Na Alex Kazenga, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Harambee iliyoendeshwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hassan Mwinyi katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) 2023, imeonyesha mwanga wa mipango ya serikali kwenye sekta ya kilimo kufanikiwa ifikapo 2030.
Moja ya mipango hiyo ni kuhakikisha mpaka inafika mwaka huo serikali iwe na jumla ya ekari milioni 8.8 za umwagiliaji zitakazowezesha uzalishaji mkubwa wa chakula kwa Watanzania na barani Afrika.
Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe wakati akimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye meza ya majadiliano baina yake na marais wanne waliohudhuria mkutano huo; Rais William Ruto wa Kenya, Rais Macky Sall wa Senegal, Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi na Rais Mwinyi wa Zanzibar, ameweka wazi kuwa wadau wa kilimo duani wameahidi kuisaidia Tanzania kwenye kilimo.
Waziri Bashe amesema kutokana na Jukwaa la AGRF kulenga kuwainua vijana, Mradi wa serikali wa Build a Better Tomorrow (BBT), ‘Jenga Kesho iliyobora’ umeonyesha nia hiyo kufikiwa mapema.
Mradi huo unaowalenga hasa vijana na wanawake, wakati wa harambee umeahidiwa kuchangiwa na taifa la Marekani pamoja na Ethiopia.
Wadau wengine walioahidi kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo ni Ofisi ya Rais wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRA), Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Sambamba na mpango huo, Waziri Bashe amesema Serikali inalenga kuchimba visima 67,500 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kumpatia kila mkulima ekari 2.5 pamoja na tenki la lita 5000 kuufanikisha.
“Kilimo kinahitaji fedha na uwekezaji wa kumusaidia mkulima mdogo ama mkubwa, kupitia mkutano wa AGRF-2023 serikali imeweza kupata fedha ambazo itaziwekeza kwenye kilimo kukamilisha mipango ya muda mrefu,” amesema Bashe.
Wakati akieleza changamoto zizoikabili sekta ya kilimo waziri Bashe amesema mojawapo ni kushindwa kufanya kilimo chenye tija na kubainisha kuwa changamoto hiyo itatuliwa kwa kumuwezesha mkulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa za kufanya kilimo.
Kutokana na jitihada za serikali katika kuinua sekta ya kilimo, mwaka jana tu amesema kulikuwa na ekari 720,000 za umwagiliaji na ndani ya mwaka mmoja wa fedha zimeongezeka nyingine zaidi ya 95,000.
Anabainisha mpango wa muda mfupi uliopo kuwa ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 Tanzania itafikia kuwa na ekari za umwagiliaji milioni 1.2.
Akizungumza wakati wa harambee, Rais Dk. Mwinyi, amesema kumekuwapo na utashi wa kisiasa unaokua kwa kasi nchini na barani Afrka kwa ujumla.
Utashi huo amesema umetokana na juhudi mbalimbali zikiwamo kupitishwa kwa mikataba ya tamko la mpango wa utekelezaji wa vijana, kuanzishwa kwa dawati la vijana katika mpango mpya wa ushirikiano wa pamoja na uwezeshaji wa vijana na wanawake katika Mradi wa BBT.
Uwepo wa kukua kwa mifumo ya kidigital inayosimamia mabadiliko ya uchumi wa dunia Rais Dk. Mwinyi amesema vimeongeza kasi kwa vijana kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi kupitia kilimo barani Afrika.
“Vijana wanayo hamu ya kuwekeza sehemu zenye matokeo chanya. Changamoto iliyopo bado tuna uzalishaji mdogo wa raslimali za uzalishaji, ujuzi na ukosefu wa mitaji,” amesema Dk. Mwinyi.