Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Kibaha

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Vijijini imeazimia kumpa kazi Mkuu mpya wa Wilaya ya Kibaha Nickson John kutatua tatizo la wakulima wa zao la korosho wa kata ya Kikongo ambao wanadai kutolipwa kiasi cha sh.milioni 76 kwa kipindi cha miaka miaka minne sasa.

Aidha Halmashauri Hiyo imeazimia Wizara ya Maliasili kuvuna mamba walioko Mto Ruvu ambao wamekuwa wengi wakiongezeka siku hadi siku na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo kwa wananchi.

Akitaja maazimio ya kikao Cha Halmashauri Kuu hiyo, Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu Kanusu alieleza, haiwezekani suala hilo kuchukua muda mrefu,huku wakulima walishatoa korosho zao kwa mnunuzi aliyetajwa kwa jina moja la Adamu ambae alinunua korosho kupitia chama chao cha msingi.

“Suala hili tutalipeleka kwa Mkuu wa wilaya mpya japo bado ni mgeni akitokea Wilaya ya Kisarawe alishughulikie suala hili ili wakulima wapate stahiki zao,”amesema

Amesema kuwa suala hilo licha ya kupelekwa maeneo mbalimbali ili lishughulikiwe lakini hadi leo ufumbuzi hakuna wanataka suala hili liishe .

“Tutahitaji tupate mikataba ya mauziano ya korosho kwani zilishauzwa na uzuri wahusika wapo kwanini kuwe na ugumu ili hali korosho zilishauzwa,”amesema Kanusu.

Kwa upande wake ofisa ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Flora Wayalla amekiri kuwepo kwa deni hilo,wamejitahidi ila malipo yamekuwa ni shida licha ya kulipeleka Mkoani Lakini lilirudishwa ili Mkuu wa Wilaya alishughulikie.

Wayalla alielezea, maamuzi ya kikao hicho yatasaidia kulishughulikia suala hilo ambalo limekuwa changamoto kubwa na endapo watalipeleka suala hilo mahakamani wakulima hawatakuwa na uwezo na litachukua muda mrefu zaidi.

Awali moja ya viongozi wa CCM Kata ya Kikongo Hija Matitu amesema kuwa hiyo imekuwa kero kubwa kwa wakulima ambao walitoa korosho zao ili ziuzwe na baadaye walipwe fedha zao.

Matitu alitaka,chama kichukue hatua kwani mhusika yupo huku korosho alizichukua na alishauza huko Mtwara hivyo wao watalipeleka suala hilo mbele endapo Wilaya itashindwa kuwasaidia.

Katika hatua nyingine Juma Kahonga amesema mamba wamekuwa ni wengi sana hivyo ni vema wakavuliwa ili kupunguza athari zinazosababishwa na wanyama hao hatari.

Mwenyekiti huyo wa CCM Kanusu amesema jambo hilo no kero kwani mamba hawajavunwa muda mrefu.