Kundi la Hamas laanza mchakato wa kumchagua kiongozi mpya baada ya Yahya Sinwar kufariki kwenye shambulio la Israel

Maafisa wawili wa Hamas wamesema kwamba majadiliano ya kumchagua mrithi wa kiongozi wa kundi hilo Yahya Sinwar, ambaye mauaji yake yalithibitishwa siku ya Alhamisi wiki jana, yataanza hivi karibuni.

Maafisa hao walisema Khalil al-Hayya, naibu wa Sinwar na afisa mkuu wa kundi hilo nje ya Gaza, anazingatiwa kuwa mgombea aliye mstari wa mbele kuichukua nafasi hiyo. Al-Hayya mwenye makazi yake nchini Qatar kwa sasa anaongoza ujumbe wa Hamas katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya kundi hilo na Israel, na ana ujuzi wa kina, uhusiano na uelewa wa hali ya Gaza.

Viongozi wa Hamas watakutana kwa mara nyingine tena kumchagua mrithi wa Sinwar, ambaye alikuwa mtu anayesakwa sana na Israel, miezi miwili tu baada ya kuuawa kwa kiongozi wa zamani Ismail Haniyeh mjini Tehran. Afisa mkuu wa Hamas alimuelezea Sinwar kama mpangaji wa mashambulizi ya Oktoba 7, akisisitiza kwamba uteuzi wake ulikusudiwa kama ujumbe wa kijasiri wa ukaidi dhidi ya Israel.

Tangu Julai, mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekwama, na wengi wanaamini kuwa uongozi wa Sinwar ulikuwa kikwazo kikubwa kwa mpango wowote wa kusitisha mapigano.

Licha ya kuuawa kwa Sinwar, afisa mkuu wa Hamas alikariri kwamba masharti ya vuguvugu hilo ya kukubali kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Israel hayajabadilika.

Hamas inaendelea kuitaka Israel iondoke kabisa Gaza, kukomeshwa kwa uhasama, uhamishaji wa misaada ya kibinadamu, na ujenzi wa eneo hilo – masharti ambayo Israel imeyakataa kabisa, ikisisitiza kuwa Hamas lazima ijisalimishe.

Walipoulizwa kuhusu wito wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa Hamas kuweka chini silaha zake na kujisalimisha, maafisa wa vuguvugu hilo walijibu: “Haiwezekani sisi kujisalimisha.

“Tunapigania uhuru wa watu wetu, na hatutakubali kujisalimisha. Tutapigana hadi risasi ya mwisho na askari wa mwisho, kama vile Sinwar alivyofanya.”

Kuuawa kwa Sinwar ilikuwa moja ya pigo kubwa zaidi kwakundi hilo katika miongo kadhaa. Hata hivyo, licha ya changamoto za kuiziba nafasi yake, Hamas ina historia ya kuvumilia mapigo ya uongozi tangu miaka ya 1990.

Wakati Israel imefanikiwa kuwaua viongozi na waanzilishi wengi wa Hamas, vuguvugu hilo limethibitisha kuwa na uthabiti katika uwezo wake wa kutafuta wapya.

Katikati ya mgogoro huu, maswali yanasalia kuhusiana na hatma ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza na nani atawajibikia usalama na ulinzi wao.

Katika muktadha huu, Mohammed Sinwar, kakake Yahya Sinwar, amejitokeza kama mtu muhimu. Anaaminika kuwa anaongoza makundi yaliyosalia yenye silaha ya Hamas na huenda akawa na jukumu muhimu katika kuunda mustakabali wa harakati hiyo huko Gaza.

Wakati Hamas inapitia wakati huu muhimu, vita huko Gaza vinaendelea.

Makumi ya watu waliuawa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza siku ya Jumamosi wakati wanajeshi wa Israel walipozidisha mashambulizi dhidi ya kile Israel inachosema ni majaribio ya Hamas kujipanga upya.