Gaza sasa ikiwa imezingirwa kikamilifu na wanajeshi wa Israel na baada ya siku tano za mashambulizi ya mabomu, hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya.
Umeme ulikatika leo baada ya kituo pekee cha umeme katika eneo hilo kukosa mafuta. Hospitali, ambazo zimejaa maelfu ya majeruhi, zinasema zinakosa dawa.
Umoja wa Mataifa unasema watu nusu milioni wa Gaza hawajapata mgao wao wa chakula tangu Jumamosi. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuanzishwa eneo la kibinadamu. Afisa mmoja wa Misri aliiambia BBC kwamba serikali mjini Cairo ilikuwa katika majadiliano na pande zote kujaribu kuruhusu msaada kuingia Gaza kupitia Misri hata kama ni kwa saa chache tu.
Wakati huo huo, kuna matarajio makubwa kwamba Israel hivi karibuni itaimarisha zaidi operesheni yake kwa mashambulizi ya ardhini.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anatarajiwa kukutana na Mahmoud Abbas, rais wa Palestina.
Chama cha Abbas cha Fatah kinatawala Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, na ni tofauti na wanamgambo wa Kiislamu wa Hamas, ambao wanadhibiti Ukanda wa Gaza.
Hamas iliiondoa kwa nguvu Fatah katika uongozi wa Ukanda wa Gaza mwaka 2007.
Hamas ambacho ni chama cha kisiasa cha Kiislamu kilichoanzishwa mwaka 1987, kimetoa wito kwa muda mrefu kuangamizwa kwa Israel.
Vyama vyote viwili vya kisiasa ni vyombo tofauti, na mazungumzo ya umoja kati ya hizo mbili yamevunjika mara kwa mara.
Msemaji wa Israel alisema vikosi, ikiwa ni pamoja na askari wa akiba 300,000, walikuwa karibu na mpaka wakijitayarisha kwa kwa mashambulizi, ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na “mwisho wa vita hivi Hamas hawana tena uwezo wowote wa kijeshi”.
Kwa idadi ya watu waliouawa na Hamas mwishoni mwa juma ambayo sasa inajulikana kuwa zaidi ya 1,200, ujumbe huo utakuwa na uungwaji mkono mkubwa wa umma wa Israeli.