Katika makala yaliyopita nilizungumzia ukweli kuwa nguzo mojawapo ya amani. Nilisema ukweli ni jambo ashrafu na ni nguvu moja ya amani. Watanzania hatuna budi kuelewa, kuthamini, kukumbuka na kutumia ukweli katika majadiliano na mazungumzo yetu, na wenzetu wa nchi za nje.
Wahenga walisema ukweli unapodhihiri uongo hujitenga. Hii ina maana kuwa hali ya uonevu, dhuluma na mashaka haipo, badala yake hali ya upendo na nguvu ya imani hujichomoza na kujenga mahakama bora ambayo huamua haki.
Leo nazungumzia nguzo ya pili ya amani ambayo ni haki. Haki inawezekana ikawa na tafsiri kadhaa katika matumizi ya jumuiya za dini, siasa, utawala, mila hata sheria. Lakini haki bado ina maana na chimbuko lake moja tu.
Haki ina historia ndefu tangu kuumbwa kwa binadamu wa kwanza. Hii ina maana haki imetokana na Muumba mwenyewe ambaye ni Mwenyezi Mungu. Kutokana na ongezeko na maendeleo ya binadamu duniani ndipo tunapoanza kupata tafsiri mbalimbali ya haki.
Padri Vic Missiaen anasema; “Haki za watu hazikuwekwa na kanisa wala serikali bali ni matakwa ya Mungu, na ndani ya mpango wake ya kwamba kila maisha yapate haki na wajibu wake kwa kadiri ya stahili kutokana na asili yake ya ubinadamu”(Uk. 4 kijitabu: Mafundisho ya kanisa kuhusu jamii).
Katika Qur’an Takatifu, Suratul Asr (103:1-3) inasema “Naapa kwa zako (ewe Nabii Muhammad) kuwa binadamu yuko khasarani. Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira (kustahimiliana).
Dhamira yangu si kutoa funzo kuhusu haki. Kwa sababu si mwanagenzi wala mudir wa haki na sheria katika moja ya jumuiya nilizozitaja, ambazo ndizo zenye dhamana ya kufundisha, kufafanua, kusimamia na kutekeleza haki kwa jamii husika.
Bali taaluma yangu ya uandishi wa habari na uzalendo wangu katika nchi hii, ndivyo vinavyonichochea kuandika kuelimisha na kukumbusha mambo ya haki kwa lengo la kuenzi na kudumisha amani. Hii ni haki yangu.
Kwa tafsiri nyepesi na sahihi, haki ni jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho. Kwa maana nyingine ni uendeshaji wa jambo kufuatia sheria au kanuni zilizowekwa sahihi na insafu.
Wajibu wa mwalimu ni kufundisha, baada ya kufundisha anastahili ujira, ujira huo ndiyo haki yake. Anayeanza uchokozi anastahili kupigwa. Kipigo atachopata ndiyo haki yake. Anayefanya uhalifu anastahili hukumu. Hukumu hiyo ndiyo haki yake.
Dhuluma ni adui mkubwa wa haki na amani. Dhuluma ni tendo lisilo la haki; ni uenevu. Unapodhulumu maana yake ni kufanya isiyo haki, onea, tesa, taabisha, thakilisha, nyang’anya haki au mali.
Kila siku vyombo vya habari vinaibua, vinatangaza na kuhabarisha umma wa Watanzania kuhusu matendo mbalimbali ya uonevu, thakilisha na unyang’anyi yanayotendwa na viongozi wasio waadilifu dhidi ya wananchi na mali zao.
Sina haja ya kurudia kutaja mfano hai kwa sababu maovu yako bayana. Hakuna Mtanzania atakayejifanya eti ni Lila na Fila! Kuhusu matendo hayo. Isipokuwa wapo Watanzania wanafiki na wazandiki katika matendo hayo. Watu hao ndiyo wanaojitia upurukushani.
Ni vema na busara kwa viongozi na wananchi turudi kwenye asili yetu ya utu, umoja na upendo. Kurudi kwenye asili yetu kutarejesha, kutaboresha na kutaimarisha amani. Kwani vurugu na ghasia zinazotokea Geita, Zanzibar, Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam, Mtwara, Arusha na sehemu nyinginezo nchini, zinatokana na kupuuza ukweli, kuikataa haki na kuutupilia mbali uzalendo.
Ndiyo maana hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika rasimu yake ya katiba mpya, kati ya mambo muhimu yaliyopendekezwa na kuwekwa ndani ya katiba hiyo ni Misingi Mikuu ya Taifa, Tunu za Taifa na Maadili ya Viongozi.
Kuhusu Ibara ya Misingi Mikuu ya Taifa, Tume imependekeza misingi saba ambayo ni uhuru, haki, udugu, amani, usawa, umoja na mshikamano. Kuhusu Tunu za Taifa (National Values), Tume imependekeza utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa, yaani Kiswahili.
Kwa upande wa Maadili ya Viongozi, Tume imependekeza Katiba Mpya iwe na ibara inayoelezea tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili kwa viongozi wanaovunja miiko ya uongozi. Mambo yote hayo yana shabaha ya kustawisha amani chini ya nguzo za kweli na haki.
Nakamilisha makala ya leo kwa kumnukuu mwanafasihi na mshairi gwiji na maarufu wa lugha ya Kiswahili katika Afrika Mashariki na Kati, Shaaban Robert.
“Maisha ni magumu kwa mtu ambaye hana rafiki, na mapendeleo ya chuki kwa mtu ni sawa na mapendeleo ya wazimu. Mapenzi ya haki hufanya maisha kuwa matamu, hasa ikiwa haki yenyewe mtu huweza kuifahamu na kuisadiki.
“Huwezi kuijua haki pasipo kuitenda, na watu wengi hawawezi kufaulu kwa sababu ya ujinga kama huu. Haki ni kitu ambacho hujiendesha katika dunia bila huzuni, na watu ambao huipenda huwa madhubuti kwa sababu ni wazima au wamekamilika.
“Haki na kweli ni sawa na watoto pacha, mtu na awe na wingi wa akili wa kushinda mchwa, lakini iwapo ana mazoea ya kutupilia mbali mambo mawili haya, basi anafanya ujinga ulio mkubwa kabisa wa fikira na fahamu.” (Uk. 41 kitabu: Kielezo cha fasihi).
Itaendelea