Waswahili tunasema: “Hakuna ziada mbovu.” Hii ni methali kongwe yenye maana kuongezwa jema ni manufaa, kwani hata kama halina kazi sasa, halitakosa kazi baadaye. Ni methali inayotaka tafakuri pana. 

“Kuongezwa jema” inatokana na asili tatu. Mosi, kutafuta kwa kufanya kazi. Pili, kuomba mahitaji, na tatu kuzawadiwa baada ya kuonyesha matendo mema. Asili zote hizi hutoa ziada kwa mtu, chombo au taifa. Hebu tuangalie katika maelezo yafuatayo ziada inavyotumika. 

Mtu hazuiwi kupata elimu zaidi juu ya fani au taaluma yoyote. Kuwa na stashahada au shahada ya kwanza haifungi mlango kupata shahada ya Uzamili au ya Uzamivu. Ndiyo maana watu wanasoma kila uchwao kupata maarifa mapya na ya ziada. 

Mkulima akipata mavuno mengi shambani mwaka huu, haina maana mwakani hatalima. La hasha! Atalima tu. Kwa sababu atahitaji mavuno ya ziada kwa ajili ya chakula, mauzo na mbegu kwa ajili ya msimu ujao. Kanuni hii inafuatwa na kila mkulima, na ndiyo inaziwezesha kaya kujitosheleza. 

Msanii hafungwi kuendeleza ujuzi katika kuchonga kinyago au kuchora picha kwa vile sanaa zake ni nzuri na bora. Ubora wa kazi zake haumzuii kutafuta ufundi zaidi. Aidha, msanii hagombwi kubuni na kutoa fikira mpya za tungo za nyimbo  na mashairi mengine, kwa vile tungo za awali zimesifiwa na kupendwa na jamii. Ataendelea na kazi kupata ziada. 

Kuwa na ajenda nzuri na sera bora za chama cha siasa haziwakatazi au kuwazuia wanachama na viongozi wao kubuni ajenda na sera mpya ambazo ni ziada kukishinda chama cha siasa pinzani, na kuhuisha uhai wa chama chao. 

Ndiyo maana chama kikifilisika kisera na kifikira, viongozi na wanachama wanatapatapa. Kwa hiyo ziada ni muhimu. 

Mfanyakazi au mfanyabiashara anapokuwa na fedha chekwa na mali tele haina maana ahitaji kuongeza fedha au kujilimbikizia mali. Ukweli anahitaji. Anafanya kazi usiku na mchana kutafuta fedha na mali zimwezeshe katika kutekeleza shughuli zake leo, kesho na siku zijazo. 

Iko mifano mingi ya kuongezwa jema ni manufaa. Nimetaja mifano michache kuonyesha si dhambi, si vibaya na si kosa kwa mtu, jumuiya au taifa lolote kuomba, kutaka au kuzawadiwa chochote kwa manufaa yake au yao. Mambo kama haya yanapofanyika uhusiano mwema unajengeka. 

Naamini si kosa kwa aliyeombwa kutoa au kutotoa. Ni hiari yake. Jambo muhimu ni kutengeneza mema kati ya mtoaji na mpokeaji. Yaani, kujenga urafiki, kusitawisha undugu na kuhuisha mawasiliano katika nyanja za utamaduni, siasa, uchumi na usalama. 

Jumuiya, au taifa kuwa na fedha, mali na watu wenye akili ni utajiri mkubwa, unaohitajika katika kupanga mipango ya maendeleo ya watu. Mikakati ya kiuchumi, utoaji huduma za jamii, ulinzi na usalama na utamaduni hupewa kipaumbele na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa. 

Kiongozi awe wa serikali, chama cha siasa, michezo na kadhalika, ni wajibu wake kuwa mwadilifu. Asipokuwa mwadilifu si kiongozi, huwa ni kama afiriti katika uongozi wake. Kiongozi wa aina kama hii ni hatari kuwa naye katika kaya hadi taifa. Ni juu ya taifa kuchukua hadhari juu ya mwenendo wake. 

Kiongozi anapoamua kuwachongea anaowaongoza, kuwasaliti anaocheka nao, kuwahadaa waliomchagua au kumteua, na kujikomba kwa wahisani apate mahitaji yake ni hatari sana kwa taifa. Hali kama hii isipewe nafasi,  na wananchi hatuna budi kukemea na kuchukua hatua za kisheria kuadhibu. 

Kiongozi anapokuwa na sura mbili kwa taifa naye pia ni hatari. Sura ya kuonekana ni mpenzi wa watu na mtetezi wa haki za wananchi. Sura ya pili ni msaliti. Ni juu ya wananchi kusoma sura hizi kwa umakini na kutoa uamuzi wa kweli juu yake. Tunasema kila mchelea mwana kulia hulia yeye. 

Natambua kusikia si kuelewa  na kuelewa si kutenda. Lakini utu, uungwana  na ustaarabu daima vinahitaji ujasiri wa matendo, na vinatuhimiza na kututaka tuwe wakweli si wanafiki. Wananchi wenzangu tufahamu na tukumbuke, “hakuna ziada mbovu.”