Qatar leo inatarajiwa kufanya mazishi ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, baada ya mauaji yake huko Tehran, katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel, jambo lililosababisha hatari ya kuenea kwa machafuko.

Haniyeh atazikwa katika maziara ya Lusail, kaskazini mwa Doha baada ya sala itakayofanywa katika msikiti mkubwa nchini Qatar wa Imam Muhammad bin Abdul Wahhab.

Hamas imesema kwamba viongozi wa Kiarabu na Kiislamu, pamoja na wawakilishi wa makundi mengine ya Palestina na raia, watahudhuria mazishi hayo. Kuuwawa kwa Haniyeh kulifanyika masaa machache tu baada ya Israel kufanya shambulizi kusini mwa Beirut na kumuua Fuad Shukr, kamanda wa kijeshi wa kundi la Hezbollah lililo na mafungamano na Hamas.