Haki ya mwanamke ni suala linalohitaji kupewe umuhimu wa kipekee katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen-Kijo Bisimba, amesisitiza suala hilo katika mafunzo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalihusu haki za mwanamke kwenye Katiba, ushiriki wa vyombo vya habari kwenye mabaraza ya Katiba na haki za binadamu na ving’amuzi.
“Suala la haki za binadamu, hasa ya mwanamke hapa nchini, liwekewe kipaumbele ili kuleta ujira stahiki kwa wakati na unaozingatia usawa kati yake na mwanaume,” amesema Bisimba.
Amesema kumekuwapo ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa kwa wanawake kwa muda mrefu nchini, kutokana na mila, desturi na tamaduni za babu zetu.
Ametoa mifano kwamba huko nyuma mwanamke amekuwa akipewa nafasi ya chini ya mwanaume, jambo lililosababisha kutolewa kwa tamko rasmi la kutambua haki za wanawake ulimwenguni mwaka 1948.
Kutokana na tamko hilo, mwaka 1979 ulitungwa mkataba wa kuondoa aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake katika masuala ya uchumi na siasa, jambo lililowezesha kuwapo kwa maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, Machi 8, kila mwaka.
Mwaka 1993 lilitolewa tamko la kuondoa aina ya kijinsia ili kuweka usawa baina ya wanawake na wanaume, ambalo lilisaidia kudhibiti ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alikosoa Katiba iliyopo kwamba haijazingatia kwa upana haki za binadamu, hasa haki za mwanamke, ambapo alitolea mifano ya sheria kama ile ya Ibara ya 13 kwamba ina upungufu.
Ametaka pawepo na marekebisho kwa kufafanua kwa kina haki za mwanamke, ili kuondoa ukatili na ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya kundi hilo la jamii.
Anatoa mifano kuhusu haki ya usawa kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kulinganisha katiba za mataifa mengine, hasa kwa kuangalia Katiba ya Scandinavia namna ilivyowezesha wananchi wa taifa hilo, kupiga hatua katika kuzingatia haki za binadamu, hasa haki za wanawake.
Anasema suala la kupewa likizo ya uzazi ni suala ambalo halipewi kipaumbele katika kuleta haki kwa mwanamke hapa nchini, hali ambayo ni tofauti na nchi zilizoendelea kama za Scandinavia, ambapo mwanamke ana haki ya kisheria ya kupewa likizo ya miezi 10 baada ya kujifungua ili kumwezesha kupumzika na kuboresha afya yake na mtoto aliyezaliwa.
“Haki nyingine zinazotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na haki za kufanya kazi kwa usawa katika sekta zote, kupewa fursa sawa katika ngazi ya uongozi ikiwamo ya urais na nyinginezo ambazo hazikupewa uzito unaostahili katika Katiba ya sasa,” anasema.
Naye Wakili na Mkuu wa kitengo cha Katiba wa LHRC, Anna Henga, akielezea kwa niaba ya Mkuu wa Dawati la Mkataba wa Maputo na Jinsia wa kituo hicho, Fatuma Semgaya, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayowalinda wanawake kwa namna moja au nyingine.
Amesema ipo mikataba ya kimataifa na ya kikabila mbalimbali inayoainisha haki za wanawake kama ule wa kwenye Tamko la Umoja wa Mataifa wa Uondoaji wa Ukatili Dhidi ya Wanawake wa mwaka 2005.
Mkataba huo unazuia vitendo vya ukatili kuhusu jinsia, kusababisha madhara au maumivu, mateso ya kimwili, au kisaikolojia kwa mwanamke, kutishia, kulazimisha na kunyima uhuru.
Akitoa mfano wa haki za wanawake katika sheria za Tanzania, Henge amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 12 (usawa wa binadamu), ibara ya 13 (usawa mbele ya sheria – ubaguzi) ni miongoni mwa sheria ambazo hazijitoshelezi kuondoa ubaguzi huo.
Amependekeza kuwa katika haki za wanawake kwenye Katiba mpya, baada ya kuangalia sheria na mikataba ambayo inalinda haki za wanawake Tanzania na mazingira yanayosababisha ukiukwaji wa haki za wanawake, mchakato wa Katiba ni nafasi muhimu ya kutoa mapendekezo ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba hiyo.
“Katiba ya nchi lazima iainishe kwa ufasaha misingi yote ya haki za binadamu, yaani kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo na kuweka ulinzi madhubuti wa haki hizo.