Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, inatarajia kujenga jengo la Utawala lenye gharofa mbili, eneo la Ukuni kata ya Dunda, Jengo ambalo litagharimu kiasi cha sh.bilioni 6.2 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi huo utakuwa wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu bilioni 1.7.
Akielezea kuhusu ujenzi huo , wakati walipokwenda kuona eneo la ujenzi Mwenyekiti wa Halmashauri, madiwani na baadhi ya watendaji, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ,Shauri Selenda alieleza hadi sasa halmashauri imetenga milioni 911 na wamepokea bilioni 1 kwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tulikubaliana kuanza ujenzi huu, tukaamua kuanza kutenga mapato yetu ya ndani milioni 500 ambapo tutakuwa tunatenga milioni 500 kila mwaka ili kukamilisha jengo hili”
“Ilikuwa ni ndoto yangu,na ndoto ya wananchi wa Bagamoyo kupata jengo la halmashauri ambalo huduma zinapatikana kirahisi,ofisi zote zipo karibu na zinapatikana Kwa wakati”alifafanua Selenda.
Alieleza, hadi sasa mkataba umeshasainiwa na wameshamkabidhi mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi itakapofika Juni 15 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Mohammed Usinga alimshukuru, Mkurugenzi huyo na kusema ameandika historia na ataacha alama ya uongozi wake.
“Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, nitakuwa sitendi haki kama sitomshukuru na kumpa sifa Mkurugenzi wetu leo, ametuheshimisha, kiukweli amefanya jambo kubwa na la historia katika Halmashauri ya Bagamoyo “alisema Usinga.
Usinga aliiomba ,Taasisi Wezeshi ikiwemo Tanesco, RUWASA,TARURA, kusogeza huduma ya maji,umeme, miundombinu ya barabara ambazo zitakazohitajika kwa haraka.
Vilevile aliwataka wakandarasi wote , kuendelea na majukumu yao kama mikataba ilivyoelekeza kuanzia sasa ikiwa ni maazimio ya Baraza la Madiwani.