Kutoka kuuza kahawa Kariakoo hadi chapuo la kuwa mbunge (2)

TABORA, NA MOSHY KIYUNGI
 
Wiki iliyopita tuliona jinsi mwanamuziki Harmonize alivyoanza kushirikiana na wanamuziki wengine wakubwa kama Fally Ipupa katika kazi zake. Hilo lilianza kumpa umaarufu ambao aliendelea nao.
Wakati fulani alitamba na kibao kiitwacho Never Give Up, wimbo ambao unaelezea historia ya maisha yake kuanzia alivyokuwa na maisha magumu sana. Harmonize anasimamiwa na Joel Joseph au kwa jina jingine Mr Puaz.
 
Maisha ya awali
 
Harmonize alisoma katika Shule ya Sekondari Mkundi iliyopo mjini Mtwara, baada ya kumaliza elimu yake alikwenda jijini Dar es Salaam ambako alijishughulisha na shughuli mbalimbali za kumpatia riziki ya kila siku.
Kama wafanyavyo vijana wengi wasio na mtaji waingiapo jijini Dar es Salaam, Harmonize naye alipitia katika shughuli mbalimbali kuhakikisha kuwa anapata fedha kwa ajili ya kumudu gharama za kuishi mjini.
Baadhi ya kazi alizozifanya ni pamoja na kusukuma mkokoteni wa maji, kuuza kahawa kwa wafanyabiashara wengine na wakazi wa Kariakoo jijini humo.
Alianza kujihusisha na muziki mwaka 2011, ambapo alitoa nyimbo mbalimbali lakini hazikuweza kupata umaarufu mkubwa, hadi alipokutana na Diamond Platnumz mwaka 2015 na kuanza kufanya muziki pamoja naye chini ya lebo ya WCB.
Wakati anaanza kazi ya muziki, Harmonize alitamani kushiriki onyesho la Fiesta Mtwara, lakini hakuweza kupata fursa ya ku-perfom.
Alieleza kisa cha kuto ku-perfom ni kwamba wakati akiwa njiani kwenda kuangalia wasanii wenzake waki-perfom kwenye viwanja vya Nangwanda Sijaona, alikutana na kundi la vibaka wakamkaba na kumpora kila kitu.
Mwanamuziki huyo alisema baada ya tukio hilo aliamua kurudi hotelini akiwa amechanganyikiwa kutokana na kuporwa kila kitu, ikiwa ni pamoja na nauli yake ya kurudi Dar es Salaam.
Harmonize alisema baada ya kufikiria sana aliamua kuchukua nguo zake zilizokuwa hotelini, akaamua kuziuza ili aweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam.
Akiwa mjini Mtwara alipatiwa namba ya simu ya Diamond Platumz na mmoja wa watangazaji mjini humo ili akirejea Dar es Salaam amtafute ili aweze kumsaidia kimuziki.
Harmonize alisema hakuamini siku alipomtumia ujumbe Diamond na kujibiwa naye kuwa amekubali kumsaidia pamoja na kumpatia malazi nyumbani kwa Diamond huko Tegeta jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuingia WCB, Harmonize akatokea kuwa mtu wa karibu sana na bosi wake Diamond, hadi kutuhumiwa kumuiga kwa kila kitu, kuanzia kuongea, kucheka, kuimba, kucheza na pozi mbalimbali.
Lakini yeye alitumia muda mwingi kujitetea kwamba hamuigi kwa kila kitu kama wanavyodai watu, lakini alikubali kuwa alikuwa akimkubali sana Diamond Platnumz huku akimuita Bigi.
Kwa sasa Harmonize amejiengua katika lebo hiyo kutokana na sababu ambazo hazijawekwa wazi. Lakini baada ya kuvunja mkataba na Wasafi Classic Baby (WCB), Harmonize alitakiwa kulipa Sh milioni 500 ili kupata haki zake zote kutoka katika mikono ya Wasafi.
Kwa mujibu wa Harmonize, masharti ya kuvunja mkataba yapo katika makundi mawili. La kwanza, ni kulipa Sh milioni 500. Pili, kama ataondoka kama yeye, asitumie jina la Harmonize pamoja na nyimbo ambazo msanii huyo alirekodi akiwa WCB.

 
Itaendelea