Tanzania inaonekana ni nchi ya amani na utulivu kwa wakati huu. Na huo umegeuka wimbo unaoimbwa na kila mmoja wetu lakini bila kuelewa vina vya wimbo huo vinapatikanaje.
Wimbo upo tangu miaka mingi iliyopita, unaimbwa kwa mbwembwe tu basi. Wengi wanaoimba wimbo huo hawajishughulishi kujua ulitungwaje na maudhui yake ni yapi.
Kwa wanaojishughulisha kuelewa maudhui ya wimbo huo, hawawezi kukubaliana na hali inayojitokeza kwa sasa, sababu wanaelewa kwamba wakati hali inayojitokeza kwa sasa ikikumbatiwa bila kujali madhara yake, wimbo huo unaweza kupotea mara moja. Na wimbo huo ukishapotea ndipo kila mmoja atakapojitahidi kujua maudhui yake.
Kwa wakati huu kuna jambo ambalo limewekwa mbele na watu wenye upeo mfupi katika mtazamo wa kisiasa na kijamii, jambo hilo ni demokrasia, kwamba watu waachiwe waendeshe mambo kwa namna wanavyotaka wao kwa vile hiyo ndiyo demokrasia. Jambo hilo ni hatari sana kwa mustakabali ya jamii yetu. Maana demokrasia bila mpangilio ni vurugu tupu, nitaeleza.
Katika kukieleza nilichokilenga nianze kwa mifano kadhaa katika kuonesha namna demokrasia ya aina hiyo ilivyo na madhara makubwa katika jamii.
Nianze na nchi ya Marekani. Hiyo ni nchi inayotamba sana duniani na kitu hicho demokrasia. Kutokana na Marekani kuwa na demokrasia ya kumtaka kila mwananchi afanye namna anavyotaka mwenyewe, nchi hiyo imekuwa na maafa makubwa ambayo hapa nchini kwetu yanazuilika kirahisi, pamoja na ukweli kwamba nchi ya Marekani inaizidi kwa mbali nchi yetu kiuwezo.
Tanzania, nchi maskini kiuchumi, inaonekana ni nchi tajiri sana katika kuilinda amani yake na kuufanya utulivu utamalaki kwa raia wake. Utajiri bila utulivu ni jambo lisilo na maana yoyote katika akili za kawaida.
Mfano hapa nchini, si rahisi mwananchi wa kawaida kwenda dukani na kununua silaha ya moto kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Mzunguko wa kuipata silaha ya aina hiyo ni mrefu mpaka mtu aweze kumiliki. Lakini kwa Marekani mtu anaweza kununua silaha ya moto sawa na mtu anayenunua peremende! Inadaiwa hiyo ni sehemu ya demokrasia!
Matokeo ya demokrasia ya aina hiyo tumeyashuhudia kila mara nchini Marekani, wakati fulani mtoto mmoja alichukua silaha ya moto na kuwafyatulia risasi wanafunzi wenzake na kuwaua kwa makumi. Taifa liliingia kwenye simanzi iliyosababishwa na demokrasia ya kumuacha kila mwananchi awe na uamuzi wake. Mambo ya aina hiyo yamekuwa ni ya kawaida nchini humo.
Hebu fikiria demokrasia inayosababisha mauaji ya wananchi ina umuhimu gani? Si ni bora kuikosa demokrasia lakini wananchi wakabaki na uhai wao? Kwa nini wananchi wateketee kisa eti ni demokrasia?
Kwa hiyo, tunaweza kuona kwamba amani na utulivu ni vitu vinavyoweza kutengenezwa au kusambaratishwa kulingana na jamii inavyojiendesha. Jamii ikitaka viwepo vinakuwapo na ikitaka vipotee basi vinapotea.
Mpaka hapo tunaweza kuona kwamba amani na utulivu tulio nao hapa nchini kwetu vinapatikana kwa juhudi zetu wenyewe, hali hiyo ni ghali mno kiasi kwamba baadhi ya mataifa, hata yale yaliyo na uwezo mkubwa kiuchumi, yanashindwa kuimudu. Ndiyo maana nikasema kwamba baadhi ya watu wanaoimba wimbo wa amani na utulivu hawaelewi wimbo huo ulitungwaje na una maudhui gani.
Kwa wakati huu hapa nchini kwetu kuna mambo yametokea hasa kwa upande wa Visiwani, hali ya kisiasa ni tete. Kule, Uchaguzi Mkuu wa 2015 umefutwa kutokana na hali iliyojionesha kuwa siyo salama na kutakiwa uchaguzi huo urudiwe tena kwa muda utakaopangwa baadaye. Lakini uamuzi huo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unalalamikiwa sana na baadhi ya watu wakiona kwamba ni uamuzi usiozingatia demokrasia!
Kusema ukweli hilo ni jambo la kusikitisha. Wanaosema hivyo ni kama hawaelewi ni kitu gani kilichosababisha ukawapo muungano wa Tanganyika na Zanzibar, muungano uliozingatia zaidi usalama wa eneo letu na kwa kiasi kikubwa ukiwa umetoa kisogo kwa demokrasia ya mashaka.
Sababu, kwa mtu anayeelewa namna Mapinduzi ya Zanzibar yalivyotokea na kuuondoa utawala wa kisultani uliokuwa hautambui utu wa watu wa asili wa visiwa hivyo, hawezi kutoa kipaumbele kwa demokrasia akiwa amesahau amani na utulivu vilivyopo visiwani mle kwa wakati huu.
Maana kilichosababisha Mapinduzi hayo yakafanyika kingeweza kujirudia kama visiwa hivyo vingebaki kama vilivyokuwa nje ya Muungano. Ikumbukwe kwamba aliyekuwa kinara wa Mapinduzi hayo, alikuwa mtu wa nje ya visiwa hivyo, John Okello, aliyekuwa raia wa Uganda. Ingawa kwa wakati huo alifanya kitu kilichopendwa na waliokuwa wengi, haieleweki kama asingetokea mtu mwingine wa aina hiyo na kufanya kitu cha aina ile ile kama Zanzibar ingebaki kama yenyewe nje ya Muungano.
Ikumbukwe kwamba visiwa vya Ngazija, ambavyo kimtazamo ni kama visiwa vya Zanzibar, vimechezewa sana na watu wenye nia mbaya na visiwa hivyo. Visiwa hivyo vimeshuhudia mapinduzi mengi kwa muda mfupi, yaliyokuwa yakiendeshwa na watu binafsi – mamluki.
Alikuwapo mtu mmoja mamluki aliyejulikana kama Bob Denard, mtu huyo tunaweza kumfananisha na John Okello. Aliyoyafanya mtu huyo, raia wa Ufaransa, hayakuwa na ridhaa ya Wangazija hata kidogo. Alikuwa akiyafanya kwa matakwa yake na maslahi yake binafsi kwa kuiweka rehani amani na utulivu wa watu wa Ngazija.
Lakini waliosumbuka ni Wangazija katika umoja wao. Sidhani kama kuna Mngazija mwenye akili timamu anayeweza kusema kwamba hayo yalikuwa mambo sahihi yaliyozingatia demokrasia kwa vile juu yake Bob Denard hakuwa na mtu wa kumshurutisha.
Kwa hiyo, wanaodai kwamba ZEC imefanya kufuru kuufuta uchaguzi ambao ulikuwa na dosari hawaeleweki lengo lao ni nini, sijui hawakijui kilichofanya Muungano ukawapo au ni wale wanaoupinga muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Na kuwaachia watu hao watimize matakwa yao tunawezaje kuendelea kuimba amani na utulivu? Amani na utulivu wanavyovitishia kuvibomoa, iwe kwa kutokujua au kwa kukusudia?
Nimalizie kwa kusema kwamba demokrasia ni kitu muhimu katika kila jamii, lakini inatakiwa demokrasia hiyo ichukuliwe kwa tahadhari kubwa bila kuiachia ikatikisa mhimili wa usalama wetu. Kwa maana ya kwamba demokrasia isiachiwe kusambaratisha amani na utulivu tulio nao. Tusiendelee kuuimba tu wimbo ambao hatujui vina vyake vikoje na vilitungwaje.
Mwisho kabisa niseme kwamba asiyekijua kifo akaitazame kaburi. Walio na demokrasia iliyopitiliza kila kukicha wako kwenye vilio, wanapata uchungu wa kujitakia. Demokrasia yenye heri ni lazima iwekewe mipaka. Mipaka yenyewe ni kama hiyo iliyowekwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).