Tasnia ya urembo nchini imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Hashim Lundenga, maarufu kama “Uncle Hashim”, aliyefariki dunia leo jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

Lundenga alikuwa mwanzilishi na Mkurugenzi wa Lino International Agency, kampuni iliyosimamia mashindano ya Miss Tanzania kwa zaidi ya miaka 23.

Kupitia uongozi wake, mashindano haya yalipata umaarufu mkubwa kitaifa na kimataifa, yakitoa majukwaa kwa warembo wa Kitanzania kushiriki kwenye mashindano ya dunia kama Miss World.

Mwaka 2018, baada ya miongo miwili ya kuyasimamia, Lundenga alikabidhi rasmi uendeshaji wa Miss Tanzania kwa Basila Mwanukuzi, aliyewahi kushinda taji hilo mwaka 1998. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara iliyoathiri mwenendo wa mashindano hayo.

Mbali na mchango wake katika tasnia ya urembo, Lundenga pia alikuwa mshiriki hai katika maendeleo ya michezo nchini, hususan kupitia klabu ya Yanga, ambako alihudumu katika nafasi mbalimbali za kamati.

Alifahamika kwa uwezo wake wa kugundua na kukuza vipaji vya warembo, wakiwemo majina makubwa kama Jackline Ntuyabaliwe (K-Lyn), ambaye baadaye aliolewa na marehemu mjasiriamali maarufu Reginald Mengi, Millen Magese, Nancy Sumari, Faraja Kota (ambaye aliolewa na mmoja wa mawaziri), na Wema Sepetu miongoni mwa wengine wengi waliotamba kitaifa na kimataifa.

Kwa zaidi ya miongo miwili, Lundenga alibeba dira ya mashindano ya Miss Tanzania tangu yalipoanzishwa mwaka 1994, hadi alipojitoa rasmi kutokana na changamoto za kiuendeshaji.