Namwona Deodatus Balile kwenye Malumbano ya Hoja (ITV). Anajitahidi kueleza, lakini inshangaza sana baadhi ya wasemaji kunadi kuwa uzalendo ni suala la hiari! Heee, ajabu sana!
Uzalendo unajengwa tena kwa gharama kubwa -tutake tusitake- siyo suala la mtu kuzaliwa na kusema kwa hiari yake atakuwa mzalendo no way. Watawala wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kujenga fikra za kizalendo ndani ya mioyo ya watu wake.
Hata tukitumia takwimu za kitafiti ili kuhalalisha uhiari wetu kuwa wazalendo ni kuleta hisia zisizoelekea kwenye uzalendo halisia. Siamini sana kwenye taarifa za kitafiti maana kuna upungufu mwingi na wakati mwingine matokeo hutegemea mhusika anataka kufanikisha kitu gani?
Mfano, Tanzania tunaripotiwa, hata kwa kutumia taarifa za kiutafiti, kuwa ni maskini. Sasa je, vigezo gani vinatumika? Mfugaji anayo mifugo yake zaidi ya 500 tunasema ni maskini eti kwa kuwa hana fedha mfukoni? Je, hiyo ni sawa?
Wengi hawana fedha, lakini wanazo mali za kutosha. Zamani sikuona baba yangu akiwa na fedha sana, lakini alikuwa na mali za kutosha – mashamba, mifugo na tulikuwa tunapata chakula chenye lishe ya kutosha hata kuliko wenye fedha mifukoni. Hakika hatukuwa maskini ingawa watafiti wangetuweka kwenye umaskini kwa kuangalia vigezo tofauti.
Tujiuulize, kwanini tunahitaji uzalendo? Kwa faida ya nani na bila kuwa wazalendo hasara yetu ni nini? Hatuwezi kujenga taifa la wenye uchoyo na ubinafsi mkubwa halafu tukasema tuwe na uzalendo wa hiari. Hiyo ni dhana potofu na ni kujidanganya na kuliangamiza taifa letu.
Uzalendo ni nguvu ya utaifa hivyo tunatakiwa kuwa na uadilifu mkubwa na nidhamu ya hali ya juu katika kufanya uamuzi na kuusimamia kwenye kuyatekeleza kwa faida ya walio wengi yaani wananchi wote.
Tuache ujanja-ujanja na tuweke maslahi ya nchi yetu mbele yaani kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli na yaliyo endelevu. Ubadhirifu wa aina yoyote ile upigwe vita na u-mimi uishe. Wengi wetu hatutaki kulipa kodi sababu ubinafsi umezidi na utaifa haumo ndani mwetu ndiyo maana huduma za kijamii zimezorota mno kwa muda mrefu. Pepo hilo baya likaripiwe kwa nguvu zote na lishindwe.
Kinachofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kutaka kuturejesha kwenye reli. Hivyo kubeza juhudi zinazofanywa sasa kwa lengo la kuelekea kwenye Tanzania ya Viwanda na kuondoa umasikini kwa kuboresha huduma za kijamii, ni kukosa uzalendo. Mwenyezi Mungu atujalie amani na hekima kubwa kwa faida ya wote.