Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, wakati wowote wiki hii, anatarajiwa kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Kama ilivyo ada, Wizara ya Maliasili na Utalii ni miongoni mwa wizara chache zenye mvuto, na kwa maana hiyo hupata orodha ndefu ya wabunge wanaochangia.
Mvuto wa wizara hii unatokana na sababu kadhaa. Mosi, hii ndiyo wizara inayoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. Takwimu za karibu zilizotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, zilionesha kuwa sekta ya utalii inaongoza kwa kuliingizia Taifa dola bilioni 2 za Marekani kwa mwaka, ikifuatiwa na dhahabu (dola bilioni 1.7), mazao ya viwandani (dola bilioni 1.3).
Bila shaka, kiwango hiki cha utalii ni mbali kabisa na manufaa ya mwananchi mmoja mmoja kiuchumi anayopata kutokana na ujio wa watalii nchini. Wataalamu wa utalii bado wanaiona Tanzania kama nchi iliyo nyuma zaidi katika kuvutia watalii wengi zaidi. Mathalani, nchi kama Misri ambayo haina vivutio kama ilivyo Tanzania, pato lake linalotokana na utalii ni dola za Marekani bilioni 11 kwa mwaka!
Pili, wizara hii ina mvuto kwa sababu inagusa maisha ya kila siku ya mwananchi. Faida zinazotokana na Hifadhi za Taifa, Mapori Tengefu, Mapori ya Akiba na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ni kubwa mno. Kutokana na maeneo hayo, wananchi wanapata ajira, maji, hewa safi na faida nyingine nyingi.
Tukijielekeza kwenye faida zitokanazo na maliasili na utalii, tunaweza tusiwe na sababu ya kuchimba madini. Tunaambiwa mgodi wa Buzwagi unafungwa mwaka 2020 baada ya dhahabu ‘kukombwa’. Kufungwa kwa mgodi huo ni salamu kwa wana-Kahama kujiandaa kuanza maisha mapya. Dhahabu ikiisha mahali, imekwisha. Haioteshwi! Buzwagi sasa ni mashimo na milima ya mawe.
Tofauti na dhahabu au madini mengine, Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na maeneo mengine, ni hazina ambayo tukiitunza vizuri, manufaa yake ni ya milele.
Naomba wabunge waniwie radhi kwa kuyarejea maneno haya hapa chini. Septemba, 1961, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitoa maneno yaliyokuja kuitwa Ilani ya Arusha. Hapa tunaona kuwa hata kabla ya Uhuru, Mwalimu alishatambua umuhimu wa kuwalinda wanyamapori na misitu, na hivyo akatoa mwelekeo (Ilani) ya kuuhifadhi urithi huu. Mwalimu alisema maneno haya:
“Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.
Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.
Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri siyo tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”
Mwalimu huyo huyo, akizungumza na viongozi wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na wa Serikali mkoani Kilimanjaro; Agosti 10, 1975, alieleza makosa yanayowagharimu watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani yaliyotokana na dhambi ya kuwaua wanyamapori na kuharibu misitu katika mataifa yao. Mwalimu alisema:
“Ni vizuri kujifunza kwa wenzetu waliotangulia. Na wakati mwingine ni kujifunza kutokana na makosa yao. Wenzetu waliotangulia tunaowasema zaidi ni wale wa nchi zilizoendelea sana hasa za Ulaya na Amerika Kaskazini.
Wamefanya makosa mawili makubwa – wao wanajua, sisi hatujui. Wao wanajua kwa sababu wameyafanya makosa hayo, sisi kwa sababu hatujayafanya hatujui kwamba ni makosa. Moja mtashangaa nikilitamka. Wameharibu sana nchi zao kwa kitu wanachokiita maendeleo. Wameua vinyama vingi sana vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu – vingi. Wameua vyote. Hawana tena makundi makubwa makubwa ya wanyama kama tuliyonayo katika Afrika na hasa katika Tanzania. Hawana kabisa. Sasa wao wanajua kwamba wamefanya makosa, na wanakuja huku wanatwambia; ‘Sisi tumefanya makosa, tumeua wanyama wetu wote tumemaliza, tafadhalini msiue wanyama wenu.’ Sisi tunawaona kama wajiiinga wanapotuambia hivyo. Lakini wao wanajua kosa kubwa la kufuta wanyama na kuwamaliza; na kukatakata misitu yao na kuimaliza. Wanajua kosa walilolifanya na wanatuomba tusilifanye kosa hilo. Sasa wanakuja kwa wingi, ndio hao mnawaita watalii. Wanakuja kwa wingi kuja kuona wanyama. Wewe unamshangaa huyu mtu mzima anatoka kwao mbaaaaali kuja…anatoka kwao mbaaaali, analipa hela kuja kuona tembo, kwanini. Ana akili, hana akili! Ni kwa sababu ana akili ndio maana anatoka kwao mbaaali sana, analipa fedha anakuja kuona tembo. Angekuwa hana akili asingekuja. Anajua faida ya kuwa na matembo, na masimba, na manyati, na machui, na mapundamilia katika nchi hii, lakini kwao wameshafuta. Sasa wanaanza kutuomba, wengine wanaanza kutuomba tuwauzieuzie angalau wafufuefufue, lakini kufufua si jambo jepesi. Ukishaifuta misitu, kuifufua na kuweka wanyama waishi kama walivyokuwa zamani ni vigumu sana, kwanza hali yake ile ni tofauti. Huwezi kuifufua, vigumu sana. Wala hawajui ilikuwaje hata waweze kuifufua. Sasa nasema wanatushawishi – Wazungu wanatushawishi katika jambo hilo ambalo hatujafanya kosa, tusifanye kosa.
Serikali ya Tanzania imekubali, nadhani wananchi wanaanza kukubali kutofanya kosa hilo lililofanywa na wenzetu. Tuhifadhi wanyama wetu na tuhifadhi misitu yetu. Tusivuruge vuruge mazingira ambayo tumeyarithi, na kwa kweli hatujui yamechukua muda gani hata yakawa hivyo; halafu tunafika sisi tunaita maendeleo tunavuruga vuruga, tunaharibu; tunaua wanyama, tunakata miti. Matokeo yake hatuwezi kuyajua. Mwisho wa kunukuu.
Maneno haya ya Mwalimu yatupasa tuyatumie kama mwongozo thabiti wa kuwalinda wanyamapori na vyote vilivyomo kwenye misitu yetu ya hifadhi. Nayasema haya kwa sababu wabunge kadhaa wana mchango mkubwa katika kuharibu rasilimali hii. Wapo waliopata ubunge kwa sababu ya kuwaahidi wapigakura kwamba endapo wangewachagua, basi wangehakikisha msitu au hifadhi inamegwa ili kuwapa fursa kulima na kuendesha shughuli nyingine za kibinadamu.
Wanasiasa wameshirikiana na matajiri kuvamia maeneo yote ya hifadhi nchini. Wananunua ng’ombe maelfu kwa maelfu na kwenda kuwanenepesha hifadhini. Leo hii Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ndiyo pekee iliyosalia katika sayari hii (dunia) kwa kuwa na msafara wa wanyamapori wanaohama, imevamiwa na wafugaji wengi. Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu yote yamevamiwa. Raia wa kigeni wamejazana kwenye maeneo yetu, na pale Serikali ilipothubutu kuwaondoa, kelele za wanasiasa na wale wanaojiita ‘watetezi wa haki za binadamu,’ ziliweza kukwamisha mpango huo halali kisheria.
Sasa Rais John Magufuli anaagiza ndege. Anataka zitoke Marekani, Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na kwingineko duniani – zije moja kwa moja hadi Dar es Salaam au Kilimanjaro. Kuna ndege yenye kubeba abiria 270 ambayo tunaambiwa itakuwa ikitoka New York, Marekani hadi Tanzania bila kutua popote njiani. Dhamira ya Rais ni kuona watalii wanapunguziwa adha na gharama za ndege zinazotokana na kutumia mashirika ya kigeni. Huu ni mpango mzuri.
Lakini mpango huu hautakuwa na faida yoyote, na tunaweza kujutia kupoteza mabilioni ya shilingi endapo Serikali yetu na wanasiasa wataendelea kuwa sehemu ya uharibifu wa hifadhi zetu nchini.
Hakuna mtalii anayeweza kulipa maelfu ya dola kuja kuangalia mbuzi, kondoo, ng’ombe, mbwa na punda-vihongwe waliojazwa Ngorongoro, Serengeti, Mikumi, Burigi, Selous, Ruaha na kwingineko. Hakuna mtalii mbumbumbu wa kupoteza fedha zake kuja kuona viumbe hao. Hayupo.
Hakuna mtalii aliye tayari kuja nchini mwetu kuangalia matanuri ya mkaa, kuni na ukataji miti unavyofanywa katika maeneo ya hifadhi. Hayupo. Hakuna mtalii anayesafiri maelfu ya kilometa kuja kupokea hadithi za ujangili namna unavyowamaliza wanyamapori nchini. Wala hakuna aliye tayari kuyaona hayo makosa halafu akarejea kwao akitusifu na kutupamba kwa lengo la kuwashawishi wenzake waje nchini. Hayupo.
Mtalii anataka akifika katika hifadhi zetu akutane na kile anachokisoma na kukisia. Anataka aone kile ambacho mababu na mabibi zake waliteketeza kwao. Anataka kuja kuona fahari ya kazi ya Mungu, na si man-made activities kama zile za Misri! Anataka atoke Tanzania akiburudika na aone value for money.
Mambo makubwa ya kuijenga nchi yanahitaji dhamira, siyo njema tu, bali inayotekelezeka. Serikali haiwezi kumfurahisha kila mtu. Leo ikisema wachungaji (ambao wengine huwaita wafugaji) waongezewe eneo, hata wakipewa Serengeti yote hawatatosheka. Wabunge wawafanye wapigakura wao wawe wafugaji badala ya kuwa wachungaji kama walivyo sasa.
Huu ni wakati wa kuwaondoa waliovamia maeneo yote ya hifadhi nchini. Hili suala halihitaji kuingiliwa kisiasa. Siasa inaua uhifadhi. Hili ni jambo lenye kugusa hatima ya uchumi wetu. Kama Taifa, walimwengu watatucheka endapo tutaruhusu kufa kwa hifadhi zetu.