Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
KATIBU Mkuu Jumuiya ya Wazazi Taifa(MNEC) Ally Hapi ,ametoa rai kwa Chama na Jumuiya kujenga umoja ili kukiimarisha chama wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu ,lengo likiwa kushika dola.
Aidha ameitaka Jumuiya ya wazazi kujijenga na kujipanga vizuri kwani ni Jumuiya kongwe zaidi ili iweze kuwa na mvuto na kuleta mchango mkubwa katika chaguzi zinazokuja.
Vilevile Hapi ameiasa Jumuiya ya wazazi kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kushuka chini,ifanye kazi na kufanya ziara kwani huu sio wakati wa kukaa maofisini wala kusimang’ana.
Akitoa rai kwa wanachama wa Jumuiya na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani, katika mapokezi ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Pwani, kwenye viwanja vya ofisi ya CCM Mkoani humo, alisema siri ya mafanikio ya chama ni kupata ushindi utakaotokana na umoja uliopo.
Alisisitiza Chama kwanza mtu baadae na kuwaomba kutanguliza maslahi ya chama na sio mtu.
“Umoja kuelekea kwenye uchaguzi lengo ni kushika dola, umoja wetu sio wa vikoba au vikao vya harusi, tusonge mbele na kushikamana kwa ajili ya ushindi wa kishindo na inawezekana”alieleza Hapi.
Alihimiza mtaji wa wanachama na kupongeza Jumuiya ya wazazi kupiga hatua kwasasa kwa kufikia uandikishaji wanachama kieletroniki milioni 2.2 ikifuatiwa na Umoja wa wanawake UWT milioni 1.5 na UVCCM milioni 1.2.
Kadhalika aliwataka wenye uwezo na sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chaguzi zijazo.
Pamoja na hayo Hapi, aliwaasa wanaCCM kusema mazuri yanayofanywa na serikali na utekelezaji mkubwa wa ilani ya CCM badala ya kutumia majukwaa kujisifia na kufanya mbwembwe.
“Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa amefanya makubwa nchini ikiwemo kujenga madarasa 21,000 ,mabweni ya wasichana, kujenga majengo ya dharura, hospital za wilaya, kusogeza huduma za kijamii na kuboresha miundombinu mbalimbali na kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwa ni sanjali na SGR na bwawa na umeme Rufiji ambalo limefikia asilimia 99.99″anasema Hapi.
Akizungumzia suala la mchakato wa kuchuja wagombea amevitaka vikao lengwa kupeleka wagombea wanaokubalika,wasiwe wa kuumiza na kukipa chama mzigo.
Hapi alikemea vurugu za wapambe nuksi zisiumize chama na viongozi ambao bado wapo madarakani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alieleza anajivunia mahusiano mazuri yaliyopo baina ya chama na serikali mkoa.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka tilioni 1.3 katika miradi ya maendeleo Mkoani Pwani katika kipindi cha miaka mitatu.
Kunenge aliahidi yale ambayo chama inataka kuona kwa serikali mkoa wataona kwa vitendo.
Mkuu huyo wa mkoa alimhakikishia Rais wakati wa uchaguzi Mkuu ujao ni mitano tena,ushindi wa kishindo kwani mengi amefanya Mkoani Pwani .