πŸ“Œ Asisitiza uwekezaji katika elimu inayozingatia sayansi, teknolojia na ubunifu

πŸ“Œ Awasihi Watanzania kuziishi falsafa za Mwl. Nyerere

πŸ“Œ Chuo cha Mwl. Nyerere cha adhimisha miaka 103 ya kuzaliwa kwa Mwl. Nyerere

Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa Watanzania kuendeleza fikra za Mwl. Nyerere kwa kuwekeza katika sekta za elimu, kilimo, viwanda, teknolojia na biashara ndogo ndogo zinazotegemewa na wananchi wengi ili kukuza uchumi jumuishi.

Aidha, Serikali na sekta binafsi zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa wananchi wa kawaida.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika Kongamano la Kumbukizi ya Kuzaliwa Kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Amesema Kongamano hilo lenye mada inayosema Maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Elimu, Uwekezaji na Ujenzi wa Taifa lenye Amani kwa Maendeleo ya Watu ni fursa ya kufanya tafakuri kwa baadhi ya mambo ambayo Baba wa Taifa aliyaamini, aliyaishi na anaendelea kukumbukwa nayo.

β€œMaono ya Mwalimu kuhusu uwekezaji kwa maendeleo yalilenga kuimarisha uchumi wa Taifa kwa misingi ya usawa na uwajibikaji wa pamoja.


Alisisitiza kuwa uwekezaji lazima uwalenge wananchi na kuhakikisha kwamba rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wote. Alipinga mifumo ya kiuchumi inayozalisha matabaka na ukosefu wa haki, huku akihimiza ujamaa na kujitegemea,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Mwl. Nyerere alitamani kuona elimu inampa mwanafunzi maarifa ya kumwezesha kuchangia maendeleo ya jamii yake na sio ya kumtenga na mazingira yake. Aidha, jamii inapaswa kujiuliza ikiwa sasa elimu inawajenga Watanzania kuwa raia wenye uwezo wa kutatua matatizo yao na kuchangia maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Amebainisha kuwa katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kiteknolojia na kiuchumi, ni muhimu kuwekeza katika elimu inayozingatia maendeleo ya sayansi, teknolojia, ubunifu na stadi za maisha ili kujiletea maendeleo ya kweli.

Akizungumzia umuhimu wa amani, Dkt. Biteko amesema kuwa hakuna maendeleo yanayowezekana bila amani na mshikamano wa kitaifa.

β€œKupitia misingi ya utaifa na umoja, aliweza kujenga Taifa lenye mshikamano thabiti licha ya tofauti za kikabila, kidini, na kijamii. Leo taifa letu linanufaika na amani, umoja na upendo wa kindugu ambavyo Baba wa Taifa alivijenga kwa juhudi kubwa,”amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara, Mhe. Stephen Wasira ameelezea sifa na jitihada mbalimbali alizofanya Mwalimu Nyerere wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika kutoka kwa wakoloni.

β€œAliunganisha nchi zetu kwa sababu aliamini Afrika lazima iwe moja, aliaamini katika umoja, leo tunakumbuka miaka 103 ya kuzaliwa kwake, kiongozi ambaye aliongoza Taifa hili kwa miaka 24,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo.

Naye, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Prof. Haruni Mapesa amesema kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwa kiongozi wa kitaifa pekee bali kimataifa na aliyeweka misingi muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Amesema Chuo hicho kilianzishwa na Mwl. Nyerere na baadaye kuwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere na kina dira ya kuwa kitovu cha utoaji wa elimu bora na kuendeleza amani nchini.

Amebainisha kuwa Chuo hicho cha Mwl. Nyerere kimekuwa na desturi ya kufanya makongamano hayo kila mwaka kwa lengo kuenzi, kuzungumza na kupigia debe mawazo na falsafa na misingi yake katika Taifa.

β€œ Mwalimu aliamini kuwa elimu ni nyenzo kuu ya uongozi na alisisitiza elimu ya kujitegemea. Leo tunapomuenzi tujiulize je tunazifuata falsafa zake za elimu kuwaandaa vijana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa au kuwa watafuta ajira,” amesema Prof. Haruni.

Pamoja na hayo, ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chuoni hapo katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni maboresho makubwa ya miundombinu ya kujifunza na kufundishia.

Licha ya maboresho hayo, Prof. Mapesa amesema Chuo hicho kinaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maktaba ya kisasa itakayo hifadhi machapisho mbalimbali yenye tija kwa Taifa.

Ameongeza kuwa Chuo hicho kinatimiza lengo la Mwl. Nyerere la kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu ya sayansi ya jamii, uzalendo na uongozi katika maeneo mbalimbali waliyopo, na kuwa sasa wana wahadhiri wenye shahada ya uzamivu wafikao 59 na wengine wakiendelea na masomo na ndani ya kipindi cha miaka miwili watakuwa na wahadhiri wenye shahada ya uzamivu 100.

Aidha, kupitia Kongamano la mwaka huu kumekuwa na mashindano ya insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari juu ya Mchango wa Mwalimu Nyerere kuhusu Elimu ya Kujitegemea katika Maendeleo ya Taifa.

Lengo la mashindano hayo ni kuwafanya vijana kuendelea kujifunza kuhusu falsafa za Baba wa Taifa na kuzitumia ambapo Dkt. Biteko alikabidhi zawadi kwa washindi pamoja na yeye kutunukiwa tuzo na Chuo hicho.