Ule usemi kuwa ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni nadhani una mantiki. Duniani mishangao inatokea kila leo. Nani alifikiria mwanasiasa kama Nape Nnauye atakuja kuomba msamaha? Kwa kosa lipi? Na kwa dhamira gani?
Mimi nilipigwa butwaa pale jioni Jumanne ya Septemba 10, mwaka huu wakati naangalia taarifa ya habari saa 1 usiku nikamwona Mheshimiwa Nape akitembea katika ile njia ya waenda kwa miguu pale Ikulu kutokea langoni mpaka ndani ya Ikulu.
Mara nikamwona anakaribishwa na Mheshimiwa Rais, wanatabasamu, wanazungumza wanapeana mikono. Ohoo! lilikuwa ni jambo la faraja sana. Hivi ipo nchi, mahasimu wakaweza kuchati namna Watanzania tunavyofanya?
Kule Kusini tuna neno moja la kukatisha tamaa, tunasema “athubutu!” kwa kumaanisha haiwezekani asilani au kamwe haiwezekani.
Hapa bongo, jamani kila kitu kinawezekana na ndivyo ilivyotokea. Mwenyekiti wa CCM kwa karama zake alizojaliwa na Mwenyezi Mungu ametumia maneno haya, “…Nape alikuwa anazungumza kauli moja ya …naomba Baba unisamehe…Mimi nimemsamehe tena kwa dhati…unaweza kuona kabisa huyu mtu anaomba msamaha na leo kaniomba aje kuniona na saa nyingine wasaidizi wangu wamekuwa wakinipa hizo habari…”
Pamoja na kuzungumza mengi wawili hawa pale Ikulu, Rais alisisitiza kusema, “…Inauma kusamehe, kunaumiza, lakini nasema kwa dhati kabisa nimemsamehe kabisa na ameeleza yaliyokuwa yanayomsibu…”
Sasa Watanzania tunajifunza somo gani katika tukio hili na mengine ya namna hii? Kwamba wapo watu, wenye vilema vyao hapa duniani na wapo watu wenye karama kubwa sana hapa duniani. Na nchini Tanzania wapo watu wa aina zote hizo.
Mei, 1962 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kujua huo upungufu wa kibinadamu miongoni mwa wanachama wa TANU, alituandikia kijitabu kiitwacho “TUJISAHIHISHE”.
Mle Mwalimu alisema wazi na nukuu, “…Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia Umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumini yake. Baadhi ya matatizo wapatayo binadamu yanatokana na Unafsi, Woga, Kutojielimisha na kosa jingine kubwa ni KUWAGAWA WATU KATIKA MAKUNDI na kadha wa kadha. (Nyerere: TUJISAHIHISHE uk. 1,3,5 na 8).
Sikusudii kuyataja yale makosa aliyotaja Mwalimu Nyerere; bali hapa nataka tu niunganishe tukio hili la Mheshimiwa Nape kuomba msamaha na tabia ya Rais Magufuli kufuata kikamilifu maneno ya Biblia Takatifu juu ya msamaha.
Kwanza kabisa Rais Magufuli ni muumini wa madhehebu Katoliki na daima anasali ile sala aliyotufundisha Bwana (BABA YETU) katika Mathayo Sura ya 6 aya ya 12. Ndiyo maana anasema “…Mimi nikiendelea kushikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe saba mara sabini…” Rais amefuata maneno ya Yesu katika Mathayo sura ile 18 mstari wa 22 pale Yesu alipomjibu Petro, “…Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini (Mt. 18:22).
Sasa hapa duniani tupo wenye vilema wengi tu – vilema wenyewe ni kama kiburi, majivuno, woga, usengenyi. Waingereza wanaita“VICES”. Huo ni upungufu wa kibinadamu. Lakini wapo pia watu vilema namna hii wenye karama zao. Hizo ni kama Unyenyekevu, Huruma, Upole, Msamaha na kwa Kiingereza wanaita “VIRTUES”. Kwa kuwa na unyenyekevu mtu unavunja kabisa kile kilema cha majivuno, kujiona, kujifikiria –“umimi”, hapo ndipo unaweza kuwa na nguvu za kuomba radhi au msamaha kwa mwenzako.
Wale wote wenye ushupavu wa kukishinda kiburi cha unafsi ndio wanaweza kuwa na nguvu za kuomba msamaha, na si vinginevyo.
Nafikiri Mwalimu alipoandika kijitabu kile “TUJISAHIHISHE” alitaka Watanzania tuwe na nguvu ya kujibadilisha, tuweze kujenga umoja wa kitaifa. Haya makundi ndani ya vyama ni alama ya kosa lile lile la ubinafsi, mara kujiita “SISI” na wengine eti ni “WAO”. Hilo linaleta mgawanyiko kwa msingi wa itikadi, dini, kabila na hata rangi ya mtu ambavyo vinavuruga umoja wa watu wowote wale.
Rais amefungua mikono yake wazi kuwapokea mara moja wote wenye kujiona wana imani ya umoja wetu. Usengenyi ni kilema kikubwa sana, fitna na makundi huzaliwamo.
Maneno ya Nape yanaonyesha ukomavu wa kifikra na maadili. Kalelewa na Youth League (Umoja wa Vijana) ndio maana aliweza kutamka “…Yaliyotokea ni mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM, mwanaye, niliona ni vizuri nije niongee na baba yangu…” Jambo hili si la kawaida katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo nimeona niandike machache kumsifu mjukuu huyu Mheshimiwa Nape (mtoto wa Kanali Moses, Mmakonde wa Nyangamara kule Kusini) kwa vile moyo wake umekuwa na ushupavu kwenda kwa baba kuomba msamaha. Wakristo tunajua vema ile hadithi ya mwana mpotevu. Pale tunayakuta maneno haya “…Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia; Baba, nimekosa…Ataondoka akenda kwa babaye.” (Luka 15 mstari wa 18). Na alivyofanya Mheshimiwa Nape, Septemba 10, 2019 hii ndivyo aliondoka, akaenda Ikulu kwa baba.
Hii kwangu si mara ya kwanza kusikia viongozi wa chama tawala wanawasamehe wale viongozi walioteleza. Huko nyuma miaka ya 1958 – 1960 kulitokea na kigogo wa TANU alikiuka maadili, tunasema alikengeuka akamdharau hata Rais wa TANU na akahamia UTP.
Baada ya kutafakari akajutia kosa lake akapiga moyo konde na kuomba msamaha. Rais Mwalimu Nyerere alimsamehe na hata akampa kazi kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1964.
Mfano mwingine ni vigogo wa TANU kwa kushirikiana na mwanajeshi mwenye cheo cha Kanali, walijaribu kumwangusha Mwalimu. Wakabambwa na kumfikisha mahakamani kwa kesi ya uhaini na watatu wakahukumiwa vifungo gerezani mwaka 1969.
Baada ya muda, Mwalimu Nyerere kwa ule moyo wake wa huruma akawasamehe na wote wakatoka gerezani na wengine akawapa kazi katika mashirika.
Lakini mifano yangu ni misamaha ile ya Mwalimu Nyerere. Ni tofauti na staili hii ya leo pale Rais Magufuli anaongea ana kwa ana na Mheshimiwa Nape. Wanashauriana, anamwelimisha na kumlea kibaba ndiyo maana ninasema “haijapata kutokea” namna hii! Ni staili mpya hii kabisa.
Mtu akisoma yale maneno ya mwisho katika ibara ya mwisho katika kitabu cha Mwalimu “TUJISSAHIHISHE” atakuta Mwalimu aliandika hivi, “Nimejaribu kuelezea makosa machache ambayo yafaa tuyaondoe na kuyaepuka katika Chama chetu. Sitaki mtu yeyote afikiri kuwa mimi niliyeandika maneno hayo sina makosa hayo. Hiyo si kweli. Kosa moja kubwa sana ambalo pia linatokana na unafki ni kutaja makosa ambayo sisi wenyewe hatunayo na kuficha makosa ambayo sisi wenyewe tunayo. Hili kosa lile lile linatufanya tulaumu tusiowapenda na kutolaumu tunaowapenda bila kujali ukweli.
Nimetaja makosa haya ili yatusaidie siyo katika kuwahukumu wenzetu tu, ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi” (Nyerere: TUJISAHIHISHE uk. 10 ibara ya mwisho)
Basi, kwa wale wote wanaojitambua upungufu wao baada ya kujitafiti na kutafakari kwa kina, kuamua kuomba msamaha ni kuonyesha moyo wa ushupavu. Woga unakutia fukuto moyoni mwako -mtu unakosa raha na unaishi kwa wasiwasi. Kukomaa kiimani ni kuwa muwazi na mkweli.
Nilipendezwa sana na yale maneno yao ya mwisho mwisho katika mazungumzo yale pale Ikulu. Wote wawili walionekana kuwa na nyuso za furaha na bashasha. Ilishangaza hasa kumwona Mheshimiwa Rais akimsindikiza mgeni wake mpaka pale mlangoni kumwona Mheshimiwa Nape anaingia kwenye gari huku wakipungiana mikono kwa kicheko. Ukisha kusamehe bwana moyo unakuwa na furaha ya ajabu. We jaribu kusamehe uonje raha hiyo.
Hii ndiyo Tanzania yetu – nchi ya umoja, furaha amani na upendo. Siyo jambo la kawaida kuona tukio namna ile. Waingereza wanasema, “Happiness Is The Tranquility To The Mind” yaani wanamaanisha furaha ni “ridhaa ya moyo”.
Mafindofindo moyoni, au fukuto la chuki au gubu la aina yoyote mtu kamwe huwezi kuwa na hiyo ridhaa ya moyo, wala hupati usingizi tunaoita wa fofofo!
Sisi Wakatoliki tuna kitu tunaita Sakramenti ya Upatanisho. Hii sakramenti bwana inataka unyenyekevu, unajitafiti makosa yako halafu unaamua kwenda kuomba msamaha kwa Muumba wako.
Kwa vile Rais ni muelewa wa sakramenti hii ya upatanisho alikubali mara kumkaribisha Mheshimiwa Nape pale Ikulu ampe nafasi ya kutamka hilo ombi lake la kutaka asamehewe. Rais alisikika akisema, “Lakini nimemsamehe huyu, bado ni kijana mdogo na ana ‘future’ nzuri katika maisha yake…”
Hili jamani halijapata kutokea hapa nchini! Sote tunapenda AMANI na FURAHA, basi tuishi kwa amani na furaha hiyo. Usiposamehe na hutasamehewa kwa maana mkisamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa Mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. (Mathayo Sura ya 6 mstari wa 14-15). Watanzania tushike ule ushauri wa Baba wa Taifa aliotuasa katika kijitabu chake kile cha “TUJISAHIHISHE”.
AMINA