Mfumo wa kufanya biashara wewe kama wewe ni wa zamani mno. Ukisoma hadithi zilizo ndani ya Kurani na Biblia utaona watu wa kale walitumia mfumo huu huu katika biashara zao ambao pia na wao waliukuta.
Ni mfumo ambao umezeeka kiuchumi, kisheria na kila nyanja. Baadaye watafiti wa uchumi na sheria wakaja na mfumo wa biashara kutoka mtu binafsi kwenda kampuni.
Hawa hawakuwa wajinga na wala hawakuwa wamekosea. Walizingatia zaidi faida anazoweza kupata mtu ikiwa atafanya biashara kutoka yeye kama yeye na kwenda kwenye mtindo wa kampuni. Pia ni sababu hii hii inaifanya serikali iwahimize wajasiriamali kurasimisha biashara. Kampuni ndiyo kurasimisha biashara. Mara nyingi tumeeleza katika makala kuwa kuunda na kuanzisha kampuni si jambo linalohitaji gharama kubwa kama wengi wanavyodhani. Si jambo lenye mchakato mrefu kama wengi wanavyodhani; na si jambo ambalo linawahusu matajiri na wenye biashara kubwa kama wengi wanavyodhani. Bali ni kinyume cha hayo yote. Ni kinyume cha hayo kwa maana kuwa hata shilingi laki mbili unaweza kuunda na kuanzisha kampuni. Kwa maana kuwa ndani ya wiki moja unaweza kuwa umekamilisha mchakato wa kuunda na kusajili kampuni na tayari ukawa na cheti chako cha kuzaliwa kwa kampuni (certificate of incorporation). Na kwa maana kuwa hata biashara yako ya kufuga kuku, maziwa, mayai unaweza kuifanya katika mtindo wa kampuni badala ya ule uliozoea wa kuwa wewe kama wewe. Sheria ya Makampuni, Namba 12 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2005 zimeeleza vizuri namna ya kuunda kampuni, namna ya kuendesha kampuni, aina za kampuni, tofauti ya kampuni na mifumo mingine ya kibiashara halikadhalika ni kwa vipi kampuni inakufa ukitaka kuachana nayo.
Kutoka katika sheria hiyo na nyinginezo, nitaeleza baadhi ya hasara za kufanya biashara nje ya kampuni kwa maana kufanya biashara ukiwa kama mtu binafsi.
1: Hasara za kufanya biashara nje ya kampuni
(a) Ni vigumu kupata mkopo. Sera za mikopo na sheria ndogondogo (by laws) za taasisi nyingi za fedha zinaepuka sana kufanya kazi na watu binafsi. Zimependelea zaidi kampuni. Zipo taasisi nyingine ziko wazi kabisa kuwa hazikopeshi kabisa kabisa mtu binafsi mpaka uwe katika kampuni.
Pia mabadiliko ya Sheria ya Mikopo ya mwaka 2008 ambayo yamebadilisha vipengele vya rehani katika Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 nayo yameongeza nguvu katika hili.
Na hata ikitokea mtu binafsi akakopesheka, basi huwa ni kiwango kidogo ambacho pengine hakiwezi kumpeleka kule anakotaka katika mafanikio makubwa zaidi tu ya kumwezesha kupata kipato cha kawaida cha kujikimu.
(b) Hakuna usalama katika mali zako binafsi. Ikiwa unafanya biashara kama mtu binafsi (sole proprietor) mali zako zote haziko salama hasa pale unapokuwa umekopa na bahati mbaya umeshindwa kurejesha. Mali yako yoyote ile pahali popote ilipo inaweza kukamatwa na kuuzwa kulipia deni.
Hii ni tofauti na kwenye kampuni ambako mali binafsi ya mmiliki wa kampuni haiwezi kukamatwa kulipia deni la kampuni. Mali za kampuni ndizo hutakiwa kukamatwa. Ni kwa sababu ya kanuni ya kisheria inayoitwa “limited liability” ambayo inamtenganisha mmiliki wa kampuni na kampuni yenyewe.
(c) Kushitakiwa kama mtu binafsi: Ikiwa unafanya biashara kama mtu binafsi lolote litakalotokea katika mchakato wa biashara iwe kuhusu masilahi ya wa/mfanyakazi, ajali au jambo lolote lile ambalo mtu anaweza kukupeleka mahakamani, basi utapelekwa wewe kama wewe na utatakiwa kujibu.
Lakini ni tofauti na ukiwa kwenye kampuni ambako hautashitakiwa wewe, bali kampuni. Na hatia itakuja kwa kampuni na si kwako mmiliki. Hata jina la mshitakiwa litaandikwa kampuni na si la kwako. Hii nayo ni kanuni ya kisheria iitwayo “capacity to sue or be sued”. Basi, unaweza kuwaza hii ni ahueni ya kiasi gani kwako mfanyabiashara.
(d) Biashara binafsi ukifa nayo imekufa. Si biashara endelevu, kwa kuwa kila kitu humtegemea huyo huyo mmiliki. Pia vitu kama TIN number (Namba ya Mlipakodi, jina la biashara, nk.) hivi navyo ukifa wanaochukua biashara yako ni lazima watafute vingine. Sheria inawakataza kutumia vile vya marehemu. Ni tofauti na kampuni ambako mtu akifa hubadilishi chochote. Kampuni inabaki vilevile na biashara inaendeea. Ni kanuni ya kisheria iitwayo ‘perpetual succession’. Hii ina faida hata kwenye mirathi japo haiwezi kuelezwa sasa kwa kuwa mada yake ni ndefu.
(e) Huwezi kupata wabia: Wabia wanaweza kuingia kwenye biashara yako kupitia njia mbili; ‘partnership’ au ‘joint venture’. Hasa wabia wageni ambao kisheria kuna vikwazo kwao katika kupata ardhi hapa Tanzania, hivyo kuwategemea wenyeji.
Ni kwamba, usitegemee kupata watu kama hawa ikiwa unafanya biashara kama mtu binafsi. Hawa huhitaji kampuni kwa sababu na wao pia huja kama kampuni. Kwa hiyo huhitaji makubaliano ya mikataba yawe kati ya kampuni na kampuni, na si kampuni na Masawe au Lutaijuka.
Hasara ni nyingi – nimetaja chache mno. Kwa ufupi mfumo wa biashara nje ya kampuni ni mfumo wa zamani mno yafaa uachane nao haraka.