Mzee Ali Hassan Mwinyi amepata kusema kila kitabu na zama zake. Kuanzia uongozi wa Awamu ya Kwanza hadi sasa Awamu ya Sita, yapo mambo yanabadilika kulingana na kiongozi aliye madarakani.
Haiwezekani staili ya kiongozi mmoja ikafanana au ikatofautiana kwa asilimia mia na ya kiongozi mwingine. Tumekuwa na viongozi waliokuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, pia tumekuwa nao wasiotaka kuwasikia.
Rais Samia Suluhu Hassan, kama walivyo watangulizi wake, hatutarajii arithi, au aache yote yaliyotendwa na watangulizi wake. Ana utashi wa kuendelea au kutoendelea na yote au baadhi.
Pamoja na haki na mamlaka aliyonayo, kuna ‘mila na desturi’ fulani zilizoibuliwa na mtangulizi wake ambazo ninadhani hakuna sababu ya kuendelea nazo. Iko hivi, kabla ya Rais Magufuli, Watanzania wengi hatukumjua shushushu mkuu wa nchi. Alivyokuja Rais Magufuli, sidhani tena kama wapo wanaopata tabu kumtambua mtu anayeshika madaraka hayo nyeti. Inawezekana ndiyo u-sasa, kwani zamani zile tuliambiwa shushushu hapaswi kujulikana kwa sura, seuze shushushu mkuu?
Lakini pia ni wakati wake ambako tulishuhudia hafla kubwa kubwa na za kawaida kabisa zikiwashirikisha viongozi wote wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Wote, kuanzia JWTZ, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Zimamoto, nk. wamekuwa wakishiriki shughuli nyingi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Si hivyo tu, bali viongozi wa mihili ya Bunge na Mahakama nao wamekuwa hawakosi kwenye hafla hizo. Hawa ni mbali na makamu wa rais, waziri mkuu, mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na kadhalika.
Nini maana ya kuwa na wakubwa wote hawa hata kama hafla yenyewe machoni mwa wengi ni ya kawaida? Kuna faida gani kiitifaki za kuwapo kwa wazito wote hawa kwenye tukio ambalo si kuuuubwa ki-hivyo? Je, Rais huwaleta wakubwa hawa kwenye hafla ili kuonyesha nguvu na mamlaka aliyonayo katika nchi? Je, ni vitisho? Ni ufahari? Ni Uafrika? Kwa mtazamo wangu ingependeza wakuu hawa wakahudhuria hafla ambayo inahusu taasisi mojawapo katika hizo.
Pamoja na wakuu hao kuitwa kwenye hafla, baadhi yao hupewa nafasi ya ‘kusalimia’. Tumeona na kusikia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Jaji Mkuu, mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi na kadhalika wakipewa muda wa ‘kutoa salamu’. Baada ya wote hao kumaliza, Rais hukaribishwa ili naye ‘awafunde’.
Ndiyo, kufunda ni jambo muhimu, lakini ninadhani kufunda kuzuri zaidi ni kama vile alivyofanya siku alipowaapisha wakuu wa mikoa. Aliwapeleka pembeni, akawapa aliyowapa.
Hapa kwenye ‘kutoa salamu’ kunaweza kufanyiwa marekebisho. Mosi, ni ‘matumizi mabaya’ ya muda. Muda unaotumiwa kwenye hotuba hizi za utambulisho na salamu ni mwingi, na kwa kweli hakuna sababu ya kufanya hivyo kwenye kila shughuli. Kwenye hafla ambayo mgeni rasmi ni Rais, inapendeza waliohudhuria na hadhira iliyo mbali wamsikilize Rais anasema nini. Alipo Rais, jicho na kiu ya wasikilizaji ni kumsikia Rais anasema nini. Na hata Rais mwenyewe sioni sababu ya yeye kuzungumza kila kwenye hafla, hasa hizi za kuapisha.
Kuwepo utamaduni wa watu kuwa na kiu ya kujua ‘leo Rais atazungumza nini’. Watu wafikie hatua ya kuwa na shauku ya kumsikia Rais kwa matarajio ya kupata kitu tangible. Ifike hatua mwananchi akisikia sauti ya Rais aache shughuli nyingine, amsikilize.
Ninashauri hafla chache ndizo viongozi wapewe nafasi ya kuzungumza, hasa wasaidizi wa Rais. Hiyo itasaidia kuondoa kasoro kama zile za wasaidizi kujisahau na kutoa amri na maelekezo kana kwamba wao ndio wenye mamlaka ya uongozi wa nchi.
Kwa upande wa vyombo vya habari, mahali alipo Rais, habari ni rais. Wasaidizi wake hata kama wana maneno matamu, hayawezi kupewa kipaumbele na kumwacha rais…sana sana watapewa nafasi endapo watafanya kituko!
Ushauri wangu, Rais apunguze kuwaita wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa baadhi ya hafla zake za kawaida. Pili, utaratibu wa kuwapa nafasi viongozi ‘kusalimia’ kwenye hafla utazamwe ili nafasi ya rais ibaki kuwa ni ya pekee. Iwe Rais akizungumza, basi amemaliza, siyo anazungumza tena kiongozi mwingine. Tatu, Rais aangalie hafla zipi azungumze, na zipi amalize anachofanya, aondoke aendelee na dhima nyingine za kitaifa.
Rais Samia ni msikivu, bila shaka ataona umuhimu wa kurekebisha baadhi ya mambo kama haya ya kuwa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kila anapokuwa na hafla. Yeye ni Amiri Jeshi Mkuu. Sisi wananchi wake tunatambua na kuheshimu mamlaka yake bila hata kuwaona wakiwa naye.