Na Helena Magabe,JamuhuriMedia, Musoma
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umma (HAIPPA PLC), Boniphance Ndengo amewaeleza waandishi wa habari kuwa amegundua wakulima ni wanunuaji wazuri wa hisa kupitia kampuni ya Umma ya HAIPPA PLC ambayo makao yake makuu ni Musoma Mjini mkoani Mara.
Hayo ameyasema jana kwenye semina ya uwekezaji na uzinduzi wa HAIPPA PLC mkoani Mara kuelekea mkutano mkuu utakaofanyika Januari 30, 2025 katika uwanja wa Mkendo Musoma mjini na baada ya hapo kuendelea kufanya semina kwenye matawi yake nchi nzima ambapo lengo likiwa ni kuwekeza angalau kwa Watanzania 6,000,000 kushiriki uwekezaji mkubwa kupitia kampuni za umma na miradi ya PPP.
Ndengo amesema kuwa HAIPPA PLC ni kampuni ya umma na iliyosajiliwa na BRELA ambayo ilianzishwa Oktoba 27, 2022 na kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2025 tayari imeshauza hisa 380,000 huku wateja wake wakiwa ni wakulima, wajasiliamari, watumishi wa Serikari , wenye ulemavu , vijana pamoja na mtu mmoja mmoja.
Amesema kampuni hiyo ilianza ikiwa na watu 8 ambapo kwa sasa ina watu zaidi ya 400 ,malengo ni kuanzisha kampuni za umma angalau 50 kwa ajili ya viwanda huku ikiwa imekusudia kuzifikia Halmashauri zote za Mkoa Mara kwa kubuni miradi, biashara, pamoja na uwekezaji mkubwa kwa Tanzania na Afrika ili kukuza kipato cha Mtanzania kufikia 2028 mwekezaji wa HAIPPA atoke kwenye wastani wa shilingi 3,000,000 kwa mwaka hadi 30,000,000 kwa mwaka.
Mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo alikuwa ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mara (MRPC) na Mkurugenzi wa Gazeti la Sauti ya Mara , Mara online news pamoja na Lake zone watch, Mugini Jacob, ambapo amesema Mkoa wa Mara una rasilimali nyingi zinazohitaji uwekezaji hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza fursa hizo ili kampuni ya uwekezaji ya HAIPPA iwe mfano bora mkoni Mara.
Amesema Mkoa wa Mara hivi sasa inakuwa kwa kasi na kubadilika kila wilaya hivyo kupitia fursa nyingi zilizopo mkoani Mara anawaomba wananchi kutumia HAIPPA kununua hisa zao kwa lengo la kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.
Mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe Timothy Itembe ameipongeza HAIPPA kwa namna ambayo imedhamiria kusimama na wakulima pamoja na wadau wengine mbalimbali ni kuhakikisha kuwa Mkoa wa Mara unakua kiuchumi kupitia uwekezaji unaofanywa na taasisi mballimbali kama HAIPPA.
Ameongeza kuwa kitendo cha Serikaki kufungua fursa za uwekezaji imesaidia kuongeza kasi ya maendeleo kupitia kwa mashirika, kampuni mbalimbali hivyo ni vyema kuziunga mkono taasisi ama kampuni zilizoonyesha nia ya uwekezaji na si kufaidika kwa baadhi ya watu kutokana na uwekezaji huo.
“Rais wa Marekani Donald Trump yupo sahihi kuiondoa WHO kwani amebaini kuwa hata fedha za afya zilizokuwa zikiingia nchini katika Mkoa wa Mara nyingi zinaishia mifukoni kwa watu wachache” amesema.