 2008, nikiwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrrika Mashariki, Dk. Diodorus Kiwanda, tulizuru kiwanda cha Maziwa cha Arusha (Arusha Diary) kilichokabidhiwa wawekezaji, kampuni ya Brookside ambayo ni ya Rais Uhuru Kenyatta.
Makubaliano ya uwekezaji yalikuwa kuhakikisha kiwanda hicho kinapata mashine za kisasa zaidi ili kiweze kukidhi viwango cha kimataifa. Arusha Diary ilichukuliwa ikiwa inafanya kazi vizuri kabisa.
Hilo la kuwekwa mashine mpya halikufanywa, badala yake majengo yakageuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia maziwa ya Brookside kutoka Kenya. Kuna uhuni mkubwa sana ulifanywa (sina hakika kama umeachwa). Walihakikisha wananunua maziwa kutoka kwa wafugaji mkoani Arusha. Wakayasafirisha hadi Nairobi. Yakasindikwa na kisha yakarejeshwa kwenye maghala Arusha tayari kuyauza kwa Watanzania.
Pale mpakani Namanga hawakulipa ushuru kwa kigezo kwamba malighafi iliyotumika ilitoka Tanzania kwa hiyo ‘kisheria’ hawakutakiwa kulipa ushuru. Kukawapo malori mengi yanayopeleka maziwa ghafi Kenya na kuyarejesha Tanzania yakiwa yameshasindikwa. Ajira wakachukua Wakenya.
Matokeo ya uharamia huo wa kibiashara yakawa kuumia kwa wafugaji Watanzania kwani bei ya maziwa ilishuka mno. Serikali ilikosa mapato, na Tanzania ikageuzwa kuwa ghala na soko la maziwa yake, lakini faida ikaishia Kenya.
Ukweli ni kuwa kiwanda kile kilifanyiwa songombingo kife ili Tanzania ibaki kuwa soko la Kenya. Wakati huo huo kiwanda cha maziwa cha Musoma Milk kilichokuwa kikimilikiwa na Dk. Gideon Mazara, bidhaa zake zikazuiwa kuingizwa Kenya. Wengi walioonja au kunywa maziwa ya Musoma Milk wanatambua ladha na ubora wa maziwa hayo.
Kenya wana kampuni za simu kama ilivyo kwa Tanzania. Mpango huu wa kumleta Mkenya hautashangaza kuona matokeo yake yakilenga kuiua Vodacom Tanzania ili walikamate soko hili ‘jipya’.
Watanzania kinachotuumiza ni fitna tu sehemu za kazi, lakini uwezo wa kufanya kazi tunao, tena kwa viwango vya juu. Fitna zimetufanya tu-miss use watu wengi mno, na hilo linaweza kuwa sababu ya wengine kudhani dawa yake ni kuwaleta wageni.
Tunao Watanzania waliofanya mambo makubwa kwenye sekta binafsi na ya kutukuka. Mfano halisi ni Dk. Charles Kimei wa Benki ya CRDB. Hii benki ameifanya iwe fahari ya nchi yetu. Kwa namna Wakenya wanavyotubana sidhani kama wako radhi kuruhusu itambe nchini mwao.
Kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoongoza mashirika na kampuni kubwa huko nje. Wameaminiwa. Nchi yenye sifa ya kuwa na watu wa aina hiyo leo haiwezi kukubali kuona Wakenya wakiletwa kutuongoza. Nayasema haya si kwa sababu ya ubaguzi, bali kwa sababu ya kuona hata huo mshahara atakaolipwa Mkurugenzi wa Vodacom unabaki hapa hapa nchini kwa manufaa ya Tanzania na Watanzania.
Bado narejea kushauri kuwa Watanzania hatuna budi kuwa jeuri katika suala zima la maendeleo. Lazima tujiamini, na daima tujione kuwa tunaweza. Vodacom ina wenyewe wanaoimiliki, basi hao wenyewe waambiwe kuwa Watanzania wangependa kuona chombo hiki kinaongozwa na Watanzania wenzao. Nasisitiza kusema kuwa huu si ubaguzi, bali ni uzalendo.
Pale jijini Dar es Salaam kampuni kutoka Kenya ilipewa kazi ya kukusanya ushuru wa Jiji. Tukalaani, na kwa bahati nzuri nadhani mamlaka za Serikali ziliona tuna hoja. Mtu unajiuliza, kweli zabuni ya kukusanya ushuru wa maegesho (narudia-ushuru wa maegesho ya magari) lazima ifanywe na mgeni? Huku ni kujidhalilisha.
Lakini haishangazi kwa sababu ndivyo tulivyokubali tuwe. Ukiona hata barabara inayoingia Ikulu inapewa jina la rais wa taifa jingine, ujue tuna tatizo kubwa. Barabara au mtaa kupewa jina la kiongozi wa nchi fulani si jambo la ajabu. Ni la kawaida mno, lakini sidhani kama ilikuwa busara kwa barabara inayoingia na kutoka katika ‘nyumba namba moja ya nchi’ ikapewa jina la kiongozi wa taifa jingine.
Tulikosa jina moja kutoka kwenye kanzidata ya wazee wetu mashujaa waliopigania ukombozi wa taifa letu? Tulishindwa kuipa jina la Isike, Kingunge, Mkwawa, Marealle, Moris Nyunyusa, Kikwete, Mkapa, Job Lusinde, au hata King Majuto; badala yake tukaona jina linalostahili ni Barack Obama?
Mwito wangu ni kuona Watanzania tunajitambua na kujiamini. Nawaomba wanaohusika ‘kusajili wageni wafanyakazi’ wazuie usajili huu unaoombwa wa kumleta Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania kutoka Kenya. Hii ni fedheha. Tusiwe wanyonge kiasi cha kuchekwa na hata kupuuzwa na wenzetu. Heshima ya Watanzania itajengwa na Watanzania wenyewe. Tuanze sasa.