Kufuatia kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa Watuhumiwa wawili wanaodaiwa kufanya udanganyifu kuwa wao ni maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwa wanao uwezo wa kusamehe Madeni ya Kodi, Kamishna Mkuu wa TRA Bw.Yusuph Juma Mwenda amesema hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kisheria kufuta Madeni ya Kodi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA leo tarehe 06.03.2025 imeeleza kuwa hata watumishi wa TRA hawana nguvu za kisheria kufuta madeni halali ya kodi kwa Walipakodi. Isipokuwa, deni la kodi linafutwa kwa kulipwa. Kwa muktadha huo, kinachotakiwa ni mtu anayedaiwa kulipa deni lake kwa taratibu za Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtu anapochelewa kulipa madeni ya kodi anasababisha kutozwa riba na adhabu hali itakayomlazimu kulipa deni kubwa zaidi ya awali.
Sheria za Usimamizi wa Kodi zimetoa ruhusa ya Kusamehe Riba na Adhabu Kwa masharti Maalumu na SIO kusamehe au Kufuta kodi halali. Kwa upande wa Riba na adhabu Sheria imetoa ruhusa kwa mdaiwa kuomba msamaha wa Adhabu na Riba kwa Kamishna Mkuu kwa kuzingatia vigezo na sababu zinazotolewa na anayeomba kusamehewa.
“Kifungu cha 70 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, kama ilivyorekebishwa ikisomwa pamoja na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021, kinampa Kamishna Mkuu uwezo wa kusamehe riba na adhabu kwa Kodi za ndani. Aidha, kifungu cha 249 cha Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 kinampa mamlaka sawa katika masuala yanayohusiana na ushuru wa forodha” imeeleza taarifa ya Kamishna Mkuu Mwenda.
Pia Kamishna Mkuu Mwenda katika taarifa yake ameeleza kuwa yeyote anayetoa ahadi ya kufuta deni la kodi anafanya udanganyifu na utapeli na ni kosa kwa mujibu wa Sheria.
“Tunawaomba na kuwatahadharisha Walipakodi wetu wa thamani wasimuamini mtu yoyote anayedai ana uwezo wa kufuta deni la kodi, hao ni matapeli, na pindi wanapokutana nao watoe taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kupitia simu namba 0800750075 au 0800780078 bure au watoe taarifa ofisi yoyote ya TRA nchini” imeeleza taarifa ya Kamishna Mkuu Mwenda.
Taarifa hiyo ya Kamishna Mkuu Mwenda imeeleza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), itachukua hatua kali kwa mujibu wa Sheria kwa yeyote anayedanganya na kutapeli kwamba anaweza kufuta deni la Kodi kwa lengo la kuwaibia walipakodi na wananchi
