Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
HALMASHAURI Kuu ya CCM, Wilaya ya Bagamoyo,Mkoani Pwani ,imeelekeza viongozi wa chama kuanzia Matawi hadi kata waongeze nguvu katika kusimamia miradi na utekelezaji wa ilani kwenye maeneo yao.
Aidha imewataka wanaCCM kuisemea Serikali kwa makubwa yanayofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake ameitendea haki ilani kwa kufanya makubwa wilaya ya Bagamoyo.
Vilevile, Halmashauri Kuu hiyo ya chama wilaya ,imehimiza wanachama wake waende wakajipange,waungane ili kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye uchaguzi wa Serikali za vijiji, vitongoji na mitaa utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa madiwani ,wabunge na Rais 2025.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Bagamoyo,Alhaj Abdul Sharif Zahoro ,aliwaasa wanaCCM kwenda kukisema chama na kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Rais dkt. Samia.
Kadhalika ,aliwahimiza kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwani kila mmoja ana haki ya kugombea na kuwahakikishia kwamba uchaguzi utakuwa wa uhuru na haki .
“Hizi nafasi ni za kila mmoja mwenye sifa ,tukagombee ,na uchaguzi mkuu mwakani ukifikia mjitokeze kwenye udiwani, ubunge lakini tuu msigombee Urais ,maana kama wilaya tumejipanga ushindi wa kishindo kwa Rais Samia Suluhu Hassan”
“Iwe jua, iwe mvua Bagamoyo itampa kuraa za kishindo Rais kutokana na makubwa aliyoyafanya Bagamoyo na yanaonekana, kikubwa tusichoke kusema, tuendelee kukisemea chama kwa utekelezaji wa ilani “alisisitiza Sharif.
Hata hivyo ,Sharif alikemea ,tabia ya wale wachache wanaojipenyeza mapema kufanya kampeni na machawa kuanza kupitapita kuwachafua viongozi wa kuchaguliwa madiwani na wabunge kabla ya muda 2025.
“Muda bado ,tuwaache viongozi wetu wamalizie ngwe yao ya miaka mitano salama, tusiwachanganye ,muda ukifika kila mmoja anaetaka kugombea atajitokeza kugombea lakini sio sasa “alifafanua Sharif.
Awali mbunge viti maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu alisema Umoja ,Upendo, Mshikamano ndio silaha ya kukiimarisha chama.
“Tumejadili taarifa ya kazi 2022-2023 , uchaguzi 2024/2025 na tumetoa tamko la kumpongeza mh.Rais kwa kasi anayoendelea nayo kutatua kero za wananchi”
Mgalu alielezea, kazi kubwa inafanyika, kilichobakia tuongeze nguvu kukisemea chama,kila mmoja wetu aseme mema yanayofanyika badala ya kunyamaza kimya.
“Mimi ni shuhuda ,ndani ya miaka mitatu nimefanikiwa kuungana na Umoja wa wanawake Tanzania UWT Taifa kushiriki ziara walizozifanya 854 ,Mimi binafsi nimeshiriki ziara na mikutano ya hadhara 120 ikiwemo Tisa mkoani Pwani,Umoja huu umezunguka na kuisemea Serikali na utekelezaji wa ilani”
Mgalu alieleza,japo bado Kuna baadhi ya changamoto kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo kero ya kukatika kwa umeme ,maji ,migogoro ya mipaka ,ardhi nk, Serikali inazitatua hatua kwa hatua.
Mbunge huyo anasema ” Tunaposema mafanikio tunamshirikisha Rais Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ukisoma kuanzia ibara ya 33 utakuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Amiri Jeshi ,Kiongozi mkuu na mkuu wa Majeshi lakini ibara ya 34:;3 shughuli zote za Jamhuri na Tanzania Bara Rais atakuwa na mamlaka nazo” alisema Mgalu.
Mgalu aliongeza kuwa , hivyo kama wanamhusisha kwa kusemea changamoto zilizopo zaidi ,kusiwe na mjadala kwahiyo wapo akiwemo na yeye wanaendelea kusemea mafanikio yanayofanyika bila kuchoka .
“Kuna watu wakiona tunasemea chama, Serikali ,tunamsemea Rais anayofanya wanaenda mbali kusema watu wanasema ili wapate vyeo ,niwaambie vyeo vipo na tayari wapo ambao wanafanya kazi na isihusishwe kuisemea Serikali ni kutaka vyeo,tuingie kazini tufanye kazi ,tuache kukatishana tamaa.”;alieleza Mgalu.