Jana Desemba 6, 2021 ilitimia miaka 10 tangu toleo la kwanza la Gazeti la JAMHURI lilipoingia kwenye orodha ya magazeti yanayochapishwa, kusambazwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi yetu.

Desemba 6, 2011 inabaki kuwa siku muhimu kwetu waanzilishi wa JAMHURI kwa sababu inabeba historia ya uamuzi mgumu uliochukuliwa na waasisi wawili – Deodatus Balile na Manyerere Jackton.

Umri wa miaka 10 si haba. Ni umri unaoweza kuandikiwa historia ndefu ya safari iliyopitia milima, mabonde, furaha na wakati mwingine huzuni.

Miaka 10 iliyopita, kwenye safu hii, tuliahidi kufanya kazi ya uandishi wa habari tukilenga zaidi kuwa sauti ya wasio na sauti, watetezi wa rasilimali za nchi, wadau muhimu katika kulinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Hayo na mengine tumejitahidi kwa uwezo wetu kuyatekeleza. Wasomaji wetu ni mashahidi wa namna JAMHURI lilivyosimama imara kwa miaka yote 10 kutetea yale linayoamini yana manufaa kwa jamii na kwa taifa letu.

Wasomaji wanakumbuka namna JAMHURI lilivyosimama imara kuwa Gazeti la Kiswahili la habari za uchunguzi lisilofungamana na upande wowote. 

Watakumbuka mchango wa JAMHURI kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya matapeli wa madini, mapambano dhidi ya majangili, wizi na utoroshaji wa tanzanite na madini mengine, na namna JAMHURI lilivyosimama imara kuibua ufisadi wa kutisha bandarini na katika biashara ya mafuta ya petroli na mafuta ya kula. Orodha ni ndefu sana.

Kwa miaka 10 tumeendelea kuwa sehemu muhuimu ya watetezi wa mazingira na rasilimali wanyamapori tukiwa tunaandika habari za ufisadi na mitandao inayohujumu rasilimali za nchi yetu.

Safari ya miaka 10 isingewezekana bila ushirika mkubwa wa wapendwa wasomaji na watangazaji wetu. Hata tulipopita katika wakati mgumu kiuchumi, hamkutuacha tufe. 

Mmesimama imara kuhakikisha hatukosi hata Jumanne moja – kwa miaka yote 10 – kuwa sokoni. Asanteni sana.

Tunawashukuru wote wenye mapenzi mema, vikiwamo vyanzo vyetu vya habari ambavyo kwa namna ya pekee vimeendelea kutuamini na kutupatia habari nyeti ambazo kwa kuziandika au kwa kuzifikisha kwenye mamlaka za dola, zimesaidia sana kuleta mabadiliko chanya. Tunawaahidi kuendelea kuwa wasiri na watiifu kwa wote walio tayari kushirikiana nasi katika kuijenga nchi yetu kupitia sekta ya habari za uchunguzi. Endeleeni kutuletea taarifa bila woga.

Tunawapongeza wafanyakazi wa JAMHURI ambao licha ya vitisho na kukatishana tamaa kunakotokana na aina ya habari tunazochapisha, wameendelea kusimama imara.

Tumetimiza miaka 10. Safari bado ni ndefu. Tunaomba wadau wote muendelee kutuunga mkono ili hatimaye dhamira yetu ya JAMHURI kuwa gazeti mahiri Tanzania na katika ulimwengu wote wa Kiswahili, itimie. Daima sisi “Tutaanzia Wanapoishia Wenzetu.”

Mungu Ibariki JAMHURI, Mungu wabariki wasomaji na watangazaji wetu, Mungu Ibariki Tanzania. Asanteni sana.