Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Watoto Hassan na Hussein Amri Jummane (3) waliozaliwa wakiwa wameungana kwenye nyonga, kifua na wana miguu mitatu sasa wamereja nchini baada ya kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa huko nchini Saudi Arabia.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Rachel Mhaville amesema watoto hao walipokelewa hospitalini hapo Agosti 2021 kutokea Igunga Tabora wakiwa na umri wa wiki mbili na kukaa hospitalini hapo miezi 11 wakipata matibabu mbalimbali na kuondoka kwenda nchini Saudi Arabia kwa ndege maalum Agosti 23, 2023 ili kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha.
Dkt. Mhaville amesema MNH ina uwezo wa kufanya upasuaji wa aina hiyo kutokana na wataalam na miundombinu iliyojitosheleza ila kutokana namna watoto hao walivyokuwa wameungana ilihitaji utaalam wa juu zaidi hivyo Serikali ya Saudi Arabia ilichukua jukumu ya kuwasafirisha ambapo tarehe 05 Oktoba, 2023 walifayiwa upasuaji huo uliodumu kwa saa 16.
Aidha Dkt. Mhaville ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada huo ambao umewarejesha watoto hao katika maisha ya kawaida na kuongeza kuwa watoto hao wataendelea kuwepo eneo la Muhimbili kwani bado wanaendelea na matibabu ya awamu mbalimbali kuboresha ustawi wa maisha yao.
Katika hatua nyingine Dkt. Mhaville amewataka Watanzania kujitolea kumjengea makazi bora mama wa watoto hao ambaye anatoka katika mazingira duni huko Igunga Tabora ili aweze kuwalea vizuri kulingana na hali walizo nazo.
Kwa upande wake Mama wa Watoto hao Bi. Hadija Shabani ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada wa matibabu ya kutenganisha watoto hao pamoja na Serikali ya Tanzania kwa jinsi ilivyoratibu zoezi la watoto hao kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.
Naye Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Watoto wa MNH Dkt. Zaituni Bokhary amesema jopo la madaktari wabobezi upasuaji wa mishipa ya damu, mfumo wa mkojo wa watoto walishiriki upasuaji huo uliofanyika hospitali ya King Abdulaziz iyopo Riyadh Saudi Arabia.