Nchi ya Marekani, sasa inataka polisi wa Kenya waliotumwa nchini Haiti kwenda kusaidia idara za usalama za nchi hiyo kukabiliana na makundi yenye silaha, kigeuzwe na kuwa kikosi kamili cha kulinda Amani cha umoja wa Mataifa.
Pendekezo hili licha ya kuungwa mkono na nchi washirika wa Marekani ikiwemo Uingereza, linapingwa vikali na Urusi pamoja na China.
Kwa mujibu wa Serikali ya Marekani, kukifanya kikosi kilichoko sasa hivi Haiti kuwa na uwezo wa kukabiliana na makundi hayo, kutasaidia kurejesha haraka utulivu pamoja na kuzilazimisha nchi wanachama kuchangia fedha na vifaa kwa wakati.
Operesheni ya kurejesha utulivu kwenye taifa hilo, ambayo inaongozwa na Kenya, imekumbwa na sintofahamu hasa kutokana na kukosekana kwa fedha na vifaa vya kisasa kuyakabili makundi ya majambazi ambayo yameendelea kutatiza usalama.Haiti ambayo kwa sasa inaongozwa na baraza la mpito haina rais wala bunge, hali inayochangia makundi yenye silaha kutumia mwanya huo kujitanua kwenye miji mbalimbali ambapo sasa wanadhibiti karibu asilimia 85 ya jii kuu la Porto au Prince na kukosekana kwa kikosi imara kuwadhibiti, kunaitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro Zaidi.
Mpaka sasa Kenya imetuma polisi 400 pekee kati ya elfu 2 na 500 waliotarajiwa kutumwa wakati mpango huu ukiridhiwa na umoja wa Mataifa mwaka uliopita.