Katibu Mkuu wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kwa dhamana ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Uchaguzi wa ndani ya chama unaonendelea huku ukifikia ngazi za mikoa chama na jumuiya, ametangaza kufuta uchaguzi katika baadhi ya maeneo, kusimamisha mchakato wa uchaguzi na kutuma timu za uchunguzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu tarehe 21 Novemba, 2022 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu amefuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu, kwa kuwepo na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wagombea na timu ya uchunguzi imeshatumwa kulifuatilia hilo kwa kina, na hatua zaidi zitachukuliwa haraka baada ya uchunguzi kukamilika.
Pia, Katibu Mkuu amesimamisha uchaguzi wa nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Mbeya na Arusha kwa sababu za kuwepo kwa tuhuma mbalimbali zikiwepo za rushwa, na sasa uchunguzi unaendelea na hatua zitachukulia.
Aidha, Katibu Mkuu ameeleza kuwa uchaguzi uliofanyika jana tarehe 20 Novemba, 2022 mkoa wa kichama wa Magharibi Zanzibar, kumekuwa na malalamiko kwa kitendo cha baadhi ya wanachama kubeba sanduku la kura na kulipeleka eneo la kuhesabia, hivyo timu ya uchunguzi inafuatilia na ikigundulika jambo hilo halikuwa na nia njema uchaguzi utafutwa na kuchukua hatua zaidi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu amewashukuru wanachama wote wa CCM kwa kuendelea na uchaguzi kwa amani na kwa utulivu mkubwa, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo ambapo Chama kinaendelea kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua kwa haraka.