Desemba 15, mwaka jana ulifanyika mkutano wa Shirika la Biashara Duniani (WTO). Mawaziri wa biashara kutoka nchi 162 wanachama walikutana jijini Nairobi, Kenya ili kuzungumzia mfumo wa biashara kimataifa.

Wajumbe 7,000 walimiminika Nairobi, wakiwamo wanaharakati na wawakilishi wa asasi za kiraia ambao walihudhuria kama watazamaji.

Kama kawaida ya mkutano huu, kulikuwako malumbano makali, hasa baina ya nchi za magharibi (tajiri) na nchi za kusini (masikini). Ilibidi mkutano urefushwe kwa siku moja na ukamalizikia Desemba 19. Malumbano haya yalianza mwaka 2001 wakati WTO ilipokutana mjini Doha na yangali yanaendelea.

Mkutano wa Nairobi ulihudhuriwa na mataifa 43 ya Afrika. Kati yao 33 yanatambulika kama mataifa ‘masikini’, pamoja na Tanzania, Uganda, Sudan Kusini na Ethopia Mwaka 2001 WTO ilianza mazungumzo mjini Doha (Qatar) kuhusu soko huria kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara.

Tangu wakati huo mazungumzo yamekuwa yakiendelea kwa muda wa miaka 14 bila mafanikio, kutokana na pingamizi zinazowekwa na nchi tajiri za magharibi. Wenyewe wanayaita mazungumzo ya Doha (Doha Round).

Hili suala la soko huria huwa linahubiriwa sana na nchi tajiri, wakidai kuwa ili nchi zetu ziendelee ni lazima tuondoe vikwazo kama kodi na ushuru ili kuruhusu mashindano ya kibiashara, yaani biashara holela. Je, hii ni kweli?  Tuanze na mfano wa India ambayo hivi karibuni imeamua kueneza umeme vijijini.

Raia milioni 400 nchini India hawana umeme. Hii ni robo ya raia wote. Sera ya serikali yao ni kuwafikishia umeme vijijini, lakini sera ya WTO (ikiongozwa na Marekani) imekuwa kikwazo kikubwa.

Ni kwa sababu serikali ya India inakusudia kutoa ruzuku na msamaha wa kodi kwa uzalishaji wa umeme kutokana na mionzi ya jua (sola). Umeme huu wa sola siku hizi unatiliwa mkazo ili kuepukana na umeme wa makaa ambao unachafua mazingira kwa kutoa hewa ukaa (kaboni) kwa wingi.

Wachafuzi wakuu wa mazingira ni nchi tajiri. Kwa mfano nchini India kaboni inayozalishwa ni wastani wa tani 1.7 kwa kila raia, wakati nchini Marekani ni tani 17 kwa kila raia. Hata hivyo ni nchi kama India ndizo zinazobanwa na nchi tajiri. Ndio maana India imeamua kupunguza umeme wa makaa na kuendeleza umeme wa sola kwa kuwawezesha wawekezaji/wazalishaji wa ndani badala ya kutegemea teknolojia hiyo kutoka nje.   

Lakini kanuni za WTO haziruhusu utoaji wa ruzuku, la sivyo India inaweza kuwekewa vikwazo vya kibiashara na mataifa tajiri kama Marekani. Matokeo yake India ikalazimika kusitisha ruzuku kwa umeme wa sola. Hii ni baada ya Marekani kuishitaki India katika WTO mwaka 2013, ikidai kuwa eti ruzuku ya India inazuia uagizaji wa vifaa vya sola kutoka nje (magharibi).

Hivi sasa India inazalisha asilimia 71 ya umeme kutokana na makaa. Ni sehemu ndogo sana inatokana na sola. Makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa mjini Paris hivi karibuni yanazitaka nchi zote zipunguze utumiaji wa makaa na badala yake zitumie njia mbadala na endelevu kama vile sola na upepo. Ndio maana India ikaanzisha mradi wa kuendeleza umeme wa sola.

Chini ya mradi huu India imekaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vya kutengeneza vifaa vya sola. Serikali ikaweka masharti kuwa sehemu kubwa ya bidhaa ghafi na vipuri kama vile beteri na mabango ya sola ni lazima yatoke ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje. Hii ni sera ya kujitegemea kiuchumi kwa kutengeneza vipuri ndani ya nchi. Serikali ikatoa ruzuku ili kuwawezesha wenye karakana za vipuri wazalishe kwa bei nafuu.

Hapa ndipo Marekani ilipokuja juu. Wakaona watakosa soko, kwani hivi sasa sehemu kubwa ya bidhaa ghafi za sola zinaagizwa kutoka Marekani. Ndipo Marekani ikalalamika kwa WTO kwa kusema eti India inawabagua. Cha ajabu ni kuwa Marekani yenyewe “inaisaidia” India kuzalisha umeme wa sola. Imetoa dola bilioni 4 ili kuendeleza sekta hii nchini India. Makubaliano yalitiwa saini Novemba 18, 2014. Lakini India imetakiwa itumie fedha hizo kuagiza vipuri kutoka Marekani. Kwa maneno mengine Marekani inatoa “misaada” ili kukuza biashara yake.

Ni sawa na kutoa ruzuku kwa wazalishaji wake ili waweze kutawala masoko ya kimataifa. Yaani hizo fedha za “misaada” kwa India zisitumiwe kuwezesha wazalishaji wa India, bali zitumiwe kwa maslahi ya kampuni za Marekani.

Wakati Marekani “inaisaidia” India kuendeleza sola, wakati huo huo inaishitaki kwa WTO kuwa eti inazibagua kampuni za Marekani kwa kuzuia uagizaji kutoka nje.  

Kwa vile WTO (kwa shinikizo la Marekani) imeikataza India isitoe ruzuku kwa wazalishaji wa ndani, maana yake sasa India italazimika kununua vipuri na malighafi kutoka Marekani. Yaani ilichofanya Marekani ni kutoa mkopo kwa India ili kuzisaidia kampuni za Marekani ziweze kuzalisha na kuuza bidhaa kwa India. Hiyo ni ruzuku ya Marekani kwa kampuni za Marekani.

Msimamo wa Marekani kuikataza India isitoe ruzuku kwa wazalishaji wake ni unafiki. Ni kwa sababu Marekani yenyewe inatoa ruzuku kwa kampuni zake zinazosafirisha bidhaa za sola nje ya nchi. Katika muda wa miaka mitano iliyopita ruzuku iliyotolewa ni wastani wa dola bilioni 39 kila mwaka. Idara yao ya kodi inatoa msamaha wa asilimia 30 kwa wawekezaji wa sola.

Wakati Marekani inalalamika kuwa India inawalinda wazalishaji wake wa ndani, wakati huo huo Marekani inazilinda kampuni zake za sola. Kwa mfano nchi hiyo inatoza kodi kubwa kwa vifaa vya sola kutoka China.  Lakini China haikunyamaza kimya, kwani iliishitaki Marekani kwa WTO na ikafanikiwa. Kwanini India nayo isifanye hivyo?

Ni kwa sababu India inahitaji uwekezaji wa dola takriban bilioni 100 za Marekani ili kufanikisha mradi wake wa sola. Zaidi ya nusu ya fedha hizi ni kutoka nje, hasa Marekani. Sasa iwapo India itailalamikia Marekani katika WTO maana yake itakosa mtaji huo. Haya ndiyo matatizo ya Waziri Mkuu Modi. Analazimika kupeana mikono na Rais Barack Obama na kutabasamu mbele ya kamera.

Ikiwa India inakabiliwa na masharti kama haya kutoka magharibi, sembuse nchi zetu za Afrika ambazo ni tegemezi zaidi? Ndiyo maana utakuta rais wetu akikimbilia Washington mara kwa mara ili kupeana mikono na Rais Obama na kutabasamu. Kwa maelezo zaidi ni vizuri tukaangalia mifano ya Afrika.

Mwaka 2003 katika Mkutano wa Baraza Kuu la WTO, Burkina Faso ilizungumza kwa niaba ya nchi za Kiafrika zinazozalisha pamba kwa wingi. Walilalamika sana jinsi uchumi wao ulivyokuwa ukididimia kutokana na sera ya Marekani ya kutoa ruzuku kwa wakulima wake wa pamba. Kwa kweli bei ya pamba ulimwenguni iliporomoka kwa asilimia 10 kutokana na ruzuku hii ya Marekani.

Bei ikianguka kwa asilimia 10 duniani, maana yake mkulima wetu wa Mwanza na Geita anapungukiwa asilimia 20. Matokeo yake anaachana na pamba na kutafuta ajira mijini.

Katika nchi za Afrika Magharibi mashamba 900,000 ya pamba yaliathirika, yakiwa yanaajiri wakulima milioni 7 hadi 8. Ukichanganya na familia zao ni jumla ya watu milioni 13 waliathirika kutokana na kuanguka kwa bei ya pamba kulikosababishwa na ruzuku nchini Marekani. Hili si tatizo la mwaka 2003 tu, bali linaendelea hadi leo. Katika mkutano wa WTO jijini Nairobi; Burkina Faso na nchi nyingine zilirudia tena madai yao na mara nyingine Marekani ikakataa kuacha kutoa ruzuku kwa wakulima wake wa pamba. Halafu wanatufundisha kuwa soko huria eti ni sera bora kwa maendeleo yetu!

Mfano mwengine ni nchi ya Kenya ambako zao moja kubwa linalosafirishwa hadi Ulaya ni maua. Huzalishwa kwa wingi karibu na Ziwa Naivasha ambalo hupata maji yake kutoka mito ya Malewa na Gilgil. Msomi mashuhuri wa Uganda, Profesa Tandon anasema katika ujana wake mnamo mwaka 1957 alitembelea maeneo hayo na akashuhudia ardhi yenye rotuba. Aliona mito yenye maji safi iliyojaa miti na wanyama wa kila aina, kuanzia ndege aina ya korongo, flamingo hadi viboko na vipepeo.

Aliona maelfu ya wavuvi wakivua samaki kwa wingi na wakulima wakipata maji ya kutosha kwa mashamba yao yaliyosheheni nafaka.

Anasema mwaka 2009 alitembelea tena na kukuta vyote hivi vimetoweka. Badala ya vipepeo, samaki na ndege sasa kuna mashamba makubwa ya maua yanayomilikiwa na kampuni kubwa zinayoajiri vibarua.  Hata nyakati zile mamia ya wakulima walikuwa wakilima maua pamoja na chakula chao. Leo wanaajiriwa na wawekezaji kutoka nje waliovamia ardhi ya wakulima wadogo. Matajiri wanatajirika na vibarua wanaishi maisha duni.

Kuna watakaosema  haya ni maendeleo. Lakini ni maendeleo baada ya kuteketeza mazingira na maisha ya wananchi wa kawaida. Hapa kwetu kuna wanaohubiri ‘maendeleo’ ya aina hii. Wanayaita ‘Kilimo Kwanza’.

Wanadai maendeleo yatakuja kwa kupitia soko huria na wawekezaji wakubwa. Huko vyuoni wanafunzi wetu watalazimishwa kumeza ‘nadharia’ hiyo na kujibu maswali wakati wa mitihani. Ni wachache kati yao wataambiwa ukweli kuwa hakuna kitu kama hicho. Soko huria haikuwapo hata wakati Ulaya ilipoingia katika mfumo wa kibepari, sembuse leo wakati wa uliberali mambo-leo?

Wanafunzi wetu hawatafundishwa kuwa wakati Marekani ilipoanza kujenga ubepari ilikataa katukatu soko huria. Nchi hiyo ilipojikomboa kwa mtutu wa bunduki kutoka ukoloni wa Uingereza mwaka 1776, watawala wapya wa Marekani wakawaambia wakoloni wa Uingereza: “Hatutakubali tena kuendelea kuwazalishieni pamba na tumbaku, na kisha tukanunua bidhaa kutoka viwanda vyenu. Kwani nasi pia tunataka kujenga viwanda.”

Ndipo Marekani ikapiga marufuku bidhaa kutoka Uingereza na badala yake wakaanza kuunda bidhaa zao wenyewe. Hivi ndivyo walivyoleta mapinduzi ya viwanda, siyo kwa kupitia soko huria.

Huu ni mfano mmoja tu wa Marekani. Kuna nchi nyingi ambazo pia zimeendelea kwa kuviwezesha viwanda vya nyumbani na kuzuia bidhaa kutoka nje. Ni pamoja na nchi za Asia kama Japan na Korea.

Leo Afrika tunaambiwa turuhusu biashara holela, eti hivi ndivyo tutakavyoendelea. Tutapokea ‘misaada’ itakayotumika kununua bidhaa kutoka kwao na kuwalipa mishahara na posho za kufuru ‘washauri’ kutoka kwao.

 

0713-562181

[email protected]