Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO),limezitaka halmashauri nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko badala ya kutegemea Serikali Kuu pekee.
Hatua hiyo itarahisisha jamii kukabiliana na milipuko hiyo kwa haraka zaidi,lengo likiwa ni kunusuru nguvu kazi ya taifa ambayo isipolindwa kuna hatari kubwa ya kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya Uelimishaji, Uhamasishaji na Ushirikishaji Jamii (RCCE), Wilaya ya Chato mkoani Geita, Ofisa progaramu Wizara ya Afya Idara ya Kinga na Elimu kwa Umma, Magdalena Dinawi, amesema Serikali Kuu haiwezi kuwafikia wananchi wote kwa haraka panapotokea majanga ya magonjwa ya milipuko na kwamba ipo haja kubwa kwa halmashauri kusaidia jukumu hilo kwa kusaidiana na wadau mbalimbali wa maemdeleo.
“Wilaya ya Chato ni miongoni mwa wilaya zilizo karibu sana na nchi jirani za Uganda,Burundi na Rwanda na mwingiliano wa watu wetu ni mkubwa sana…ndiyo maana Wizara ya afya tukaona ipo haja kwa mkoa wa Geita kuwajengea uwezo ili wasaidie kuifikia jamii iliyoko chini kuwaelimisha namna ya kuepukana na magonjwa ya milipuko”.
Kadhalika amesema Wilaya ya Chato inayo makundi mengi yenye mikusanyiko wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini,wavuvi wa samaki,Magulio,wanafunzi,waumini wa madhehebu mbalimbali,waganga wa jadi pamoja na wasafiri na wasafirishaji abiria.
“Tunaamini tukielimisha wachache nao wataenda kuelimisha wengine wengi zaidi, lengo letu kubwa likiwa ni kuhakikisha wananchi wanaelimika kwa kuzingatia taratibu na kanuni zinazopaswa kufuatwa na kila mmoja wetu” amesema Dinawi.
Ofisa elimu afya kwa Umma na Afya ya akili kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Jerry Mlembwa ,amesema moja ya malengo muhimu ya shirika hilo ni kuhakikisha usalama wa jamii na kwamba bila ya jamii kuwa na afya bora itakuwa ni ndoto kufikia malengo mengine.
Kutokana na hali hiyo,ameisisitiza jamii kuungana kwa pamoja kukabiliana na magonjwa ya milipuko kabla na baada ya kutokea kwa kubadili mitindo ya maisha ikiwemo kusalimiana kwa kushikana mikono, kusogeleana karibu zaidi na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
“Niwashauri ajenda ya magonjwa ya mlipuko inapaswa kupewa kipaumbele kwa kila vikao vyenu kwenye halmashauri…ni muhimu pia kuwashirikisha wadau wenu wa maendeleo katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko…sisi kama WHO tupo tayali kuzisaidia nchi wananchama ikiwemo tanzania kwenye magonjwa hayo” amesema Mlembwa.
Kwa mujibu wa Mganga mkuu wa Wilaya ya Chato,Dk.Eugen Rutaisire,wilaya hiyo imejipanga vyema kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kutokana na taarifa za kutokea kwa baadhi ya wagonjwa wa “Marburg” kwenye mkoa wa Kagera ambao upo jirani zaidi na wilaya ya Chato.
Mbali na kuipongeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na WHO kufika haraka wilayani humo kuimalisha kamati za majanga na dharula ili kuwa na uelewa wa pamoja na jamii,amesema elimu hiyo itawafikia wananchi walioko kwenye jamii ya chini zaidi ili watambue thamani ya kujilinda.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala wilayani hapa, Pumuka Masanja,amewataka waganga wa jadi kujiepusha na kung’ang’ania wagonjwa ambao watagundua kuwa magonjwa yao huenda yanatokana na milipuko ili kunusuru maisha ya wagonjwa na familia zao, badala yake wawaelekeze haraka kwenda Zahanati,Vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya matibabu sahihi.