Mtuhumiwa ni nani?

Ni mtu yeyote anayewekwa chini ya ulinzi na polisi au chombo cha usalama kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai.

Makosa ya jinai ni yapi?

Ni makosa ambayo mtu akipatikana na hatia hupewa adhabu. Ni makosa kama wizi, ubakaji, mauaji, kufanya makosa ya kuhatarisha amani na mengine ya namna hiyo.

Haki za mtuhumiwa

Mtuhumiwa anapowekwa chini ya ulinzi ana haki ya kuelezwa sababu za kukamatwa au kutiliwa shaka.

Mtuhumiwa ana haki ya kudai risiti ya orodha ya vyombo/mali atakayokuwa nayo wakati wa kumpekua zile zinazochukuliwa kituoni na pale anapokabidhiwa polisi.

Mtuhumiwa akiwa mwanamke lazima kukaguliwa na polisi mwanamke.

Mtuhumiwa ana haki ya kudai kibali cha hakimu pale majadiliano au maelezo kwa polisi yanapozidi saa nane.

Mtuhumiwa anayo haki ya kudai awasiliane na mtu anayemtaka akiwa chini ya ulinzi. Kwa mfano rafiki, ndugu au wakili.

Mtuhumiwa ana haki ya kufikishwa mahakamani katika muda usiozidi saa 24.

Mtuhumiwa ana haki ya kukaa kimya wakati wa mahojiano na polisi na anapaswa kuelezwa kwamba chochote ambacho mtuhumiwa atawaeleza polisi kinaweza kutolewa mahakamani kama ushahidi dhidi yake.

Mtuhumiwa ana haki ya kutojibu maswali ya polisi na kukaa kimya hadi polisi anayemuuliza au anayeendesha mahojiano awe amemueleza mtuhumiwa yafuatayo:- Kwanza, cheo alicho nacho na jina lake.

Pili, amtahadharishe kwamba yuko chini ya ulinzi.

Tatu, kosa alilofanya au sababu ya kuwa chini ya ulinzi. Mtuhumiwa anaweza akaomba dhamana wakati yuko chini ya ulinzi wa polisi.

Haki wakati wa mahojiano

Zifuatazo ni haki za mtuhumiwa wakati wa mahojiano mikononi mwa askari polisi:- Kwanza, kupata utambulisho kutoka kwa askari polisi anayefanya mahojiano. Hii ni pamoja na kueleza jina, cheo chake na sababu za kutiwa nguvuni.

Pili, kuelezwa kwa lugha fasaha inayoeleweka kwa mtuhumiwa.

Tatu, kupata tahadhari kutoka kwa askari polisi anayehoji kwamba hawajibiki kujibu maswali yote isipokuwa yale yanayohusu maelezo binafsi (wasifu wake) na jina lake. Hivyo mtuhumiwa ana haki ya kutojibu.

Nne, kuwasiliana na mwanasheria wake au ndugu zake akiwa mikononi mwa polisi, isipokuwa kama kuna sababu ya msingi ya kuzuiliwa asiwasiliane na hao wahusika.

Tano, kuthaminiwa utu wake pamoja na haki zake za binadamu.

Sita, haki ya kudai asomewe kilichoandikwa kabla ya kuweka sahihi kwenye maelezo.