Zaidi ya wakazi 1,100 kutoka wilayani Mkuranga mkoani Pwani wameruhusiwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuishitaki Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga iliyogawa ekari 750 za ardhi yao kwa mwekezaji.
Wakiwakilishwa na wenzao saba, wananchi hao 1,119 walikwenda mahakamani kudai haki yao baada ya uongozi wa Halmashauri ya Mkuranga kuwaondoa katika maeneo yao na kuligawa eneo hilo kwa Kampuni ya Soap and Allied Industries inayomilikiwa na Hamidu Bharmal, ambaye hata hivyo hajawekeza chochote katika eneo hilo.
Wananchi hao kutoka vijiji vya Lugwadu na Magodani wamepata ushindi huo kupitia hukumu iliyotolewa Novemba 8, mwaka huu baada ya Mahakama Kuu kuyatupilia mbali mapingamizi matano yaliyowekwa na wakili wa Halmashauri ya Mkuranga.
Wakiwawakilisha wenzao 1,119, Abdallah Ndogondogo, Omari Madanganya, Kassim Mkumba, Mariam Wimbe, Ubaya Mnyimadi, Somoe Bakari na Juma Nguta walifungua kesi iliyopewa namba 764 ya mwaka 2018, dhidi ya halmashauri hiyo wakipinga kuuzwa kwa eneo hilo ambalo vijiji vyao vimekuwa vikilimiliki kwa miaka mingi. Wamesema kuwa baada ya kupata ushindi katika hatua yao ya kutafuta haki yao, sasa wanapanga kuiandikia barua Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ili kuitaarifu azima yao ya kuifungulia kesi mahakamani, kama ambavyo sheria inataka.
Katika ushahidi wao mahakamani, wanakijiji hao wamesema walishangazwa na hatua ya halmashauri kuuza eneo la vijiji vyao kwa sababu awali halmashauri hiyo ilikubaliana na Kijiji cha Kazole Vikindu kumuuzia mwekezaji ekari 1,000 katika shamba namba 271. Wameeleza kuwa kwa kutumia njia zisizo halali, uongozi wa halmashauri kwa kuhusisha watendaji wa serikali wasio waaminifu, walimuongezea mwekezaji huyo eneo la ekari 750 za shamba hilo zinazomilikiwa na serikali ya Lugwadu na Magodani.
Wameieleza mahakama kuwa tangu amilikishwe shamba hilo mwaka 1988, mwekezaji huyo hakuwahi kuliendeleza ingawa hati ya umiliki wake namba 34681 inaonyesha kwamba atalitumia eneo hilo kwa kilimo na ufugaji.
Akizungumza na JAMHURI baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mmoja wa wakazi wa Lugwadu na Magodani, Lugano Mwamakamba, amesema inashangaza kuwa halmashauri sasa imepima viwanja katika eneo hilo na kusema kuwa wananchi hao ndio watakuwa wanufaika wa awali.
Amesema kuwa baada ya kukabidhiwa eno hilo, mwekezaji huyo alivunja nyumba za watu waliokuwa wakiishi hapo kwa usimammizi wa halmashauri.
Amesema kabla ya kwenda mahakamani walihangaika sana kutafuta haki yao hadi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ambaye awali alionyesha nia ya kuwasaidia lakini baadaye akawageuka na kuwa upande wa mwekezaji.
“Sisi tunataka halmashauri kwanza iturudishie ekari zetu 750. Suala la wao kupima viwanja katika eneo hili eti na sisi wananchi tuanze kunufaika tunaona kama ni mchezo unaotengenezwa makusudi. Tunaiomba serikali imnyang’anye hili shamba huyu mwekezaji kwa sababu eneo limegeuka kuwa pori tu ingawa linalindwa kwa mitutu bila shughuli ya kimaendeleo inayofanyika,” amesema Mwamakamba.
Wakazi hao wamesema suala hilo limesababisha hofu miongoni mwao, kwani baadhi yao wameshawahi kubambikiwa kesi na kufungwa kwa njama za mwekezaji huyo.
Kila mara walipojaribu kutafuta haki yao walishindwa kwani hata uongozi wa mkoa ulionekana kuwa pamoja na mwekezaji huyo.
“Sisi hili jambo la kupigania ardhi yetu tunalifanya kwa woga kweli kweli, ila tumejitoa kweli kweli, maana tunayepambana naye ana nguvu kubwa. Amewanunua viongozi wote waliokuwa na lengo la kutusaidia tumebaki sisi kama yatima ila tumeamua liwalo na liwe, lazima haki yetu ipatikane,” amesema mkazi mwingine, Kassim Mkumba.