*Mwaka mmoja wa uvuvi haramu watikisa uchumi, watishia kuliua Ziwa Victoria
*Makokoro, nyavu hatari kutoka Uganda, Burundi vyaingizwa kwa fujo
*Kidole cha lawama chaelekezwa kwa viongozi wa serikali ngazi ya vijiji
*TAFIRI wakiri, watega nyavu kwa saa mbili ziwani na kuambulia samaki mmoja
Dar es Salaam
Na Alex Kazenga
Amini usiamini, samaki wanakwisha ndani ya Ziwa Victoria, hali inayotishia afya, uchumi na hata amani kwa mamilioni ya wananchi wanaolizunguka ziwa hilo; JAMHURI linaripoti.
Tishio hilo linatokana na uvuvi haramu ulioshamiri kwa takriban mwaka mmoja sasa, ukifanyika mchana na usiku bila hofu ya kuwapo kwa serikali.
Akizungumza na JAMHURI, mkazi mmoja wa Kanda ya Ziwa anasema: “Hali hii (uvuvi haramu bila hofu) imeanza tangu mwaka jana. Si hapa tu, ipo na inaonekana wazi katika wilaya za Muleba, Sengerema na Ukerewe.”
Ni aina hii ya uvuvi ndio unaozuiwa kisheria. Ndio umesababisha kuadimika kwa samaki wa kila aina ndani ya Ziwa Victoria.
Uvuvi ndio shughuli kubwa ya kiuchumi kwa Kanda ya Ziwa na kudorora kwake kunazua hofu kwa wengi.
JAMHURI linafahamu kwamba kwa takriban miezi mitatu sasa samaki maarufu aina ya sato na sangara wameadimika ziwani na kusababisha ugumu wa maisha kwa watu waliojiajiri au kuajiriwa katika sekta ya uvuvi.
Zana haramu, hatari
Mkazi wa Muleba mkoani Kagera aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema zana haramu kama makokoro, timba na malumalu zimeingizwa kwa wingi nchini kutoka Uganda na Uganda.
Malumalu ni nyavu za nailoni zinazotumika kuvulia dagaa ambazo haziozi hata zikikatika na kuzama majini, hivyo kuendelea kuua dagaa, samaki na viumbe wengine.
“Hizi ni nyavu hatari sana kwa kuwa hukamata hadi samaki wachanga wenye ukubwa wa inchi moja.
“Hali inazidi kuwa mbaya kila siku. Lazima serikali iingilie kati na kuchukua hatua za ziada kudhibiti matumizi ya zana haramu, la sivyo hata samaki wachache waliosalia nao watakwisha ndani ya Ziwa Victoria na kubaki maji matupu,” amesema mtoa taarifa huyo akionyesha hofu ya wazi hasa kwa namna uvuvi haramu unavyofanyika bila kificho.
Amedai kuwapo kwa dalili za mlungula unaotolewa na wavuvi wenye fedha kwa viongozi wenye jukumu la kulinda rasilimali ya taifa ili waruhusiwe kuvua maeneo ya mzalia ya samaki; akiwanyoshea kidole maofisa uvuvi na wenyeviti wa vijiji.
“Kuna tetesi za kuwapo baadhi ya viongozi wasioitakia mema serikali hii, wanaotengeneza mazingira yatakayosababisha wananchi kulaumu kwamba Serikali Kuu haifanyi kazi,” amesema.
Maeneo yaliyo hatarini
Maeneo yanayotajwa kuwa hatarini zaidi kwa uvuvi haramu ni visiwa vya Lwiza, Iramba, Bumbile, Kinagi, Rubili na Chakazimbwe vilivyopo Muleba mkoani Kagera.
Lakini pia mialo ya Chato, Sengerema na hata Magu inatajwa kuwa maeneo hatari kwa uvuvi haramu.
“Huko visiwani kila mwalo kuna kokoro. Kijiji cha Maria, Kisiwa cha Bumbile kina mialo zaidi ya 10 na kila mwalo una makokoro kati ya matatu na matano,” amesema mkazi mmoja wa Bumbile.
Makokoro hayo na nyavu nyingine haramu huvua kati ya kilo 200 hadi 600 za samaki wachanga wasiotakiwa sokoni kwa wakati mmoja.
Maeneo mengine yaliyokithiri kwa uvuvi haramu ni vijiji vya Kamanga na Kalumo wilayani Sengerema na visiwa vya Ukerewe.
Taarifa kutoka Kamanga zinaeleza kuwa wavuvi haramu hujenga ushirika wa kulindana na kulindiana siri.
Kama ilivyo Bumbile, Muleba, mzalendo mmoja mkazi wa Kamanga ameliambia JAMHURI kuwa wavuvi haramu maeneo ya Kamanga huwahonga maofisa wa serikali waliopo mialoni na kuendesha uvuvi haramu.
“Hapa Kamanga kuna maeneo hata mchana wavuvi wanavuta samaki kwa kokoro. Hawaogopi! Utadhani nchi sasa inaongozwa bila kufuata sheria.
“Wanavua hadi vifaranga vya samaki. Ukitoa taarifa, viongozi wala hawashtuki au kuonyesha dalili za kuchukua hatua! Ukizidi kiherehere unageuziwa kibao na kubambikiwa kesi,” amesema.
Matumizi ya betri za ‘solar’
Wakati teknolojia mpya duniani ikitumika kuboresha maisha, hali ni tofauti Kanda ya Ziwa ambako sasa wavuvi wa dagaa wanadaiwa kuchagiza kwisha kwa samaki.
“Siku hizi samaki na dagaa huvuliwa kwa wakati mmoja kutokana na matumizi ya taa zenye mwanga mkali kuanzia volti 18 hadi 20, sambamba na nyavu ngumu.
“Wavuvi wameacha kutumia karabai. Hizi betri za ‘solar’ zina mwanga mkali sana unaomulika hadi chini kabisa ya ziwa na kuwavutia pia samaki wa kawaida na kujikuta wakinaswa kwenye mitego ya dagaa,” anasema mmoja wa watoa habari wetu.
Hali hii inafanyika pamoja na kuwapo kwa sheria inayoelekeza wavuvi wa dagaa kutumia taa zenye volti tisa.
JAMHURI linaamini kuwa taarifa zinazotolewa kwa mamlaka za juu kuhusu hali ya uvuvi Ziwa Victoria si sahihi, kukiwamo vitisho kwa wasamaria wema wanaotaka ukweli uwekwe hadharani.
Viongozi wakana kuhusika
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahiga, Bumbile, wilayani Muleba, Jovin Tikyena na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kamanga, Sengerema mkoani Mwanza, Manumba Ndalawa, wamepinga tuhuma zinazoelekezwa kwao.
Wamesema katika maeneo yao hakuna uvuvi unaofanyika kwa kutumia makokoro na nyavu haramu na kwamba kuadimika kwa samaki kunatokana na walichokiita “mabadiliko ya tabianchi”.
Mwenyekiti wa Mahiga, Tikyeba, amekiri kuadimika kwa samaki kwenye mialo ya kijiji hicho, akisema: “Ni ziwa lenyewe ndilo limejifunga kutoa samaki. Hali kama hii haijawahi kushuhudiwa kabisa.
“Kwa sasa hupati hata kilo moja ya samaki! Wavuvi wanakwenda kuvua kwenye maji marefu, nao wanasema huko pia hakuna samaki. Hakuna mtu mwenye jibu kamili ni nini kimetokea.
“Kwa sasa kinachovuliwa ni ‘visamaki’ wala si samaki tuliozoea kuwaona. Hali ni mbaya. Nafikiri kitafika kipindi hata hivyo ‘visamaki’ navyo vitakwisha ziwani,” anasema Tikyeba.
Pamoja na hayo, Tikyeba amepinga kufahamu kuwapo matumizi ya nyavu haramu, akisema nyavu zinazotumiwa na wavuvi ni zenye matundu yenye kipenyo cha inchi sita na kuendelea.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kamanga, Ndalawa, amesema uhaba wa samaki Ziwa Victoria hasa Kamanga umesababishwa na tukio la mwaka jana ambapo samaki wengi walikufa ziwani.
“Mwaka jana samaki wengi walikufa na kuelea juu ya maji na hakuna sababu za kitaalmu zilizotolewa hadi leo. Nasikia hali hii ilionekana mialo karibu yote kuanzia Musoma hadi Bukoba.
“Tangu wakati huo wavuvi wakaanza kulalamika samaki kupungua ziwani,” amesema Ndalawa.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mahiga, Bugomba Daud, akisema vifo vya samaki vilishuhudiwa kwenye mialo ya kijiji hicho mwaka jana.
Amesema wavuvi wamelazimika kuhamia visiwa vya mbali kama Goziba, Kinagi na Kerebe karibu na Uganda kwenye maji marefu, lakini nako samaki hawapatikani.
“Hapa Mahiga hakuna nyavu haramu, labda kama zinaletwa na kutumiwa usiku wa manane, lakini hata ingekuwa hivyo tungejua tu,” amesema.
Alipotafutwa kutaka kauli yake kuhusu hali hiyo, Ofisa Uvuvi Wilaya ya Muleba, Wilfred Tibendelana, amekataa kuzungumza akitaka kwanza kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
“Hata hivyo, watu sahihi katika suala hili la upungufu wa samaki Ziwa Victoria ni Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI). Mimi si mtaalamu na kwa kawaida tafiti hupingwa kwa utafiti mwingine. Ninaweza nikakujibu kumbe sipo sahihi,” amesema.
Ushuhuda wa TAFIRI
Mmoja wa maofisa waandamizi wa TAFIRI aliyezungumza na JAMHURI (jina tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji wa taasisi), amesema upungufu wa samaki Ziwa Victoria umesababishwa na mambo mengi, akisisitiza kuwa chanzo kikuu ni uvuvi haramu.
“Kwenye utafiti tulioufanya mwaka jana tulibaini kuwa samaki wamepungua. Kuna siku tulitega nyavu kwenye maji marefu ndani ya saa mbili tukapata samaki mmoja tu.
“Hii ni tofauti na nyakati kama hizi siku za nyuma. Wakati huo ilikuwa ukitega nyavu kwa saa mbili, ukivuta mtego unapata kuanzia kilo 600 za samaki,” amesema ofisa huyo.
Wizara kuokoa jahazi, mdau atoa ushauri
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, ameliambia JAMHURI kuwa hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa kubaini matumizi ya nyavu haramu katika shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria.
“Nimetuma timu kwenda kuchunguza suala hilo na Alhamisi (ya wiki hii) italeta majibu. Ninakuhakikishia kuwa tunarejesha operesheni ya kukamata watu wenye nyavu haramu hata kama hawaipendi.
“Taarifa zako (JAMHURI) tunazipokea na tutazifanyia kazi. Sisi kila taarifa kwetu ni muhimu,” amesema Ndaki.
Kwa upande mwingine, Gazeti la JAMHURI limebaini kuanza kuporomoka kwa kipato cha watu, wakiwamo wakulima wa Kanda ya Ziwa.
Hali hii inatokana na kupungua kwa mzunguko wa fedha, hasa baada ya kudorora kwa shughuli za uvuvi.
Mmoja wa wakulima wa muhogo wilayani Muleba, Eustard Fulela, ameliambia JAMHURI kwamba biashara yake imeyumba kwa kuwa wateja wake, wavuvi, kwa sasa hawana fedha za kutosha.
“Matajiri waliowaajiri wamepunguza wafanyakazi kwenye shughuli za uvuvi, kwa hiyo siwezi kupeleka mzigo mkubwa kama zamani. Sasa hivi ninafikiria namna nyingine ya kufanya biashara hii ya mihogo,” amesema Fulela.
Wafanyabiashara wanaopeleka samaki viwandani wanadaiwa kukumbwa na hofu ya kushindwa kufanya marejesho ya mikopo waliyochukua benki baada ya uvuvi kuyumba.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, mkazi wa Mugaza wilayani Chato, Juvinary Atwenda, amesema ameanza kurejesha nyumbani vifaa vya kukusanyia samaki ili atafute biashara nyingine isiyohusiana na uvuvi.
“Mitaji ya watu sasa hivi inakatika mno, njia nzuri ya kujiokoa ni kuacha biashara hii kwa muda,” amesema Atwenda.
Atwenda anaishauri serikali kufunga shughuli za uvuvi kwa walau miezi mitatu au hata minne ili kutoa nafasi ya samaki kuzaliana.