Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Hanang
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang iliyopo mkoani Manyara imedhamiria kuwekeza kwenye Madini ya Ujenzi hususan kokoto ili kuongeza vyanzo vingine vya mapato.
Hayo yamebainishwa leo Julai 04, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Teresa Irafay baada ya kutembelea banda la Wizara ya Madini katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, maeneo mengi yaliyopo ndani ya Halmashauri hiyo yana miamba inayotumika kama kokoto ambayo wananchi wengi wamekuwa wakijishughulisha na uchimbaji wa kokoto lakini Halmashauri imeona hiyo kama fursa ya kuwekeza ili kuongeza vvyanzo vingine vya mapato.
“Halmashauri yetu hivi sasa tunategemea shughuli za kilimo, ufugaji, utalii, misitu kwa asilimia kubwa, ila tunataka tuanze kuwekeza katika madini ujenzi ambayo tunayo kwa wingi sana katika maeneo yetu” amesema Irafay.
Kwa upande wake, Mhandisi Migodi kutoka Wizara ya Madini Neema Mwafumbila amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, Halmashauri hiyo inapaswa kuomba Leseni kwa ajili ya kuchimba Madini hayo ya Ujenzi na baada ya kupata leseni hiyo Halmashauri itakuwa na uwezo wa kuiuza kwa Mwekezaji kama chanzo cha mapato.
Amesema kuwa shughuli zote za uchimbaji wa madini kwa uhalali zinahitaji leseni kutoka Tume ya Madini kwa kufuata utaratibu maalum uliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini.