Licha ya uongozi wa Manchester United ya England, kukana kuzungumza lolote kuhusu kinachoendelea kati yao na Kocha Jose Mourinho, taarifa za uhakika zinasema pande zote mbili, zimekuwa na mazungumzo mazito.
Mourinho ni kocha mzoefu, mwenye maneno ya karaha na kejeli kwa wapinzani wake, lakini mhamasishaji wa mashabiki na wachezaji kwa timu zote alizopata kuzinoa ikiwamo Chelsea, kwa sasa ananukia kuinoa United au Mashetani Wekundu wa England.
Mbali ya Chelsea iliyomfuta kazi Desemba, mwaka jana, kocha huyo ana rekodi nzuri ya kuzifundisha timu nyingine kwa mafanikio ambazo ni FC Porto ya Ureno, AC Milan ya Italia na Real Madrid ya Hispania.
Habari za kuaminika zinasema, wakala wake amemekuwa na mazungumzo na United huku Mourinho akitajwa kuwa mmoja wa makocha wanaowania kazi katika timu ya Manchester United ambayo inatapatapa chini ya Lous van Gaal.
Van Gaal ameripotiwa kutaka kuondoka baadaye mwakani, hivyo hatua hiyo itampa fursa Mourinho ambaye anadaiwa kufurahia mpango huo wa kuinoa Manchester United.
Maofisa wa juu wa United wanatarajiwa kutoa jibu baada ya majirani zao Manchester City kuchukua huduma za Pep Guradiola ambaye pia anatarajiwa kuanza kazi Mei, mwaka huu.
Kuwasili kwa Mourinho kunamaanisha kwamba upinzani mkali utaanza kati ya City na United kama ule uliokuwepo kati ya Real Madrid na Barcelona wakati makocha hao walipokuwa katika timu hizo mbili.
Katika kipindi cha wiki mbili, kazi ya Van Gaal imekuwa ikiyumbayumba hasa baada ya timu hiyo kushindwa katika michezo kadhaa ya Ligi Kuu ya England.