Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa hali ya usalama jijini humo iko shwari na Serikali haitaruhusu aina yoyote ya uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Chalamila ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kufuata sheria pale wanapokuwa na malalamiko.
Amesisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo, na Serikali ipo tayari kuhakikisha hakuna mtu au kikundi kinachohatarisha utulivu uliopo.

Aidha, Chalamila amewaasa viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kushirikiana katika kulinda amani na utulivu hadi wakati wa uchaguzi utakapofika.

“Dar es Salaam ni jiji kubwa lenye shughuli nyingi, hatuwezi kuruhusu vurugu au maneno ya uchochezi,” alisisitiza Chalamila.